Bongo5 Makala

Hongera Dogo Janja, ipe elimu kipaumbele zaidi ya muziki


Juzi Dongo Janja alithibitisha kuwa anao mashabiki wengi wanaomuunga mkono kwa lolote jema analolifanya. Msanii huyo alijikuta akikutana na mapokezi mazito kwa shangwe na vifijo kutoka kwa mashabiki mbalimbali walioamua kuacha shughuli zao na kwenda kumpokea katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Aliwasili jijini Dar es Salaam jana mida ya nne akitokea Arusha baada promoter wa muziki nchini Ustaadh Juma kumpigia simu na kumpa ofa na mkataba utakaohakikisha kuwa mtoto huyo anaendelea na shule na kumsaidia kimuziki pia. Uamuzi wa Ustaadhi Juma wa watanashati kumchukua Dogo Janja umefufua matumaini mapya ya mtoto huyo yaliyokuwa yamefutika kwa muda baada ya kukosana na familia yake iliyomleta Dar, Tip Top Connection.

Kwa sasa macho na masikio ya wapenzi wa muziki nchini yameelekezwa kwake kutaka kujua nini kitafuata baada ya msanii huyo kutoka Arusha kuwa mikononi mwa uongozi mpya. Tunafahamu kuwa kabla ya kurudi Arusha, Dogo Janja ndio kwanza alikuwa kidato cha pili katika shule ya Makongo.

Kwa inavyoonekana ni kwamba hata kama akirudi shule, hatasoma tena Makongo hivyo kuna uwezakano wa kutafutiwa shule nyingine ili kuendelea na masomo. Ingawa lawama nyingi mpaka sasa zinaelekezwa kwa kambi ya TipTop Connection kutokana na tukio zima,kuna haja ya kuzichukulia uzito japo kidogo tu shutuma za utoro dhidi ya Dogo Janja zilizotolewa na Madee.

Kwa mujibu wa Madee ambaye kwa sasa kila mtu anamuona mbaya (ni haki kumuona hivyo kutokana na shutuma mbaya dhidi yake), Dogo Janja alikuwa akiendekeza starehe na kusahau shule.

Hizo zinaweza kuwa ni shutuma zinazotolewa na kambi ya Tip Top kama njia ya kujilinda baada ya kuchukua uamuzi wa kumrudisha kwao Arusha lakini suala la utoro hasa kwa mtoto anayeishi maisha ya muziki kama yeye linaweza kuwa na ukweli ndani yake.

Hata hivyo kwakuwa tayari kila upande umefungua ukurasa mpya na maisha yanaendelea kama kawaida,hatuna budi kuyasahau yaliyopita na sasa tuangalie namna na kumsaidia kijana huyo ambaye bado yupo kwenye umri wa kijinga asipotee njia na kuja kujuta baadaye.
Kwetu sisi tunaamini kuwa ni elimu pekee ndiyo itakayomsaidia kuwa mwanamuziki mwenye mafanikio baadaye.

Tunafahamu namna ambavyo baadhi ya wasanii wakubwa nchini wanavyojuta sasa hivi baada ya kubweteka na muziki na kudharau elimu, wakati huo walipokuwa na muda na uwezo wa kuitafuta.

Ili kufanikiwa katika muziki wa sasa, wasanii wanapaswa kujiimarisha kielimu hasa kama malengo yao ni kuvuka mipaka ya Tanzania.
Msanii aliyeelimika hujiamini zaidi na hupata uwezo wa kupambanua mambo kisomi na kujilinda dhidi ya hatari ya kudhulumiwa.
Dogo Janja atumie nafasi hii kusoma zaidi ili kama muziki usipompa matunda anayoyatarajia elimu itabaki kuwa mkombozi wake na kuendelea na maisha mengine bila shida.

Ili Ustaadh Juma aonekane wa maana, anatakiwa kumhimiza kijana huyu kujitahidi darasani na kuugawa muda wake vizuri wa kuwatumikia mabwana wawili, shule na muziki. Uongozi mpya umkalishe chini na kumpa maneno ya busara yatakayompa uelekeo salama wa safari mpya atakayoianza akiwa chini ya uongozi mwingine.

Huu ni muda wa Dogo Janja kuwathibitisha wale ambao bado wana wasiwasi naye kutokana na kile kilichosemwa dhidi yake kwa kuwa mnyenyekevu na kuzingatia masomo darasani. Akumbuke namna mama yake alivyoumizwa na tukio zima la yeye kurudishwa Arusha, na kuwa wanamtegemea aje kuikomboa familia yao.

Afanye muziki na kuzingatia masomo darasani kwa kuikumbuka sauti ya mama yake iliyokuwa inazungumza kwa uchungu kwenye radio, mama ambaye muda wote amekuwa akimuombea mwanae afanikiwe. Kama akipuuzia elimu na kubweteka na muziki atambue kuwa atakuwa anawaangusha sana wazazi wake waliompa uhuru wa kuzifuata ndoto zake.

Tunamtakia kila lakheri kijana huyu katika maisha mapya ya muziki.
Karibu tena Dar es Salaam Dogo Janja.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents