Habari

Hukumu ya mwanasiasa wa upinzani Rwanda, Diane Rwigara na Mamake Adeline Rwigara kutolewa

Mahakama mjini Kigali leo inatarajia kutoa uamuzi wake wa mwisho kuhusu kesi dhidi ya mwanasiasa wa upinzani Diane Rwigara na Mamake Adeline Rwigara. Wawili hao wameshitakiwa makosa ya kuchochea vurugu na mgawanyiko miongoni mwa wananchi pamoja na kughushi nyaraka.

Kwa mujibu wa BBC, Muendasha mashtaka ameshaomba mahakama kuwapa kifungo cha miaka 22 jela.

Walikanusha madai hayo wakisema yana misingi ya kisiasa.Marekani imeishinikiza Rwanda kuondoa mashitaka hayo,lakini Rwanda imejibu kwamba haishinikizwi na yeyote na kuomba vyombo vya sheria visiingiliwe.

Kinachotarajiwa leo ni uamuzi wa mwisho kuhusu maombi ya upande wa mashitaka ya kuwapa kifungo cha miaka 22 jela katika kikao cha mwisho mwezi uliopita,huku upande wa mawakili wao wakipinga maombi hayo na kusisitiza wateja wao kuachiwa huru mara moja.

Waendesha mashtaka waliomba hukumu hiyo wakisema Diane Rwigara alihusika katika kughushi nyaraka wakati alipokuwa akikusanya saini za wafuasi wake wakati wa kutaka kugombea urais kama yalivyo masharti ya tume ya uchaguzi na kwamba kumekuwa na saini za wafuasi hewa baadhi wakiwa walifariki dunia na wengine wakiwa hawapo nchini.

Kadhalika Diane Rwigara na Mamake walishitakiwa kuchochea chuki na kusambaza uvumi kwa lengo la kuhamasisha umma kugoma dhidi ya utawala.

Uamuzi wa Alhamisi unasubiriwa kwa hamu na gamu baada ya Diane Rwigara na mamake Adeline Mukangemanyi kukamilisha kesi hii wakiwa hawako kizuizini.

Kwa mshangao wa wengi , mapema mwezi wa 10 mwaka huu mahakama ilichukua uamuzi wa kuwaachilia huru kwa dhamana ikisema sababu za kimsingi zilizosababisha kesi yao kusikilizwa wakiwa kizuizini hazipo tena.

Wao Wanakanusha mashtaka dhidi yao wakisema yalichochewa kisiasa hasa baada ya Diane Rwigara kujitokeza katika ulingo wa kisiasa,akipinga wazi sera za chama tawala na kutaka kugombea urais katika uchaguzi uliofanyika mwaka jana.

By Ally Juma.

 

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents