Shinda na SIM Account

Hospitali ya kisasa kujengwa Kisarawe

Hospitali kubwa ya kisasa ambayo itakuwa kubwa kuliko Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), inatarajiwa kujengwa wilayani Kisarawe hivi karibuni.

Na Joseph MwendapoleHospitali kubwa ya kisasa ambayo itakuwa kubwa kuliko Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), inatarajiwa kujengwa wilayani Kisarawe hivi karibuni.


Hospitali hiyo itakayokuwa chini ya Chuo Kikuu cha Tiba ya Afya Muhimbili (MUCH), itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 2,000 wa nje na kulaza wagonjwa 1,000 kwa siku.


Hayo yalisemwa jana na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Kisali Pallangyo, wakati akizungumza na waandishi wa habari chuoni hapo.


Alikuwa akizungumzia mkakati wa chuo hicho kuongeza udahili wa wanafunzi wanaosomea udaktari ili kupunguza upungufu wa madaktari uliopo.


Alisema hospitali hiyo ikikamilika itasaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi kwa kuwa itakuwa na vifaa vya kutosha.


Alisema hivi sasa chuo hicho kina uwezo wa kudahili wanafunzi 200 wa udaktari kwa mwaka, ambao hawakidhi mahitaji yaliyopo.


Alisema hospitali hiyo itajengwa pamoja na kampasi nyingine ya chuo hicho ambayo itakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 400 kwa mwaka.


Profesa Pallangyo, alisema eneo ambalo wamepata kwa ajili ya kujenga hospitali hiyo na kampasi ya chuo hicho lina ukubwa wa hekari 3, 800.


Alisema awali ujenzi huo unatarajiwa kuanza kwa kutumia Dola milioni 80 za Marekani na kwamba tayari wafadhili mbalimbali wameonyesha nia ya kufadhili ujenzi huo.


Aidha, Profesa Pallangyo alisema hivi sasa uwiano wa wagonjwa na daktari ni mkubwa sana nchini kulinganisha na nchi za Kenya na Uganda.


Alisema nchini Kenya daktari mmoja anahudumia wagonjwa 8,000 kwa mwaka wakati Tanzania daktari mmoja anahudumia wagonjwa 30,000 kwa mwaka.


Hatujajua lini ujenzi utaanza kwa kuwa hatujapata fedha lakini mipango yote ikiwa ni pamoja na kupata kiwanja imekamilika, alisema Profesa Pallangyo alipoulizwa ujenzi huo unatarajia kuanza lini.


Aliongeza kuwa katika mpango huo, serikali inataka kila hospitali ya mkoa iwe na madaktari bingwa wa upasuaji, wanawake, watoto, mifupa, nusu kaputi na magonjwa ya akili.


Hata hivyo, Profesa Pallangyo, alisema lazima madaktari wawekewe mazingira mazuri ya kazi na maslahi ili waachane na kawaida ya kukimbilia nje ya nchi.


Source: Nipashe

Related Articles

Bongo5

FREE
VIEW