Tupo Nawe

Je unamwamini mpenzi wako kiasi gani?

Unamwamini mpenzi wako? Mfano ni huu hapa, Je anaweza kwenda likizo wakati wewe haipo likizo? Je unaweza kumruhusu kutoka na ex wake? Au ikitokea amekutana na ex wake mtaani kwa bahati mbaya na wewe ukiwepo unajisikiaje?

Black-woman-white-man

Au unaweza ukamwachia simu yako na usiwe na presha? Hayo maswali yanaweza kukujulisha akilini mwako ni kiasi gani unamwamini mpenzi wako. Kama humwamini mpenzi wako namna utakavyoitikia mambo hayo yanapotokea kuna ishara ambazo zitajulikana wazi kwamba humwamini hata kama unajifanya kupotezea.

Na hii imepelekea wengine hata wanapokuwa wanakwenda bafuni kuoga wanakwenda na simu zao na ikitokea amesahau kwenda nayo ikiita tu atakimbilia kuipokea badala ya kumwambia mume/mkewake au mpenzi wake ‘naomba uipokee simu hiyo.’

Kuna dalili nyingi za kuonesha kwamba hamuaminiani au mmoja hamwamini mwenzie;

Dalili ya kwanza ni nywila au password kwa lugha rahisi. Watu wengi simu zao zina password ambazo wapenzi wao hawazijui kabisa. Huficha password hizo ili kuzuia mwenzie asije akaingia kwenye simu kwa namna yoyote na kuona vilivyomo ndani. Na wengine hata kama kuna password ukishika simu yake anakuwa mkali au anakunyang’anya haraka na kuanza kuitumia kana kwamba alikuwa na kitu bize cha kufanya bali ni mbinu ya kuhakikisha huoni kuna nini kwenye simu yake kwasababu ya kutoaminiana.

Imani kwa mtu ndio kitu pekee ambacho kitasaidia kuweka uaminifu kati yenu wawili. Ingawa kama wewe mwenyewe hujiamini au ni mtu wa kuruka njia , ni ngumu sana kumwamini mwenzio kwani unafikiri anafanya kama unavyofanya. Hali ya kutoaminiana haipaswi kuwepo kwa wapenzi hasa kama mna mpango wa kuishi pamoja maisha yenu yote hapa namaanisha kama unahitaji kujenga uaminifu ndani yako mwenyewe ndipo uweze kuwaamini watu wengine.

Kuna mwandishi mmoja alisema kutokana na kutokuaminiana wakati mwingine tunakuwa na wasiwasi na wapenzi wetu hata wakiwa wamelala huku wakipumua kwa nguvu kama wanaota kitu fulani wewe unaweza kuwaza kwani alikuwa anamwota nani?

Uaminifu hujengwa katika misingi ya kuwa na imani na mtu huyo kwamba alipokubali kuwa na wewe inamaanisha hana mtu mwingine kwenye maisha yake mwenye mahusiano kama mliyonayo. Na fikra hii inatakiwa ianze kwako mwenyewe pale ambapo unaanzisha mahusiano na mtu unatakiwa kujua kwamba hutakiwi kuwa na mtu mwingine ndipo itakuwa rahisi kuamini kwamba mwenzako hana mtu mwingine.

Uwazi wa mambo na sehemu ambazo unakwenda na kila mara
Watu wengi kwasababu ya mambo yao ambayo hawaeleweki huwa ni wasiri sana kiasi kwamba hawapendi kuona kwamba mpenzi wake anatakiwa kujua yuko wapi hivyo kukwepa maswali hayo au kuwa wakali katika kuyajibu maswali hayo. Hiyo ni dalili ya kwamba hujiamini na si mtu wakuaminiwa kabisa kwenye mahusiano. Kuwa muwazi ni jambo la msingi sana, inaondoa ile hali ya kutoaminika na mwenzio. Usiruhusu hata chembe ya kutiliwa mashaka katika maeneo unayokwenda au simu na jumbe fupi za mawasiliano unazopokea mara kwa mara.

Uwazi huo haUmaanishi kwamba usijue kitu gani kinaendelea kwa mwenzako, ni kujua na kuwa na uhakika kwa kila kinachofanyika kwamba hakitaathiri mahusiano yenu. Mfano ni marafiki wa mwenzi wako na hata safari ambazo wanafanya pamoja, unahitaji kujiridhisha kwa kila kitu kwa maana unaweza kuwa ni mtu mzuri lakini watu unaoambatana nao hawaaminiki hivyo na wewe mwenyewe unakuwa huaminiki kulingana na tabia za rafiki zako.

Kitu kingine unatakiwa kuacha uongo kabisa

Kuna wengine uongo kwao ni kama kawaida mara nyingi tunakutana na hali hiyo kwenye daladala mtu anapokea simu labda mko Morocco mnaelekea Makumbusho akaulizwa” Uko wapi?” mtu huyo anajibu “ndio niko Mwenge nakuja Mbezi muda si mrefu”. Sina uhakika kama una mahusiano na huyo mtu na ukajua anadanganya watu wengine je unafikiri wewe umedanganywa mara ngapi?

Mtu kama si mwaminifu anaweza kufanya kitu hapo hapo ulipo si mpaka asafiri kwenda mbali. Hivyo basi kama ni mtu anayejiheshimu hata akisafiri atajiheshimu na kujua kuwa yeye yuko kwenye mahusiano na kama hajiheshimu usipoteze muda ukafikiri akiwa na wewe atabadirika. Unahitaji kuwa na uhakika na mtu mwenyewe kabla ya kuingia kwenye mahusiano naye badala ya kuwa kwenye mahusiano unafanya kazi ya ulinzi na kumlinda kujua yuko wapi na anafanya nini kila saa.

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW