Tupo Nawe

Huyu ndiye Mtanzania aliyeacha kazi ya udaktari aliyosomea kwa miaka mitano na kujiajiri kama msanii wa uchoraji

Unawezaje kuacha kazi ya udaktari na kuwa mchoraji? Hilo ni swali ambalo Peter Bulugu amekuwa akikabiliana nalo kwa miaka mitatu sasa.

Bulugu, mwenye miaka 32, ni daktari wa binadamu aliyefunzwa kwa miaka mitano (2008-2015) katika chuo kikuu mashuhuri zaidi cha sayansi ya tiba nchini Tanzania cha Muhimbili (Muhas).

Baada ya hapo akafanya kazi ya utabibu kwa kipindi kifupi, awali kama sehemu ya mafunzo kwa vitendo katika hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar na Hospitali ya Rufaa Morogoro.

Bulugu alipata ajira katika hospitali binafsi Makete ambapo alidumu kwa miezi nane tu, na kufikia maamuzi ya kuacha kazi mapema 2016 na kujiajiri kama msanii wa uchoraji.

“Mama yangu na baadhi ya ndugu hawakunielewa kabisa kipindi nimewapa taarifa hii,” anaeleza Bulugu.

“Udaktari ni kitu nilichokuwa nakipenda, na masomo ya sayansi nilikuwa nayamudu… Kwa familia (za kimasikini) tulizotoka kupata mkopo (wa masomo ya chuo kikuu) ndicho kilikuwa kipaumbele, na kusoma sayansi kulihakikisha mkopo kwa asilimia zote.”

Pia, anaeleza kuwa aliamini kazi hiyo ya utabibu ina maslahi makubwa: “Huenda pia zilikuwa akili za kitoto kwamba ukiwa daktari utakuwa na hela! Nikasoma udaktari.”

Lakini aligundua kuwa uhalisia wa mambo haukuwa hivyo baada ya kuanza kazi, “Kulitokea changamoto kati yangu na uongozi wa hospitali hii binafsi wakati wa kuandika mkataba wa kazi. Hivyo kutokukubaliana huko kukasababisha niache kazi lakini nikitegemea kuwa huenda ajira za serikalini zingetoka muda si mrefu, la haikuwa hivyo!”

Dkt Bulugu hakuacha kazi aliyosomea ili akajifunze kuwa mchoraji, tayari alishagundua na kukiendeleza kipaji chake toka awali.

“Kuchora nilianza nikiwa mdogo kabisa shule ya msingi. Na nimewahi kuwakilisha mkoa wa Dodoma (alipozaliwa) kwenye michezo na taaluma kwa shule za msingi (Umitashumta) pale Morogoro ambapo ilifanyika kitaifa na kuwa mshindi wa tano mwaka 2000.

Michoro ya Dkt Bulugu

Mwaka 2003 mpaka 2005 wakati yupo kwenye masomo ya sekondari pia alikuwa mchora katuni kwenye gazeti la Sauti ya Dodoma lililokuwa chini ya mradi wa kupinga tohara kwa wanawake, AFNET.

“Na nikiwa kidato cha nne niliwahi kushiriki shindano la kuandaa nembo kwa ajili ya shirika moja la kujihusisha na watoto yatima. Nikawa mshindi wa kwanza na hivyo nikapata zawadi lakini tayari nikiwa kidato cha tano pale Tabora, nikatumiwa zawadi yangu. Hii iliendelea kunipa moyo kutoiacha sanaa hii ya uchoraji.”

Akiwa chuo kikuu Muhimbili pia aliendelea kujitosa kwenye mashindano kadhaa ikiwemo ya shirika lisilo la kiserikali linaloangazia masuala ya elimu, Hakielimu, na kuwa mshindi wa nne kitaifa.

“Nikiwa chuo pia niliwahi kujikuta nikiwa matatani kwa Kuchora katuni ambayo uongozi wa chuo haukupendenza nayo!”

Wakati akiwa Zanizibar kwenye mafunzo ya udaktari kwa vitendo mara baada ya kuhitimu chuo kikuu alikuwa pia akichora picha na kuziuza kwa wenye maduka ya kitalii.

Hivyo mara baada ya kuacha kazi akaamua kwenda kuanza maisha ya ujasiriamali visiwani Zanzibar. Tayari ana maduka mawili la kwanza lipo Kaskazini kwenye kijiji cha utalii cha Nungwi na la pili lipo mjini kabisa eneo la Mji Mkongwe.

Dkt Bulugu

Picha zake anachora katika ‘canvas’ na kutumia rangi zenye uborana na ni kwa matumizi ya nyumbani, ofisini na sehemu nyengine.

“Kuwa mchoraji kumenipanafasi ya kufanya kazi kwa uhuru, lakini pia nimekutana na watu mbalimbali na kufanya mambo mengine pia. Ni ngumu mwanzoni kutoka kupokea mshahara kila mwezi hadi kuanzisha biashara ambayo mapato ya mwanzo hutumika kukuza biashara na pengine wewe usijilipe kwa muda mrefu. Lakini dhamira ya ndani ilinisukuma kufanya kazi kwa bidii sana huku nikichora picha nyingi iwezekanavyo kujaza maduka yote mawili.

Bulugu ameiambia BBC kuwa nje ya mfumo wa ajira kumempa ujasiri na nidhamu. “Bado sijafikia yale mafanikio niyaonayo mbele yangu lakini naona niendapo. Na hii imenipa kufanya hata kazi zile za kujotolea nikijua zitalipa baadae.”

Mwezi Disemba mwaka 2018 alianza mradi wa kuhusianisha michoro na hospitali. Na alianza kuchora picha ndogo ndogo na kuzipeleka hospitali za Vijibweni, Temeke na Kairuki zote za Dar es salaam.

Picha hizo zimewekwa katika wodi za watoto.

Dkt Bulugu

“Na mwaka huu nimeweza kuchora katika kuta za wodi katika hospitali ya rufaa Morogoro wodi ya watoto, ambapo jumla nilijitolea michoro 20. Hii ilinipa nguvu kwani moja kwa moja niliweza kuona mwitikio wa watoto, walezi wao na hata wauguzi na madaktari wa wodi husika. Pia nimefanya michoro katika hospitali binafsi ya Bochi iliyopo Mbezi hapa Dar es salaam.”

Michoro hiyo Dkt Bulugua anasema inasaidia kwa sehemu kuhamisha mawazo ya mgonjwa kutoka kwenye ugonjwa na maumivu aliyonayo na pia kutengeneza mazingira rafiki.

“…kuna tafiti chache zilizofanyika kuthibitisha uhusiano chanya kati ya kazi za sanaa na tiba.”

“Malengo yangu ni kuona hili wazo likienea pote na kufanya hospitali zetu ziwe sehemu rafiki kimazingira. Kila wodi iwe na picha ndiyo dhamira yangu. Hivyo wasanii mbalimbali kwa sehemu moja ama nyingine wanaweza kufanikisha hili,” amedhamiria Bulugu.

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW