Habari

Hukumu bosi TPA sasa kusoma mwezi ujao

Hukumu ya kesi ya matumizi mabaya ya madaraka inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA), Ephraim Mgawe na Naibu wake aliyekuwa anashughulikia huduma, Hamad Koshuma, kwa mara nyingine imeahirishwa hadi Februari 10 mwaka huu.

Awali, kesi hiyo ambayo ilikuja katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilipangwa kutolewa hukumu Oktoba 13, mwaka jana lakini iliahirishwa tena kwa mara tatu. Wakili Mwandamizi wa Serikali, Mutalemwa Kishenyi alidai mbele ya Hakimu Wilbard Mahauri kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya hukumu na kwamba walikuwa tayari kusilikiza.

Alidai kuwa kesi hiyo ipo mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Cyprian Mkeha kwamba ambaye hayupo. Hata hivyo, Hakimu Mashauri alisema kuwa hajaachiwa kitu chochote kuhusu kesi hiyo na kwamba maelekezo aliyoachiwa ni kuahirisha kesi hadi Februari 10, mwaka huu.

Katika kesi hiyo, Mgawe na mwenzake inadaiwa Desemba 5, 2011, walitumia madaraka yao vibaya kwa kutoa zabuni ya upanuzi wa gati namba 13 na 14, katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa Kampuni ya China Communications Construction Company Ltd (CCCC), bila kutangaza zabuni.

Inadaiwa washitakiwa hao walitenda kosa hilo wakati wakitekeleza majukumu yao ya utumishi wa mamlaka hiyo kwa nafasi ya mkurugenzi mkuu na naibu wake.

Aidha, katika hati ya mashtaka, watuhumiwa hao wanadaiwa kuweka saini mkataba wa kibiashara na kampuni hiyo ya kichina bila zabuni shindanishi, ambapo ni kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma namba 21 ya 2004, ambapo walitumia dola za kimarekani milioni 600.

Mbali na kesi hiyo, Mgawe na wenzake watatu wanakabiliwa na kesi nyingine ambapo hivi karibuni walipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na kusomewa mashitaka ya kuomba rushwa zaidi ya Sh milioni nane.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi wa uhandisi TPA, Bakari Kilo, Meneja wa manunuzi TPA, Theophil Kimaro (54) na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya DB Shapriya Ltd, Kishor Shapriya.

BY: Emmy Mwaipopo

Chanzo:Habari Leo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents