Burudani

Hizi ni sababu za kwanini Diamond ataendelea kufanikiwa zaidi

MUZIKI unachukua sehemu kubwa ya maisha yetu ya kila siku, umekuwa ukitupa faraja pale tunapoonekana kukata tamaa, ukitajiririsha ile furaha tuliyonayo katika nafsi zetu na kuturejeshea kumbukumbu za kitambo.

Basi muziki ni nini?. Muziki ni mpangilio ala na uimbaji unaoleta athari fulani kwa kiumbe, twende pole pole hapa, yaani naweza kusema kama msanii hawezi kupangilia ala na kuimba kwa ufundi hapo hakuna muziki. Tusimame hapo. Kwa hapa nchi muziki wa Bongo Fleva ndio umetawala sana ukilinganisha na aina nyingine za muziki. Bongo Fleva inasikika kila kona kuanzia majumbani, mtaani, mtandaoni, kwenye vyombo vya usafiri na vyombo vya habari.

Ukitaja majina matatu ya wasanii wanaofanya vizuri katika Bongo Fleva huwezi kuacha kumtaja Diamond Platnumz, kwa kipindi cha miaka saba aliyodumu katika muziki huu amekuwa na mchango mkubwa sana. Kwa miaka hiyo amekuwa akidondosha burudani ya uhakika, hakuwahi kusimama sehemu yoyote ile, ni yeye na kazi, kazi yeye, yaani bampa to bampa kama anavyoeleza Darassa katika wimbo wake wa muziki.

Sote tumekuwa mashuhuda wa mafanikio yake toka alipoanza, tumeshudia akibeba tuzo mbali mbali kama KTMA, AFRIMMA, MTV EMA na nyinginezo.

Kwanini leo Diamond?

Leo nimevutiwa kuandika makala haya mara baada ya msanii huyu kuanzisha wavuti ya kuuza nyimbo za wasanii ijulikanayo kama Wasafi.com. Hii ni hatua kubwa katika muziki wa Bongo Fleva.
Nadhubutu kusema ni hatua kubwa kwa sababu hakuna msanii mwingine aliyewahi kufanya hivyo, yeye ameiona hiyo fursa na kuamua kuifanyia kazi. Pongezi za kutosha kwake.

Mtandao huu unakuja kuleta ushindani mkubwa kwa mitandao kama Mdundo, Mkito na Muziki ambayo ilitangulia kufanya biashara hiyo. Wasanii ni wengi hadi sasa waliyokubali kuweka kazi zao katika mtandao huo. Nimemuona Prof Jay, Navy Kenzo, Barnaba, Kasimu Mganga, Harmonize, Billnas, Saida Karoli, Ray C, Belle 9, Chenge na Temba, Ben Pol na wengineo.

Ni wazi Diamond anazidi kujitunua kisanaa na kibiashara pia, kwa mantiki hiyo hakuna ubishi kuwa ataendelea kuwepo katika muziki huu kwa kipindi kirefu kutoka anafanya kazi na kundi kubwa la watu ambalo linahudumu katika ‘sekta’ ya muziki. Kwa hiyo usitengemee jamaa atashuka kimuziki miaka ya hivi karibuni, hilo sahau kwa sasa na ni vema ukaendelea na mambo mengine kuliko kukaa na kuwaza hilo. Narudia teno hilo sahau kwa sasa.

Mambo anayofanya ndiyo yanamfanya kuendelea kusalia juu. ‘Hakuna uchawi wala ndumba’ alijisemea Prof Jay katika wimbo wake wa Zali la Mentali. Kiufupi Diamond mwenye ametaka iwe hivyo.
Unawekeza kutoka moyoni Aliyekuwa mtangazaji wa redio na mwandishi wa vitabu nchini Marekani (1938-1946) Earl Nightingale aliinua mkono wake na kuandika maneo yasemayo “watu wenye malengo hufanikiwa kwa sababu wanajua kule wanakoelekea kimaisha.”

Wakati Diamond anaondoka Sharobaro Records kwa Bob Junior, sehemu iliyomtoa kimuziki alienda kuanzisha kitu kinaitwa ‘Wasafi’. Neno Wasafi lilikuwa likisikika kwenye nyimbo zake nyingi lakini wengi walizani zilikuwa mbwembe tu. Nani kakudanganya, tena nikupe pole sana. Diamond alikuwa akiishi katika maneno ya Earl Nightingale, alikuwa anajua anapoelekea na Wasafi hakuitaja tu bure, alijiona hapa alipo sasa.

Hakuna aliyetengemea kuwaWasafi itakuja kuwa lebo kubwa nchi ya kusamimia wasanii na kufanya biashara mbali mbali za muziki lakini ndilo tunaishi nalo kwa sasa. Kwani ameenda kwa mganga?, wee!, tena ishia hapo hapo. Siri ni moja tu, Diamond ni msanii aliyewekeza sana katika muziki wake, tunapozungumzia uwekezaji si fedha pekee bali hata muda.

Kuna baadhi ya wasanii wana uwezo mkubwa sana lakini wamekuwa wagumu kuwekeza, mikono yao imekuwa migumu kuzama mfukoni na muda wao mwengi umekuwa ukichukulia baadhi ya mambo yasiyokuwa na uhusiano wa moja kwa moja na muziki wao. Moja ya nukuu kutoka kwa Anna Kleimer ni ile inayosema, “fanya unachopenda, na penda unachofanya”. Hii kanuni rahisi sana ambayo inawezesha watu kufikia malengo yao. Kwa asilimia kubwa watu mwenye mafanikio makubwa dunia ni wale wanafanya yale wanayoyapenda kutoka ndani.

Diamond anapenda muziki wake ndio maana anamwaga fedha kuwekeza, kuna wasanii wanafanya uwekezaji mkubwa nje ya muziki wao na wamefanikiwa huko, si jambo baya lakini kufanya hivyo ni kumuhakikishia Diamond kuzidi kutawala Bongo Fleva kwa kipindi kirefu zaidi, wala hakuna uchawi.

Chukua hii kwanza

Kuna mambo huwa nikikumbuka naishia kucheka tu. Miaka kadhaa nyuma kulikuwa kunaripotiwa visa vya mganga fulani aliyekuwa akidai ni mganga wake ni Diamond. Mganga alikuwa akidai kuwa yeye ndiye aliyemtoa Diamond na mafanikio yake anahusika hata ushindi wa tuzo saba za KTMA mwaka 2015 anahusika. Sikumshangaa kwa sababu hii imeshakuwa ni tabia kwa baadhi yetu kuamini mtu anapofikia mafanikio fulani katika umri mdogo lazima kuna jambo nyuma ya pazia.

Kiufupi hatuamini katika juhudi binafsi. Sikuwahi kuamini katika maneno ya mganga yule, ila nilijua hata Diamond akitetea vipi hatu hawawezi kumuamini, lakini niliamini kuwa muda na juhudi zake ipo siku zitatupa jibu. Muda hutoa majibu ya baadhi ya maswali yanayoshindikani katika nyakati fulani. James Richardson raia wa Marekani alifungwa jela kwa kusingiziwa lakini baada ya kutumikia kifungo chake kwa miaka 21 ilibainika hakuwa na hatia hivyo akaachiwa huru.

Hivi ndivyo muda hutoa majibu yake. Sasa tunamuona Diamond katika ‘level’ za mbali zaidi kuliko kile kipindi cha hayo maneno, je yule mganga yupo wapi?, akiibuka tena leo wangapi watakaomuamini. Bila shaka jibu litakuwa ‘Acha maneno weka muziki.’ Ndiyo, hilo ndilo jibu pekee kwa sasa, kwani Diamond tunamuona jinsi anawekeza, anatengeneza ‘connection’ na watu mbali mbali wa ndani na nje na vile anavyobrand muziki wake. Tusimame hapo kwanza.

Biashara ni wateja

Biashara yoyote dunia inatengemea wateja ili iweze kujiendesha na kumletea faida yule anayeimiliki au kuisimamia. Biashara ya kuuza muziki kupitia mdandao wa Wasafi.com naiona ikimuugiza Diamond fedha nyingi kwa kuuza tu nyimbo zake binafsi kutokana na ‘fun base’ (followers) kubwa aliyonayo katika mitandao ya kijamii.

Diamond ndio msanii anayeongoza kufuatiliwa na watu wengi mtandaoni kwa hapa Bongo, watu zaidi ya milioni tano wanamfuatilia. Katika mtandao wa instagram ana watu milioni 3.4, twitter 363,000 na Facebook milioni 2.9 (takribani milioni tatu).

Idadi hii ya watu ndio inampa Diamond ‘kiburi’ cha kusema kwa sasa hatengemei radio na TV kama njia ya kutangaza muziki wake. Watu milioni tano ni wengi sana na kila siku wanaongezeka, uzuri ni kwamba jamaa mwenye kaona fursa ndani yao. Kama nusu ya watu hao, yaani milioni 2.5 wataamua kununua wimbo wake mmoja kupitia Wasafi.com kwa sh. 300, Diamond atakuwa ameingiza sh, 750,000,000 (milioni mia 750). Nimegawa idadi hiyo ya watu nusu kwa kuwa wapo wanamfuatilia katika mitandao yote mitatu.

Kwa hesabu vilivyo wazi kiasi hiki bado mtasema ameloga au anafanya biashara fulani ya magendo, bila shaka huu utakuwa ujinga wa kiwango cha PhD, si bure. Hapo bado hatujaangalia ‘show’ zake anazofanya kuanzia Bongo hadi nje, kampuni mbali mbali anazofanya nazo biashara ya matangazo na kadhalika, kiufupi jamaa ‘kajiloga’ mwenyewe tu na hii iwe fundisho kwa wasanii wengine.

Na Peter Akaro
Author Professional: Jounalist
Contact: 0755 299596

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents