Habari

Idadi ya watu duniani kufika bilioni 11.2 mwaka 2100

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa na idara ya uchumi na masuala ya kijamii ya shirika la kushughulikia idadi ya watu duniani katika umoja huo, inakadiria kuwa idadi ya hivi sasa ya watu duniani ya takriban bilioni 7.6 itaongezeka hadi kufikia watu bilioni 8.6 ifikapo mwaka 2030, bilioni 9.8 ifikapo 2050 na bilioni 11.2 ifikapo mwaka 2100.

Ripoti hiyo inakadiria idadi ya watu wa India itaipiku ya China katika kipindi cha miaka saba ijayo, na Nigeria inatarajiwa kuipiku Marekani na kuwa taifa la tatu duniani lenye idadi kubwa ya watu ifikapo 2050.

China hivi sasa ndiyo inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu ikiwa na watu bilioni 1.4, ikifuatiwa na India yenye watu bilioni 1.3. Ifikapo 2024, India inatarajiwa kuipiku China. Kwa mujibu wa ripoti hiyo inasema uzazi umepungua kwa takriban kila eneo katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, huku watu milioni 83 wanazaliwa duniani kila mwaka.

John Wilmoth ambaye ni Mkurugenzi wa kitengo hicho cha idadi ya watu amesema, ripoti hiyo imekusanya takwimu kutoka mataifa 233 duniani na kuongeza idadi ya watu barani Afrika inakua kwa kiwango cha juu na inatarajiwa nusu ya idadi ya watu duniani kati ya sasa hadi mwaka 2050 itatoka barani humo.

Kwa upande mwingine, idadi ya watu barani Ulaya itapungua katika kipindi cha miongo kadhaa ijayo. Shirika hilo la Umoja wa Mataifa limebashiri kuwa kuanzia sasa hadi mwaka 2050 idadi ya watu itaongezeka hususan katika mataifa haya ya India, Nigeria, Congo, Pakistan, Ethiopia, Tanzania, Marekani,Uganda na Indonesia. Katika kipindi hicho hicho, idadi ya watu katika mataifa 26 ya Afrika itaongezeka karibu mara mbili.

Nchi kumi zenye idadi kubwa ya watu hivi sasa lakini zinaviwango vya chini vya uzazi ni China, Marekani, Brazil, Urusi, Japan, Vietnam, Ujerumani, Iran, Thailand na Uingereza. Mbali na kupunguwa kwa ukuaji wa idadi ya watu, viwango hivyo vya chini vya uzazi vimesababisha kuongezeka kwa idadi ya wazee.

Idadi ya watu walio na umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea itaongezeka kutoka watu milioni 962 hivi sasa hadi watu bilioni 2.1 ifikapo 2050. Robo ya idadi ya watu barani Ulaya tayari wana umri wa miaka 60 na zaidi. Hata hivyo bado kuna pengo kubwa kati ya mataifa masikini na matajiri katika suala la usawa. Makadirio ya umri wa mtu kuishi katika mataifa tajiri ina kadiriwa kuishi miaka 80 huku watu wanaoishi Afrika wanakadiriwa kuishi hadi umri wa miaka 50.

By Peter Akaro

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents