Siasa

Hatimaye mahujaji waondoka

RAIS Jakaya Kikwete, alilazimika kuingilia kati yeye binafsi utata uliogubika safari ya mahujaji wa Kiislamu wanaofikia 1,500 waliokuwa wamekwama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam kwa siku kadhaa kabla ya kuanza kupata usafiri wa kwanza jana jioni.

Imeandaliwa na Mobin Sarya, Khadija Khalili na Mwanne Sekuru.


RAIS Jakaya Kikwete, alilazimika kuingilia kati yeye binafsi utata uliogubika safari ya mahujaji wa Kiislamu wanaofikia 1,500 waliokuwa wamekwama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam kwa siku kadhaa kabla ya kuanza kupata usafiri wa kwanza jana jioni.


Hayo yalibainishwa jana na Waziri Mkuu, Edward Lowassa wakati alipokwenda katika uwanja huo wa ndege kuzungumza na mahujaji hao ikiwa ni pamoja na kuwapa pole kwa tatizo lao hilo lililodumu kwa takriban wiki moja sasa.


Lowassa aliwaeleza mahujaji hao ambao walikuwa wameshaanza kukata tamaa ya kwenda Makka kuhiji kuwa, Rais Kikwete alikuwa akitarajia kukutana nao usiku huo huo wa jana, wakati akiwa njiani kuelekea Marekani kwa ziara ya kikazi.


Habari zaidi zilizothibitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro jana jioni, zilieleza kuwa ndege ya kwanza yenye uwezo wa kubeba abiria 397 iliyokodiwa na Shirika la Ndege la Tanzania (ATC) kutoka Kampuni ya Al-Wassan iliwasili uwanjani hapo majira ya saa 1.20 usiku.


Kandoro aliwahakikishia mahujaji hao kuwa ndege hiyo itawapeleka baadhi ya mahujaji na kurejea tena leo asubuhi ili kuwafuata mahujaji wengine wanaotoka katika nchi jirani za Comoro na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambao nao wamekwama uwanjani hapo.


Alisema kuwa pamoja na ndege hiyo, pia serikali ilikuwa imekodi ndege nyingine mbili, moja ikiwa ni kutoka Ureno na nyingine Hispania na kuwa mamlaka husika zilikuwa zikifuatilia vibali vya ndege hizo kutua Jeddah.


Alisema iwapo vibali hivyo vitapatikana, ndege hizo, ambazo kila moja ina uwezo wa kuchukua abiria 370, zingewasili Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo ambayo ndiyo siku ya mwisho ya kuwasili Mji Mtakatifu wa Makka.


Kandoro alisema serikali iliamua kuchukua hatua hiyo ili kuokoa jahazi baada ya kubainika kuwa, hali imekuwa ngumu kwa ATC kuweza kuimudu peke yake.


Hata hivyo, alisema kuwa ATC itawajibika kuirejeshea serikali gharama za kukodi ndege hizo mbili zilizokodiwa kutoka Kampuni ya Al-Zahra Air.


Wakati huo huo, ilielezwa kuwa mahujaji kadhaa, ambao tangu Jumapili jioni waliingia ndani ya jengo la kusubiria ndege baada ya kuelezwa kuwa ndege itakayowasafirisha ipo njiani, walikuwa katika hali mbaya jana kutokana na kukosa huduma muhimu za kijamii ndani ya jengo hilo.


Taarifa ambazo Tanzania Daima ilizipata kutoka uwanjani hapo zinaeleza kuwa, wanawake ndio waliokuwa katika hali mbaya zaidi, kwani kwa muda huo wote walikuwa wakikosa fursa za kuwatosheleza kuoga na kubadili mavazi kutokana na kutokuwepo mabafu ya kutosha ndani ya jengo hilo.


Hayo yalielezwa na mmoja wa viongozi wa taasisi ya Hajji Trust, Juma Abdallah ambaye alisema kuwa ubinadamu ulipaswa kuangaliwa zaidi katika suala hilo, kwani watu wanateseka bila sababu za msingi.


Wakati huo huo, baadhi ya mahujaji waliliambia gazeti hili jana uwanjani hapo kuwa, kwa sababu ya kukaa uwanjani hapo kwa muda mrefu, wamejikuta wakiishiwa fedha za matumizi hata kabla hawajaondoka kwenda kuhiji.


Khadija Mgambo, ambaye hakujitambulisha safari yake inaratibiwa na taasisi gani, alisema katika suala hilo, wanajiona kuwa wamedharauliwa.


Alisema kitendo cha kuwalaza sakafuni kwa muda wa wiki nzima uwanjani hapo, kimewafanya waonekane kama wakimbizi.


“Licha ya kucheleweshwa kuhudhuria katika ibada hiyo takatifu, lakini pia tumesikia hatutaweza kurudishiwa pesa zetu ambazo tumetoa kwa ajili ya ibada ambayo hatukuweza kufanikiwa kwenda hadi sasa,” alisema mama huyo jana jioni.


Hujaji mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Seifullah alisema kuwa wanatambua kwamba serikali haina dini, lakini wananchi wake ndio wenye dini, hivyo rais na viongozi wengine wote walipaswa kuwasaida kwa njia yoyote ile ili hali waweze kuungana na wenzao kuhudhuria ibada hiyo.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents