MichezoUncategorized

Hawa ndio wachezaji 10 wa soka duniani waliozitengenezea timu zao faida kubwa

Mchezo wa soka kwa sasa umekuwa ukiwatajirisha zaidi wachezaji katika kipindi kifupi tofauti na ilivyokuwa zamani. Hawa chini ni wachezaji 10 ambao walisajiliwa kwa kiasi kidogo cha fedha na baadae waliuzwa kufedha nyingi zaidi.

Neymar

Mchezaji huyu alinunuliwa na Barcelona mwaka 2013 akitokea klabu ya Santos ya Brazil kwa kiasi cha paundi milioni 49. Hata hivyo katika kipindi cha usajili wa majira ya joto msimu huu Barca ilijikuta ikitengeneza faida kubwa zaidi ya kiasi cha paundi milioni 149 baada ya kumuuza mchezaji huyo kwenda PSG kwa ada ya uhamisho wa paundi milioni 198.

Philippe Coutinho

Kiungo huyu kutoka Brazil alisajiliwa na Liverpool mwaka 2013 akitokea Inter Milan kwa kiasi cha paundi milioni 8.5. Ikiwa ni misimu takribani mitano imepita akiwa na klabu hiyo ya uingereza, siku chache zilizopita Coutinho amesaini mkataba wa miaka mitano wa kuichezea Barcelona kwa ada ya uhamisho wa paundi milioni 145. Katika usajili huo Liverpool imefanikiwa kutengeneza faida ya paundi milioni 136.5.

Paul Pogba

Katika msimu uliopita mchezaji huyu aliweza kuweka rekodi ya dunia katika usajili ya paundi milioni 89 akitokea Juventus. Awali mchezaji huyu aliwahi kuchezea Manchester United kabla ya kuondoka kama mchezaji huru katika msimu wa mwaka 2012 na kutua Juventus ambapo alicheza kwa zaidi ya miaka minne. Kupitia Pogba Juve imeweza kujitengenezea faida ya kiasi hicho hicho cha cha paundi milioni 89 kwa kuwa haikutoa fedha yoyote wakati wa kumsajili.

Ousmane Dembele

Ousmane Dembele kabla ya kutua Barcelona mapema msimu huu katika majira ya joto alikuwa anacheza Borussia Dortmund ambayo ilimsajili kwa kiasi cha paundi milioni 13.5 akitokea Rennes ya Ufaransa. Mwaka mmoja baadae Dortmund wameweza kumuuza mchezaji huyo kwa vinara wa La Liga [Barcelona] kwa kiasi cha paundi milioni 94.5. Kutokana na biashara hiyo Borussia ilifanikiwa kutengeneza faida ya kiasi cha paundi milioni 81.

Gareth Bale

Huyu ni mchezaji mwengine ambaye amewahi kushikilia rekodi ya mchezaji aliyesajiliwa kwa fadha nyingi zaidi akitokea Tottenham Hotspurs na kutua Madrid kwa kiasi cha paundi milioni 86. Tottenham ilimsajili mchezaji huyo mwaka 2007 akitokea Southampton kwa kiasi cha paundi milioni 10. Miaka sita baadae Spurs ndio ilifanikiwa kumuuza kwa Madrid na kutengeneza faida ya paundi milioni 76.

Cristiano Ronaldo

Mchezaji huyu bora wa dunia kwa mara tano, alisajiliwa na Manchester United mwkaa 2003 akitokea Sporting Lisbon ya Ureno kwa kiasi cha paundi milioni 17. Ronaldo aliweza kuichezea United kwa misimu sita na mwaka 2009 Real Madrid waliweza kuweka rekodi ya dunia kwa kumsajili kwa kiasi cha paundi milioni 80. Katika biashara hiyo Man United iliweza kutengeneza faida ya kiasi cha paundi milioni 63.

Virgil Van Dijk

Huyu ni mmoja kati ya mabeki ambao amezitoa ulimi nje timu nyingi kubwa za Uingereza kuanzia msimu uliopita. Beki huyo ambaye ni raia wa Uholanzi alisajiliwa na klabu ya Southampton mwaka 2015 akitokea Celtic. Kubwa lililowashangaza mashabiki wengi wa soka duniani ni kiasi cha paundi milioni 75 ambacho Liverpool wamekitoa katika dirisha hili dogo la usajili msimu huu kwa ajili ya kumnyaka beki huyo. Usajili wa Dijk kwenda Liverpool umeifanya Southampton kuingiza faida ya kiasi cha paundi milioni 62.

Luis Suarez

Suarez anakumbukwa sana na mashabiki wa Liverpool kutokana na mchango wake ambao ameutoka katika klabu hiyo. Liverpool walimsajili mchezaji huyo mwaka 2011 kwa ada ya uhamisho wa paundi milioni 22.8 akitokea Ajax. Hata hivyo baada ya kupita takribani miaka mitatu na nusu alisajiliwa na Barcelona kwa kiasi cha paundi milioni 75 ambapo kuliifanya Liverpool kutengeneza faida ya kiasi cha paundi milioni 52.2.

Zinedine Zidane

Ukiulizwa miongoni mwa makocha waliopata mafanikio makubwa katika kipindi kifupi tena wakiwa na umri mdogo hutaacha kuumtaja Zinedine Zidane. Kama Zidane kwa sasa ndio angekuwa anacheza soka basi aneweza kusajiliwa kwa mamilioni mengi ya fedha kutokana na kipaji chake alichobarikiwa. Juventus iliwahi kufanikiwa kumyakuwa mchezaji huyu mwaka 1996 kwa kiasi cha paundi milioni tatu akitokea Bordeaux. Hata hivyo baada ya kuchezea timu hiyo kwa misimu mitano Zizou alinyakuliwa na Real Madrid kwa kiasi cha paundi milioni 48. Katika usajili huo Juventus waliweza kutengeneza faida ya paundi milioni 45.

Romelu Lukaku

Romelu Lukaku ambaye ndio mfungaji bora wa timu ya taifa ya Ubelgiji, alisajiliwa na Everton mwaka 2014 baada ya kuichezea timu hiyo kwa mkopo wa mwaka mmoja akitokea Chelsea. Katika usajili huo Everton waliilipa Chelsea kiasi cha paundi milioni 28. Msimu huu Manchester United walifanikiwa kumsajili mshambuliaji huyo kwa kulipa kiasi cha paundi milioni 75. Usajili huo wa Lukaku kutua man United uliifanya Everton kuingiza faida ya kiasi cha paundi milioni 38.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents