Habari

Hii ndio sababu ya mtoto wa Mfalme Prince William kutaka kukutana na Rais Magufuli

Hii ndio sababu ya mtoto wa Mfalme Prince William kutaka kukutana na Rais Magufuli

Mwanamfalme William wa Uingereza amepangiwa kukutana na rais wa Tanzania Dkt John Magufuli wiki ijayo wakati wa ziara yake ya siku saba Afrika,Mwana huyo wa mfalme anatarajiwa kuzuru pia Kenya na Namibia katika ziara hiyo ambayo si ya kikazi, Ziara hiyo itafanyika kuanzia 24 Septemba hadi 30 Septemba.

Kwa mjibu wa BBC Lengo kuu la mwanamfalme huyo litakuwa kufuatilia juhudi za kukabiliana na ujangili na uhifadhi wa wanyama. Prince William atafanya ziara hiyo katika wadhifa wake kama rais wa mashirika yanayotetea uhifadhi wa wanyama ya United for Wildlife na Tusk Trust. Amekuwa pia mlezi wa shirika la Royal African Society linalolenga kukuza uhusiano kati ya Afrika na Uingereza na hushiriki sana juhudi za kukabiliana na ujangili.

Akiwa ziarani Tanzania, Mtawala huyo wa Cambridge, atafanya mashauriano na Rais Magufuli kuhusu juhudi zinazopigwa na taifa hilo katika kukabiliana na ujangili na ulanguzi wa wanyama pori kwa mujibu wa shirika la habari la Press Association. Kadhalika, atazuru bandari ya Dar es Salaam kujifahamisha zaidi kuhusu juhudi zinazopigwa na taifa hilo. Moja ya malengo ya ziara ya Mwanamfalme William Afrika ni kupigia debe mkutano mkuu wa kukabiliana na ulanguzi wa wanyamapori ambao utaandaliwa jijini London kati ya 11-12 Oktoba.

Mkutano huo ambao kwa kirefu unafahamika kama Illegal Wildlife Trade Conference, unalenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na ulanguzi wa wanyamapori, kwa kuangazia mambo matatu makuu: ulanguzi wa wanyama, wadudu na mimea kama uhalifu, kujenga ushirikiano na kufunga masoko yanayotumiwa na wahalifu kulangua wanyamapori.

Taarifa ya Kensington Palace inasema ingawa atakuwa katika ziara ya kibinafsi, ameombwa na Malkia kutekeleza shughuli kadha rasmi kwa niaba yake.Akiwa nchini Kenya, Mwanamfalme William atatembelea kikosi cha wanajeshi wa Uingereza cha 1st Battalion cha Irish Guards Battlegroup.

William huwa na cheo cha kanali wa jeshi la Ireland, na anatarajiwa kujifahamisha ni jinsi gani wanajeshi wa Uingereza na Kenya wanafanya kazi kwa pamoja kuimarisha shughuli zao. Kikosi hicho cha Irish Guards Battlegroup hujumuisha wanajeshi wa Ireland na kundi la wanajeshi wa kenya ambao wamekuwa wakipokea mafunzo kutoka kwa kikosi cha jeshi la Uingereza.

Nchini Namibia, mtawala huyo anatarajiwa kukutana na makamu wa rais Nangolo Mbumba na pia ahudhurie hafla ya kusherehekea ushirikiano kati ya Uingereza na Namibia katika makazi ya balozi wa Uingereza nchini humo Kate Airey. Mwanamfalme William ameeleza wazi upendo wake kwa bara Afrika.

Aliomba posa kutoka kwa mkewe Kate Middleton wakiwa katika mgahawa mmoja wa porini karibu na Mlima Kenya mwaka 2010. Mwanamfalme William, 36, majuzi alipokuwa anakubali kuwa mlezi wa shirika la Royal African Society alieleza anavyolipenda bara hilo. “Nilianza kuipenda Afrika mara ya kwanza nilipokaa kwa muda Kenya, Botswana na Tanzania nikiwa bado kijana mdogo. Nilifurahia sana na nimekuwa nikitaka kurudi mara kwa mara kadiri iwezekanavyo tangu wakati huo,” alisema.

Mara ya mwisho kwake kuzuru Kenya ilikuwa mwaka 2016 ambapo alikutana na Rais Uhuru Kenyatta na kushauriana kuhusu usalama na uhifadhi wa wanyama. Wengi watasubiri kuona iwapo atasafiri na Catherine, Bintimfalme wa Cambridge. Amekuwa katika likizo ya uzazi tangu mwezi Machi alipojifungua mwanamfalme Louis. Lakini anatarajiwa kurejelea majukumu yake rasmi karibuni.

Wamejaliwa watoto wengine wawili, Mwanamfalme George, 5 na Bintimfalme Charlotte, 3. Mwanamfalme William ni wa pili katika orodha ya warithi wa kiti cha ufalme wa Uingereza baada ya babake Mwanamfalme Charles, Mtawala wa Wales.

 

By Ally Juma

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents