Habari

Homa ya Bonde la Ufa sasa kupimwa nchini

Sampuli za kubaini homa ya Bonde la Ufa, sasa zitaanza kupimwa hapa nchini baada ya serikali kununua mashine mbili za kupima sampuli hizo.

Na Mwandishi Maalum

Sampuli za kubaini homa ya Bonde la Ufa, sasa zitaanza kupimwa hapa nchini baada ya serikali kununua mashine mbili za kupima sampuli hizo.

Kabla ya kununuliwa kwa mashine hizo, sampuli hizo zilikuwa zikipelekwa nje ya nchi, hususan Nairobi, nchini Kenya ama Afrika Kusini.

Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Bw. Anthony Diallo, aliyasema hayo jana kwenye kikao cha kazi kilichoitishwa na Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kiliwashirikisha Wakuu wa Mikoa wote na baadhi ya Mawaziri.

Bw. Diallo alisema sampuli hizo sasa hazitapelekwa tena nje ya nchi kwa ajili ya vipimo kubaini homa ya Bonde la Ufa.

Hali kadhalika, Waziri Diallo amewatahadharisha wananchi wasifadhaike kutokana na ugonjwa wa homa hiyo inayowakabili binadamu na mifugo kwa vile serikali imekwishachukua hatua za kuudhibiti.

Alisema wizara yake imeagiza dozi milioni 1.8 za chanjo kwa mifugo zinazotarajiwa kufika katika vipindi mbalimbali katika mwezi mmoja.

Tayari iliagiza dozi za dharura 200,000 na sehemu yake kubwa imekwishasambazwa katika wilaya nane zilizo hatarini kuambukizwa ugonjwa huo ambazo ni Ngorongoro, Babati, Monduli, Longido, Hai, Simanjiro, Mkinga na Kilosa, alisema Diallo.

Alisema kwamba serikali, kwa kupitia Halmashauri za Wilaya husika, imepiga marufuku usafirishaji holela na uchinjaji ovyo wa mifugo.

Hata hivyo, alihimiza watu waendelee kula nyama, alimradi ipikwe na kuiva vizuri bila kuwa na damu.

Waziri Diallo pia alivitaka vyombo vya habari kutoa habari sahihi za ugonjwa huo na hatua za tahadhari kwa umma na siyo kuwaogopesha wananchi.

Ugonjwa huo ambao binadamu huambukizwa kutoka katika mifugo, uliingia nchini hivi karibuni kutoka nchi jirani ya Kenya.

Hutokea katika nchi za ukanda wa Bonde la Ufa ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Somalia, Ethiopia, Sudan na Misri.

Mara ya mwisho ugonjwa huo kutokea nchini ni mwaka 1998 baada ya mvua kubwa za El- Nino.

Homa ya Bonde la Ufa hutokea baada ya mvua nyingi zinazoleta mafuriko hasa baada ya ukame wa muda mrefu na mbu kuzaliana kwa wingi ambapo binadamu na wanyama wanaambukizwa kwa kuumwa na mbu wenye virusi vya ugonjwa huo.

Binadamu pia huambukizwa ugonjwa huo kwa kuchinja, kuchuna ngozi, kula nyama au kunywa maziwa yasiyochemshwa kutoka kwa mnyama mgonjwa.

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents