Habari

Homa ya Bonde la Ufa hofu yazidi Dar

UGONJWA wa Homa ya Bonde la Ufa (RVF) unaendelea kusambaa nchini na sasa umeikumba mikoa ya Singida na Morogoro baada ya mikoa ya Arusha, Manyara na Dodoma.

Waandishi Wa Habari Leo

 

UGONJWA wa Homa ya Bonde la Ufa (RVF) unaendelea kusambaa nchini na sasa umeikumba mikoa ya Singida na Morogoro baada ya mikoa ya Arusha, Manyara na Dodoma. Kuenea kwa ugonjwa huo katika mikoa hiyo kunadhihirisha hatari ya kulikumba jiji la Dar es Salaam lenye wakazi zaidi ya milioni nne wanaotegemea nyama kutoka mikoani.

 

Juzi iliripotiwa kuwa wagonjwa kadha wamelazwa katika Mkoa wa Morogoro, Wilaya ya Kilombero, hali ambayo itakuwa vigumu ugonjwa huo kutokufika Dar es Salaam. Kutoka Singida, Mwandishi Wetu Hudson Kazonta anaripoti kuwa ugonjwa huo umeibukia mkoani humo baada ya watu kadha kulazwa huku mifugo ikifa ovyo.

 

Habari kutoka katika wilaya za Manyoni na Iramba ambako ugonjwa huo unadaiwa kuibuka, zinasema kuna mamia ya wanyama wameathirika na ugonjwa huo na baadhi yake kufa.

 

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Robati Salim akizungumza jana kwa simu alithibitisha kuwa na wagonjwa sita wanaohisiwa kuugua ugonjwa huo ambao hadi sasa wamelazwa hospitalini.

 

Wachambuzi wa masuala ya afya wanasema kuna hatari kubwa kwa ugonjwa huo kuingia Dar es Salaam kutokana na nyama nyingi kudaiwa kuuzwa bila kupimwa machinjioni. Gazeti dada la HabariLeo, la HabariLeo Jumapili, toleo la Januari 28 liliripoti hatari inayowakabili walaji wa nyama katika Dar es Salaam kutokana na kula nyama ambayo haijapimwa na madaktari wa mifugo.

 

Gazeti hilo lilisema hatari hiyo ipo kutokana na kutokuwapo ufuatiliaji mkubwa katika kupima nyama inayokadiriwa kufikia kilo 36,000 ambayo inaliwa Dar es Salaam kila siku, ingawa kiasi hicho kimepungua tangu ugonjwa huo uzuke nchini.

 

Mmoja ya viongozi waandamizi serikalini aliyezungumza na gazeti hili jana kwa masharti ya kutotajwa jina lake, alizishauri Wizara za Afya na Ustawi wa Jamii na Maendeleo ya Mifugo kuwa makini kuhakikisha ng’ombe wanaochinjwa hivi sasa wanakaguliwa kwa kiwango cha juu.

 

Alisema hali hiyo inatokana na ukweli kwamba ng’ombe wanaochinjwa Dar es Salaam, wanatoka katika mikoa ambayo imekumbwa na ugonjwa huo, ikiwamo ya Dodoma, Singida na hata Morogoro. Ugonjwa huo ulilipuka Kenya mwaka jana na kuua watu 80, hatua iliyoifanya Serikali ya Tanzania kuwatahadharisha wananchi kuhusiana na ugonjwa huo.

 

Hata hivyo katika kipindi kifupi ugonjwa huo ulilipuka Arusha na kusambaa katika maeneo mengine. Mkoa uliokumbwa zaidi na ugonjwa huo ni Dodoma ambako hadi sasa watu 16 wamefariki dunia, huku wengine karibu 100 wakiwa wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na ya Mirembe. Juzi, Serikali ilifunga machinjio ya mjini Dodoma isipokuwa yale ya Serikali kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kuzuia mfumuko zaidi wa ugonjwa huo.

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents