Siasa

Jeetu agonga mwamba

OMBI la mfanyabiashara Jeetu Patel anayetuhumiwa kuwa kinara wa ufisadi katika kuchota mabilioni kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje kutaka hisa zake alizowekeza katika Benki M aziuze kwa raia wa Falme za Kiarabu, halijapata kibali kutoka BoT

Shedrack Sagati


OMBI la mfanyabiashara Jeetu Patel anayetuhumiwa kuwa kinara wa ufisadi katika kuchota mabilioni kutoka kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kutaka hisa zake alizowekeza katika Benki M aziuze kwa raia wa Falme za Kiarabu, halijapata kibali kutoka Benki Kuu (BoT).

Badala yake, BoT imesema ombi hilo bado liko kwenye mchakato wa
kutathmini wanahisa wa benki hiyo, kitendo kinachoelezwa kuwa kinahusisha wadau mbalimbali.

Februari mwaka huu, Jeetu kupitia Benki M alipeleka maombi BoT ya kutaka kuuza hisa hizo kwa Tarek Al Asharam baada ya kuenguliwa katika umiliki wa benki hiyo.

Benki M ilimwengua Jeetu katika umiliki wa benki hiyo kutokana na kukumbwa na tuhuma mbalimbali za kughushi na kujipatia mabilioni ya fedha kwa njia ya uongo. Kwa sasa, anachunguzwa na vyombo vya dola baada ya kutajwa kushiriki katika kuchota mabilioni ya EPA.

Kurugenzi ya usimamizi wa mabenki katika BoT imesema mchakato wa kutathmini wanahisa katika benki hiyo unawahusisha wadau mbalimbali na itachukua muda mrefu kukubali au kukataa maombi hayo.

Jeetu kupitia kwa makampuni yake ya Noble Azania Investments Limited (NAIL) anamiliki asilimia 20 ya hisa za benki hiyo zenye thamani ya Sh bilioni 1.3, wanahisa wengine kwenye benki hiyo ni Negus Holdings Ltd (Sh bilioni 1.3b), Africarriers Ltd (Sh bilioni 1.3), Equity and Allied Limited (Sh bilioni 1.3), Kumar (Sh milioni 650) na Nair (Sh milioni 650).

“Tunapenda kukujulisha kwamba hisa za Benki M bado hazijabadilika na zinamilikiwa na wanahisa wale wale,” ilisema BoT katika barua yake iliyosainiwa na A. Kobelo na A. Ukhotya ambao ni maofisa katika Kurugenzi ya Usimamizi wa Mabenki.

Kurugenzi hiyo ilisema hizo zinazomilikiwa na mfanyabiashara huyo ambaye jina lake kamili ni Jayantkumar Chandubai Patel, hazijauzwa wala kuhamishwa kwa mmiliki ye yote.

Benki M ilipeleka maombi ya kumwengua Jeetu kutokana na matakwa ya kisheria chini ya sheria za benki ya mwaka 2006 na kanuni za taasisi za fedha ya mwaka 1997. Taratibu za BoT zinaeleza kuwa maombi ya kuhamisha hisa ni lazima yafanyiwe tathmini kufuatana na vifungu na kanuni zilizo ndani ya sheria zilizotajwa hapa juu.

Kwa mujibu wa sheria ya benki ya mwaka jana, leseni ya kufungua na kuendesha benki haiwezi kutolewa kwa mtu mwenye historia au rekodi ya makosa ya jinai, kufilisika, kukosa uaminifu au hujuma kwa Serikali.

Watu wengi wamekuwa wanaishutumu BoT kwa kutoa kibali cha kuanzishwa kwa Benki M wakati mmoja wa wanahisa wake ambaye ni Jeetu akiwa na rekodi ya kushiriki kwenye makosa ya jinai.

Kifungu cha 12 cha sheria za benki na taasisi za fedha kinasema mtu anakoma kuwa mkurugenzi na mmiliki wa benki iwapo atabainika kuwa amefilisika au atakapotiwa hatiani kwa makosa ya kughushi au ya kutokuwa mwaminifu. Katika kifungu hicho pia inaeelezwa kuwa mtu anakoma kuwa mkurugenzi wa benki iwapo ataondolewa na bodi ya benki husika.

Jeetu kupitia kampuni tisa anatuhumiwa kuchota mabilioni ya fedha katika BoT. Kampuni hizo ni Bencom International Ltd, B. V Holdings Ltd, Venus Hotels Ltd, V.B Associates Company Ltd, Bina Rosort Lt na Bora Hotels & Apartment. Kampuni zake nyingine zinazotajwa kutumika kwenye ufisadi huo ni Maltan Mining Company, Ndovu Soaps Ltd na Navy cut Tobacco Tanzania Ltd.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo Nimrod Mkono, Februari mwaka huu alinukuliwa na gazeti hili akithibitisha kuwa tayari benki hiyo imeshamwengua Jeatu katika umiliki na ukurugenzi wa benki hiyo. “Sio mkurugenzi tena…tumeona hatuwezi kuendelea kuwa na mtu ambaye ana kashfa nyingi kiasi hicho,” Mkono aliliambia gazeti hili.

Kutokana na kushiriki katika uchotaji wa mabilioni ya EPA, Jeatu ni mmoja wa watu wanaochunguzwa na Timu maalumu iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete inayoongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika. Wengine katika timu hiyo ni Wakuu wa Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents