Habari

Hoja za za Richmond, EPA moto

HOJA mbili zenye ushawishi mkubwa; Kashfa ya EPA na ripoti ya uchunguzi wa Richmond zinaonekana kugusa hisia za wabunge wengi na hivyo kubadili kabisa mwelekeo wa kisiasa katika siku za karibuni.

na Peter Nyanje

 

HOJA mbili zenye ushawishi mkubwa; Kashfa ya EPA na ripoti ya uchunguzi wa Richmond zinaonekana kugusa hisia za wabunge wengi na hivyo kubadili kabisa mwelekeo wa kisiasa katika siku za karibuni.

 

Mwenendo wa mambo ndani na nje ya Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo linaendelea kukutana mjini hapa unaonyesha kuwa, hoja hizo zimepandisha joto la kisiasa kiasi cha kumlazimisha Spika wa Bunge, Samuel Sitta, aahirishe ziara yake ya kikazi nchini Marekani iliyokuwa ianze jana.

 

Mabadiliko hayo ya ghafla ambayo hadi hivi sasa sababu zake hazijawekwa bayana yalitangazwa bungeni jana na Naibu Spika wa Bunge, Anne Makinda, mara baada ya kipindi cha maswali na majibu, wakati wa matangazo.

 

“Ni yeye mwenyewe ndiye amesitisha safari hiyo. Leo (jana) anahudhuria sherehe za siku ya sheria pale Dar es Salaam na ujumbe niliousoma ambao aliniandikia unasema kuwa kesho atakuwa hapa,” alisema Makinda.

 

Hata hivyo, alipotakiwa aeleze ni lini sasa masuala kuhusu Richmond na EPA yatajadiliwa, Makinda alisema kuwa hilo linatarajia ratiba ya shughuli za Bunge.

 

Akifafanua, alisema kwa mujibu wa kanuni zilizopo, ratiba ya mkutano wa Bunge inaandaliwa kwa kuzingatia kwanza shughuli za serikali na baadaye kufuatiwa na shughuli za kamati.

 

Alisema baada ya kwisha kwa shughuli hizo, ndipo hoja binafsi hupewa nafasi na kusema kuwa masuala hayo mawili yanahusisha kamati, itatarajia kwisha kwa shughuli za serikali.

 

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa mwanzoni mwa mkutano wa 10 wa Bunge unaoendelea, kulikuwa na miswada sita ya serikali pamoja na mazimio ambayo ilipaswa kujadiliwa katika mkutano huu.

 

Hadi jana, miswada miwili ilikuwa imeshapitishwa na jana Bunge lilikuwa likijadili Muswada wa Maliasili. Bado kuna miswada mingine mitatu, ikiwamo miwili kuhusiana na nishati, ambayo wabunge wengi walionekana kuipinga kupitia semina iliyofanyika Jumapili.

 

Habari za kuaminika ambazo Tanzania Daima imezipata jana kutoka ofisi za Bunge, zinaeleza kuwa Spika amelazimika kuahirisha safari hiyo kutokana na shinikizo kutoka kwa wabunge ambao wanataka kujadiliwa kwa masuala hayo mara moja.

 

Mwishoni mwa wiki, Spika alitangaza kusitisha mjadala wa hoja hizo kwa muda kutokana na yeye kuwa nje ya nchi kikazi kwa siku kadhaa.

 

Katika tangazo lake hilo, Sitta, alisema alikuwa akitarajia kusafiri jana kwenda Marekani kwa mwaliko rasmi wa Baraza la Wawakilishi la nchi hiyo na atarejea nchini Alhamisi wiki hii.

 

“Sikutaka Naibu Spika (Anne Makinda) akurupuke na kuvamia masuala haya nyeti, itabidi yasubiri mpaka pale nitakaporejea… tunayo wiki nzima ya kuyaangalia haya,” alikaririwa akisema Spika mwishoni mwa wiki iliyopita.

 

Habari zaidi ambazo Tanzania Daima inazo zinaeleza kuwa, wakati wabunge wakijiandaa kujadili hoja hizo mbili, kuna taarifa zinazoonyesha kuwapo kwa mipango ya siri inayosukwa yenye lengo la kuhakikisha kuwa mijadala kuhusu Richmond na EPA haijadiliwi bungeni.

 

Taarifa zilizolifikia gazeti hili kutoka kwa baadhi ya wabunge ambao hawakuwa tayari kutaja majina yao zimeeleza kuwa, mipango hiyo inahusisha pia kuhakikisha hata Bunge halipati fursa ya kujadili hoja hiyo, si tu katika mkutano wa 10 unaoendelea, bali pia moja kwa moja.

 

Hilo litafanikiwa kwa kuhakikisha suala hilo linafikishwa mahakamani mapema iwezekanavyo hivyo kuwaziba mdomo wote ambao wamekuwa na dhamira ya kutaka kuona ripoti hiyo inawekwa bayana.

 

Tanzania Daima imedokezwa kuwa mipango ipo mbioni, ili wiki hii watu kadhaa wafikishwe mahakamani kuhusiana na kashfa ya EPA na Richmond.

 

Kwa mujibu wa sheria, hakuna taasisi au mtu ambaye anaruhusiwa kulijadili hadharani suala lolote ambalo limefikishwa mahakamani, kwani inaaminika kuwa kufanya hivyo kunaweza kuharibu ushahidi wa kesi husika.

 

Mpasha habari wa kuaminika aliliambia gazeti hili kuwa inashangaza kuwa awali, maombi ya watu kadhaa, kutaka waliohusika katika kashfa hizo, hasa ya EPA, wakamatwe na kufikishwa kortini, yalidharauliwa.

 

“Tuliambiwa kuwa tusubiri uchunguzi unaoongozwa na timu iliyochaguliwa na Rais… lakini tulihoji kuwa iwapo ulikuwepo ushahidi wa kuwezesha kumwondoa (Dk. Daudi) Ballali (aliyekuwa Gavana wa BoT) na pia kampuni zilizochota fedha kwenye akaunti ya EPA zikitajwa waziwazi kulikuwa na nini kinachohitajiwa zaidi, ili suala hilo lifikishwe mahakamani?

 

“Tuliambiwa kuwa imeundwa kamati itakayofanya kazi kwa miezi sita, hatujamaliza hata mwezi mmoja, kamati hiyo imefanya kazi lini?” alihoji mpasha habari huyo.

 

Kwa upande mwingine, gazeti hili lilielezwa kuwa baadhi ya viongozi wakubwa serikalini wamekuwa wakihaha kujua kilichomo ndani ya ripoti ya Richmond, iliyoandaliwa na kamati ya Bunge iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela-CCM).

 

Inadaiwa kuwa uvumi unaosambaa kuwa vigogo hao wametajwa kuhusika kimakosa katika mchakato wa kuipata kampuni hiyo, ndio uliowatia hofu viongozi hao, kiasi cha kubuni mbinu ya kuizima hoja hiyo kujadiliwa hadharani.

 

Lakini suala hilo linazidi kuchukua sura mpya kufuatia kuwepo kwa taarifa kuwa baadhi ya wabunge ndani ya Chama Cha Mpinduzi (CCM) hawaridhishwi na jinsi baadhi ya masuala yanavyoendeshwa.

 

Inadaiwa kuwa kundi hilo linajumuisha wabunge ambao walibaguliwa kwa kutopatiwa fedha zinazodaiwa kuchotwa kutoka BoT, ambazo zinadaiwa kuingizwa kwenye mchakato wa kampeni za CCM.

 

Msukumo pia unatoka kwa baadhi ya wabunge ambao wanaamini kuwa wamepatwa na mikasa mikubwa wakati wa kampeni za uchaguzi ndani ya chama, ambao baadhi yao hivi sasa wana kesi mahakamani.

 

Inadaiwa kuwa hao ndio wamekuwa wakishinikiza suala la Richmond liletwe bungeni haraka kwani inaelezwa kuwa mmoja wa viongozi anayedaiwa kupanga njama za kuwaharibia baadhi ya wabunge, ametajwa katika ripoti hiyo.

 

Wabunge hao walikatishwa tamaa mwishoni mwa wiki iliyopita pale Sitta alipoahirisha mijadala ya masuala hayo mawili hadi atakaporejea kutoka Marekani.

 

Waliamua kuzishusha hasira zao hizo jana kupitia semina ya wabunge kujadili miswada ya sheria za nishati, pale walipoikataa miswada hiyo na kuitaka Kamati ya Uwekezaji na Biashara, kuishauri Kamati ya Uongozi kuiondoa miswada hiyo katika orodha ya shughuli zitakazofanywa katika mkutano unaoendelea wa Bunge.

 

Wabunge hao walidai wazi wazi kuwa hawawezi kujadili sheria mpya inayohusu umeme, wakati kuna ripoti ya Richmond ambayo haijajadiliwa na hawajui inaeleza kitu gani.

 

Baadhi ya wabunge walienda mbali zaidi na kueleza kuwa muswada wa umeme, ambao moja ya vipengele vyake vinahusu kuruhusu kampuni binafsi kuingia katika biashara ya umeme, unalenga kuwanufaisha watu fulani ndani ya serikali.

 

Mmoja wa wabunge hao alisema kuwa anahisi kuwa fedha zilizochotwa BoT zimetumika kuanzisha makampuni ambayo yatakuja kujiingiza katika biashara ya umeme na kuiua Tanesco.

 

Wabunge wengi walisema kuwa miswada hiyo imeletwa ili kuhalalisha wizi huo na kulitumia Bunge kama muhuri wa kuhalalisha masilahi ya watu wachache.

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents