Habari

Iringa sio sehemu salama – Waeleza Maofisa Uhamiaji

Wahamiaji haramu wapatao 83 kutoka nchini Ethiopia wamekamatwa mkoani Iringa wakiwa kwenye lori wakisafirishwa kwenda Malawi kisha Afrika Kusini.

Wahamiaji hao walikamatwa na Maofisa Uhamiaji mkoani humo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kijiji cha Mbigili wilayani Kilolo ambapo imeelezwa kuwa katika purukushani hiyo dereva wa lori ambalo ni mali ya mkazi wa Tukuyu mkoani Mbeya alifanikiwa kutoroka.

Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Uhamiaji Mkoa wa Iringa, Hope Kawawa amesema wahamiaji hao walikamatwa Februari 22, 2018 saa 11 jioni na kutoa onyo kwa watu wote wanaojihusisha na biashara ya kusafirisha watu hao waache mara moja kwani Iringa sio sehemu salama kwa biashara hiyo.

Naomba niwaambie madalali wanaosafirisha hawa wahamiaji kuwa mkoa wa Iringa si mahala salama kuwapitisha kwa kuwa tuko makini saa 24 na tukiwabaini hatua kali zitachukuliwa dhidi yao,”amesema Kawawa.

Kawawa amesema wahamiaji hao walipelekwa kituo cha polisi cha Lugalo na taarifa za kukamatwa kwao zilipenyezwa Uhamiaji na wananchi wazalendo na wahamiaji hao watafikishwa mahakamani kesho Jumatatu.

Kwa upande mwingine, Kawawa ametoa wito kwa Watanzania kutoa taarifa pindi wanapohisi baadhi ya watu si raia wa Tanzania na wanapowaona watu wasiowatambua.

Chanzo:Mwananchi

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents