Habari

Idadi ya vifo ajali ya moto mkoani Morogoro yaongezeka, Majeruhi wote walazwa ICU

Idadi ya vifo vya ajali ya moto iliyotokea baada ya Lori la mafuta kuwaka moto mkoani Morogoro imeongezeka kutoka watu 95 hadi 97, Hii ni baada ya majeruhi wawili kati ya 20 waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, kufariki dunia.

Akiongea na waandishi wa habari, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma Muhimbili, Aminieli Aligaesha, amesema idadi ya majeruhi waliobaki hospitali hapo ni 18 na wote wako katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU).

Akitaja majina ya majeruhi waliofariki dunia, Aligaesha amesema ni Rosijo Mollel (35) na Neema Chakachaka (30), hivyo idadi ya majeruhi waliofariki wakiwa hospitalini hapo ni 29.

Majeruhi wawili wamefariki dunia, kuna Rosijo Mollel ana miaka 35 ambaye aliletwa juzi kutoka Hospitali ya Rufaa Morogoro, huyu alifariki jana mchana saa nane na Neema Chakachaka alifariki saa 11:30 alfajiri ya leo (jana), huyu alilazwa ICU iliyopo jengo la wazazi. Kati ya majeruhi 47 walioletwa hapa, wamebaki 18 na wote wako ICU. Waliopo ICU ya Mwaisela wapo 14, mtoto mmoja yupo ICU ya watoto na wengine watatu wako ICU ya HDU Mwaisela, mpaka sasa majeruhi waliopoteza maisha wakiwa hapa hospitali wamefikia 29,” amesema Aligaesha.

Aligaesha amesema Hospitali ya Muhimbili inaendelea kutoa huduma kwa majeruhi waliobaki ili waweze kurejea katika hali nzuri,”Bado tunaendelea kupambana, madaktari wetu na wale wa JWTZ wanaendelea kuwapatia matibabu majeruhi hawa ili waweze kurejea katika hali nzuri,” .

Chanzo: Gazeti Mtanzania

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents