Habari

Idara ya Maendeleo ya Jamii yaendesha mafunzo ya udhibiti wa viashiria hatarishi sehemu za kazi

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) imeendesha mafunzo kuhusu Mfumo wa Udhibiti wa Viashiria Hatarishi Mahali pa Kazi yanayofanyika Ukumbi wa VETA mkoani Dodoma.


Kaimu Katibu Mkuu wa Idara Kuu ya Maendeleo ya jamii, Jinsia Wazee na Watoto Bw. Maercel Katemba akifungua Mafunzo ya Mfumo wa Udhibiti wa Viashiria Hatarishi Mahala pa Kazi kwa watumishi wa Idara Kuu Maendeleo ya Jamii yanayofanyika katika katika Ukumbi wa VETA mkoani Dodoma.

Mafunzo haya ya siku nne yanajumuisha wakuu wa Idara, wakuu wa vitengo, wakurugenzi wasaidi na wasimamizi wa udhibiti wa vihatarishi katika sehemu ya kazi.

Akifungua mafunzo hayo Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii- Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii Bw. Marcel Katemba amesema kuwa suala la udhibiti wa viashiria hatarishi linatokana na matakwa ya Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2001 (2010) na Waraka wa Hazina namba 12 wa 2012/2013 unaoitaka kila Taasisi ya Umma kuzingatia uandaaji na utekelezaji wa Mfumo wa Menejimenti ya Viashiria vya Vihatarishi mahala pa kazi.

“Mafunzo haya ni nyenzo ya utumishi wa umma katika kudhibiti wa mifumo ya ndani ya Taasisi na hivyo kuleta ufanisi katika shughuli na utendaji wa kazi za kila siku na kuwezesha upatikanaji wa taarifa za kiutendaji na za fedha zenye kuaminika” alisema Bw. Katemba.

Kaimu Katibu Mkuu Bw. Marcel Katemba amewakumbusha washiriki kuwa, mafunzo hayo ni mwendelezo wa yale yaliyofanyika mwezi Julai, 2016, hivyo ni jukumu la pamoja kati ya Menejimenti na watumishi wote wa Idara kuu ya Mendeleo ya Jamii kwa ujumla wao kusimamia kikamilifu Viashiria Hatarishi katika Idara na Vitengo husika.

Ameongeza kuwa muendelezo huo utawaongezea uwezo watendaji, kuwa na uelewa wa pamoja wa kutosha kuhusu viashiria vilivyo katika maeneo ya kazi.

Akitoa mada katika mafunzo hayo, Mratibu Bw. Dickson Rusage amesema kuwa Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ni miongoni mwa Wizara tano (5) kati ya Wizara 21 za Serikali ambazo zimeweza kuanzisha mfumo wa udhibiti wa viashiria hatarishi mahala pa kazi na kuutekeleza.

Ameongeza kuwa Idara kuu ya Mendeleo ya Jamii imepiga hatua zaidi kwa kuwatumia wataalam wake wa ndani katika kutoa mafunzo ya uelewa na kusimamia udhibiti wa vihatarishi.

Bw. Rusage amebainisha kuwa changamoto zilizopo katika kuendesha mfumo huo ni pamoja na ukosefu wa rasilimali fedha, mfumo kutopewa kipaumbele, kutokuwepo dhamira ya dhati katika matumizi ya mfumo, kutozingatia mfumo katika kufikia malengo ya Wizara, Idara, na Taasisi husika.

Kwa upande wake Mwezeshaji katika Mafunzo hayo Bw. Moris Jackson amesema kuwa manufaa ya mfumo wa udhibiti wa viashiria mahala pa kazi ni kuwa Wizara inayokuwa na mfumo huu, wabia wa maendeleo wataiamini Taasisi kwamba rasilimali zinazotolewa zitakuwa salama maana viashiria vinafahamika na vimewekewa mifumo ya ufuatiliaji na udhibiti kwa manufaa mapema.

Mada zitakazowasilishwa katika mafunzo hayo ni pamoja na Maana na makundi, Faida na Kanuni za Usimamizi wa Viashiria vya Vihatarishi, Matakwa ya kisheria kuhusu Usimamizi wa Vihatarishi nchini, Muundo na maeneo muhimu ya kimwongozo, Mgawanyo wa majukumu katika Usimamizi wa Vihatarishi na nyaraka mbalimbali zitakazotumika wakati wa kuandaa na kusimamia Vihatarishi.

Mategemeo ya mafunzo hayo ya mahala pa kazi yanalenga washiriki kuweza kubaini vihatarishi ambavyo viliwekwa mwaka jana na sasa havitakiwi kuwepo tena, kubaini vihatarishi vipya ambavyo ama vilisahaulika au vitaibuliwa sasa kutokana na shughuli na kazi za Idara na Vitengo hasa baada ya mwaka kuisha na kupata maoni na ushirikiano wa kutosha ili kwa pamoja kufikia malengo yaliyokusudiwa katika kudhibiti viahatarisi kazini.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents