HabariUncategorized

Je, kula nyama siku ya Ijumaa kuu ni dhambi kwa wakristo? na kwanini hawali nyama maandiko matakatifu yanasemaje?

Leo Aprili 19, 2019 ni siku ya Ijumaa Kuu. Siku ambayo Wakristo duniani kote wanaadhimisha kumbukumbu ya mateso na kifo cha Yesu Kristo msalabani.

Image result for Ijumaa kuu

Kanisa katika moja ya amri zake, linahimiza waamini hususan Wakatoliki kutokula nyama katika siku hii. Hata hivyo, wapo baadhi ya watu wanaoamini kuwa, ni lazima kuacha nyama katika siku hii huku wengine wakiamini tofauti.

Katika jamii nyingi, nyama ni miongoni mwa vyakula vya starehe. Ndivyo inavyoaminika kwa watu wengi. Hivyo, hapana budi kujua kuwa, maana ya msingi ya kutokula nyama katika Ijumaa Kuu, ni moja tu, kufunga starehe. Ijumaa Kuu ni siku ya mateso na kifo cha Yesu Kristo.

Katika mazungumzo na Katibu Mtendaji (Mkuu) wa Idara ya Liturujia wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Paul Chiwangu alisema kwa Mkristo Mkatoliki, kula nyama katika Ijumaa Kuu ni dhambi maana Kanisa linahimiza kujinyima siku hii ili kuyakumbuka mateso na kifo cha Yesu Kristo.

Katika moja ya machapisho ya gazeti la Kiongozi linalomilikiwa na TEC, Padri Titus Amigu aliwahi kuandika akisema, “Mateso hadi kifo cha Yesu msalabani, yamempata kutokana na dhambi zetu hivyo nasi tunakusudia kuacha starehe zetu na tunafunga ili tujutie dhambi zetu.”

“Hii ni kusema kuwa, tunafunga ili tutubu dhambi zetu na Mungu atuonee huruma na kutusamehe dhambi zetu na wengine ambao ni wadhambi kama sisi maana, kufunga, ni mapambano baina yetu na dhambi pamoja na mkuu wa dhambi yaani shetani.”

Injili ya Marko 6:26 inasema kwamba, katika kesi na masuala fulani, shetani hatoki pasipo sala na kufunga. Padri Amigu ambaye ni miongoni mwa wataalamu wabobezi wa Biblia anaandika kuwa, katika suala la kufunga, inampasa mtu kuchagua kitu kizuri cha kukiacha.

Anasema, “Kwa mfano, huwezi kufunga kitu kama kula ugali wa muhogo wakati ugali wa namna hiyo kwako ni shida, bali unafunga kitu kizuri kama labda kula wali na pilau. Huko ndiko kweli kufunga, kujikatalia na kujitesa kwa toba.”

Akaongeza: “Ieleweke kuwa, tangu enzi zile za kale, huko ilikoanzia dini yetu na huko kulikoanzia kufunga, waamini waliacha kula nyama na vitu vitokanavyo kama vile siagi na maziwa kwa vile vilikuwa ni vitu vinavyochukuliwa na kueleweka kuwa ni vya anasa na vile vilivyowakilisha anasa vilipopatikana.”

 “Hilo, ndilo tulilolipokea kutoka kwa wamisionari kwamba, tunapofunga tuache kuvitumia vitu vya anasa na starehe; nyama ikiwa kitu kimojawapo.”

Kimsingi, kwa vile vitu vya starehe hapa duniani sio nyama pekee yake, kila mwamini anaalikwa kukagua vitu vyake vya starehe na hivyo, navyo tuviache siku ya kufunga apate muda zaidi wa kuhuzunika na dhambi zetu tukiomba toba kwa Yesu Kristo aliyesulubiwa kwa ajili ya dhambi zetu.

Kadhalika, katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya, Padre Amigu aliyekuwa Mkuu wa Seminari Kuu ya Peramiho Jimbo Kuu Katoliki la Songea, alisisitiza kuwa, mbali na sababu za kiimani katika dini, pia ipo sababu nyingine ya kibinafsi inayowafanya watu wengine wafunge kula nyama siku kama ya leo.

Akasema, “Hii ni ile sababu ya kufananisha nyama ya kuliwa na mwili au nyama ya Yesu Kristo aliyepigwa mijeledi na kutobolewa na kuchubuliwa na kuachwa akivuja damu nyingi. Hii ni hali inayowafanya wengine, washindwe kula nyama wakiona maiti ya mtu yeyote.”

Akasisitiza kuwa, hii ni sababu ya kibinafsi kwa kuwa Kanisa linapowasisitiza waamini kufunga kula nyama katika Ijumaa Kuu, lina hoja moja kubwa na ya msingi, ile ya kuacha starehe na kufunga na, siyo hiyo nyingine ya kuona nyama kama kitu kinachofanana na nyama au mwili wa Yesu Kristo ambayo kimsingi haina nguvu.

Kwa msingi huo katika Ijumaa Kuu pamoja na kuacha kula nyama tuache starehe zetu, mambo yanayotuvutia ili tukumbuke dhambi zetu na kutubu toba ya dhati inayotoka ndani ya moyo. 

Makala haya yameandikwa na Joseph Sabinus.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents