Technology

Jamii Media yafungua kesi kupinga sheria ya makosa ya mtandao

Kampuni ya Jamii Media, inayoendesha mitandao ya JamiiForums.com na FikraPevu.com, imefungua kesi kupinga baadhi ya vipengele kwenye sheria ya makosa ya mtandao iliyopitishwa mwaka jana.

1352147_Wallpaper1

Kwenye maelezo yake, kampuni hiyo imesema:

Pamoja na kuendelea kutoa huduma hata katika nyakati ngumu, mtandao wa JamiiForums unakumbana mara kwa mara na changamoto nyingi zinazopelekea waanzilishi na waendeshaji wake kuwa katika misukosuko mara kwa mara.
Kwa takribani miezi mitatu iliyopita, Jeshi la Polisi limekuwa likiushinikiza mtandao huu (kwa njia ya barua rasmi) kutoa taarifa za baadhi ya wateja wake wanaoonekana kutoa taarifa zile ambazo kwa namna moja ama nyingine zinaibua ufisadi mkubwa na ukwepaji wa kodi.

JamiiForums katika kuhakikisha inasimamia usiri (privacy) wa wateja wake, imekuwa ikihoji mashinikizo hayo yanazingatia sheria gani na kutaka kujua ni vifungu gani vya sheria ambavyo wadau wa mtandao huo wamevivunja bila kupewa maelezo yanayoridhisha zaidi ya kuelezwa kuwa hatua zaidi zitachukuliwa kama hautatolewa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi.

Baada ya kupata mashinikizo takribani manne yanayoashiria kuwa haki ya watanzania watumiao mtandao wa intaneti na hasa watumiaji wa mtandao wa JamiiForums, Jamii Media imeshauriana na Wanasheria wake na kuona ni wakati sasa wa Kuilinda haki ya wananchi kupata taarifa na kulindwa kwa Uhuru wao wa Maoni na Kujieleza inayolindwa kwa mujibu wa Katiba ya Nchi ibara ya 18 ambapo imefungua Shauri katika Mahakama Kuu ya Tanzania (Kesi namba 9 ya mwaka 2016); kutaka Sheria ya Makosa ya Mtandao, kifungu cha 32 na 38 viangaliwe upya kwakuwa vinapelekea kuvunjwa kwa haki za msingi za watanzania watumiao mitandao ili kulinda maslahi ya umma kwa kuzingatia vifungu 26(2) na 30(3) vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Mtandao wa JamiiForums utaendelea na shughuli zake kama kawaida na utaendelea kuwahakikishia watumiaji wake kuwa mahala salama pa kutolea madukuduku yao na hata kuisaidia Serikali kuonyesha nyufa zilipo kwa maslahi mapana ya Taifa (wakizingatia mwongozo wa ushiriki wa mijadala anuai).

Mwisho, JamiiForums inamuunga na itaendelea kumuunga mkono Rais Magufuli katika jitihada zake za kupambana na ufisadi kwa kutoa uwanja/fursa salama na rahisi kwa wananchi kuweza kuyaainisha yale wanayoyabaini kuwa yanachelewesha maendeleo ya Taifa lao.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents