Habari

Hospitali ya Muhimbili yaimarisha uwezo wa wataalam wa kupandikiza Figo

Katika kipindi cha miezi nane Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH) imefanikiwa kupandikiza figo wagonjwa 10 kwa mafanikio makubwa ambapo katika kambi ya tatu ya upandikizaji figo, upasuaji umefanywa na watalaam wa MNH kwa zaidi ya silimia 80wakisimamiwa na watalaam kutoka nchini India.

Akizungumza leo Juni 26, 2018 jijini Dar es salaam, na Wanahabari Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru amesema MNH ilianza upandikizaji figo Novemba 2017 kwa kupandikiza mgonjwa mmoja ambapo Aprili 2018 wagonjwa wanne walipandikizwa figo na Juni 24 hadi 25, 2018 wagonjwa watano wamepandikizwa figo.

“Pamoja na upasuaji huo kufanyika, mwaka 2016 hospitali ilipeleka watalaam wake nchini India kujengewa uwezo wa kupandikiza figo hivyo napenda kuwafahamisha kuwa tangu tumeanza upandikizaji wa figo tunaendelea kupata mafanikio makubwa kwa baadhi ya watalaam wetu wa ndani kuwa na uwezo wa kushika kufanya wenyewe katika mchakato mzima wa uchunguzi hadi kupandikiza figo,” amesema Prof. Museru.

“Tunaamini katika kambi mbili zinazokuja za upasuaji wa kupandikiza figo, madaktari wa upasuaji wazalendo watafikia kiwango cha asilimia 100. Hii ni hatua kubwa sana katika kipindi cha miezi nane kwani mara ya kwanza walikuja watalaam wote wanaohitajika wapatao 15, tulipofanya mara ya pili walipungua wakaja watalaam saba na safari hii mara ya tatu wamepungua wamekuja watano tu, tunaamini wataendelea kupungua katika kambi tatu zijazo na hatimaye kusimama wenyewe na kufanya kwa viwango na ubora uleule,” amesisitiza Prof. Museru.

Kwa upande wake Daktari Bingwa wa magonjwa ya figo kutoka hospitali ya Saifee ya nchini India, Dkt. Mustafa Khokhawala amesema Madaktari wa Muhimbili wameshiriki upasuaji huo kwa asilimia kubwa ambapo kati ya wagonjwa watano waliopandikizwa figo, mgonjwa mmoja amepandikizwa na wataalam wa ndani na kwamba hatua hiyo ni nzuri na inaonyesha kuwa watalaam wa MNH wanauwezo mkubwa wa kuendelea na upandikizaji.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents