Habari

Jifunze haya toka kwa Jack Ma: Bilionea aliyekataliwa mara nyingi zaidi

Tujifunze kutoka kwa ‘Ma Yun’ maarufu kwenye ulimwengu wa biashara ya mtandao kama Jack Ma. Bilionea kutoka China mwanzilishi na mwenyekiti mtendaji wa Alibaba Group, moja ya familia ya biashara ya mtandao iliyofanikiwa zaidi duniani.

Jack Ma ni mtu wa kwanza kutoka China (Mainland China) kuonekana kwenye kurasa ya mbele ya jarida maarufu la Forbes. Mwaka 2014 dunia ilishuhudia IPO (Initial Public Offering- kuuzwa kwa mara ya kwanza kwa hisa za kampuni kwenye soko la hisa) kubwa zaidi kuwahi kutokea duniani kwenye soko la hisa la Newyork, na kuifanya Alibaba group kuweka rekodi kama world’s biggest public stock offering.

Pamoja na kupingwa mara kwa mara kuwa Alibaba hawaweki nguvu ya kutosha katika kuzuia udanganyifu wa mauzo kwenye mtandao wa Alibaba, Ma bado anaipeleka Alibaba kwenye mauzo ya hali ya juu na mafanikio makubwa. Rekodi ya shughuli za kibiashara zipatazo $463 bilioni zilifanyika kupitia mtandao wa Alibaba mpaka mwezi machi 2016.

Kampuni ya Alibaba imeweka malengo ya kutengeneza biashara zenye faida milioni 10 na si chini ya ajira milioni 100 kwa miaka 20 ijayo.
Mafanikio sio ajali. Haikumchukua Jack Ma usiku mmoja kufikia hatua hii kubwa na inayoshangiliwa kila kona ya dunia. Ilimgharimu mapambano na kukataliwa mara kadhaa lakini alisonga mbele.

Ma alianza kujifunza Kiingereza katika umri mdogo na kwa bidii ya hali ya juu, na hapo ndipo alipopata jina la “Jack” baada ya rafiki wa kigeni kushindwa kutamka jina lake la kichina. Akiwa kijana mdogo, Ma alihangaika kuingia chuo kikuu. Mitihani ya kujiunga na chuo kikuu hufanyika mara moja kila mwaka nchini China na ilimchukua Jack Ma miaka minne kufanikiwa, akajiunga kusoma digrii ya kiingereza-B.A in English (Jinsi gani Ma alipenda kiingereza).

Baada ya kumaliza chuo Jack ma aliomba kazi 30 tofauti bila mafanikio, zote alikataliwa. “Niliomba kazi ya upolisi; wakasema ‘wewe sio mzuri kwa kazi hii” Ma alimwambia mwanahabari Charlie Rose. KFC walivyoenda kwa mara ya kwanza kuanzisha biashara kwenye mji anaotoka Ma, Watu 24 waliomba kazi, 23 walifanikiwa kupata kazi. Alikuwa ni Jack Ma peke yake ambaye alikosa kazi hiyo. Lakini pia Ma aliomba kujiunga na chuo kikuu cha Harvard mara kumi na mara zote alikataliwa.

Maisha ya Jack ma ni ushahidi mwingine mkubwa wa bilionea aliyekutana na vikwazo na kukataliwa mara nyingi zaidi, lakini hakukata tamaa. Moja ya misimamo mikuu katika maisha yake ni kuzoea kukataliwa (Get used to rejection) na kuendelea kuifanya ndoto yako iishi (Keep your dream alive). May 2015 kwenye kituo cha televisheni cha KBS cha nchini Korea ya kusini, Ma alizungumza na vijana na wajasiriamali wadogo na kuwapa maneno yenye nguvu kubwa mno kwenye maisha yao , alisema ; Usiogope kila kosa unalofanya ni kipato kwako, kabla ya miaka 20 kuwa mwanafunzi mzuri, jifunze kwa nguvu. Kabla ya miaka 30 kuwa mfuasi wa mtu mwenye mafanikio, mwenye uzoefu na anayefanya vizuri kwenye maisha yake, nenda kwenye kampuni ndogo ndogo, mara nyingi kwenye kampuni kubwa ni kama unakuwa part of the big machines. Lakini ukienda kwenye kampuni ndogo ndogo unajifunza kuwa na shauku, unajifunza kuhusu ndoto zako. Unajifunza kufanya vitu vingi kwa wakati mmoja. Kitu muhimu kabla ya miaka 30 sio kampuni gani uliyofanyia kazi, lakini ni bosi wa aina gani umekuwa chini yake. Hii ni muhimu sana, kwasababu kila bosi anakufundisha tofauti.

Ukiwa chini ya miaka 40 unahitaji kuchukua muda wako na kujiuliza kwa makini sana, kama unataka kufanya kazi kwaajili yako na kama kweli unataka kuwa mjasiriamali. Miaka 40 mpaka 50 hakikisha unafanya vitu ambavyo una uwezo navyo na unavijua zaidi, sio muda wa kujaribu tena. Weka malengo na maisha yako, kama Mungu atakupa uhai ukafika miaka 60 wekeza kwa vijana, fanya kazi na vijana kwasababu wao wana nguvu kuliko wewe, wanafikiri vizuri kuliko wewe. Ukiwa ndani ya miaka ya ishirini fanya makosa mengi, fanya makosa kadri ya uwezo wako kwa lengo la kujifunza zaidi.

Haijalishi ni mara ngapi umejaribu ukashindwa na kukataliwa, usiache kusonga mbele, unahitaji kufanikiwa mara moja tu kwenye maisha yako. Unahitaji kutengeneza uvumilivu mkubwa na hali ya kutokukatisha mambo yako (Procrastination). Jifunze zaidi katika umri mdogo kuliko kufikiria kulipwa pesa nyingi tu, work to learn and money will follow you. Tembea na ndoto zako popote uendako na uzifanyie kazi kila siku bila kuchoka wala kukata tama mpaka pale ushindi wako utakapotengeneza historia kama Jack Ma na Alibaba.

Imeandikwa na :
Japhet Lutambi
E-mail: [email protected]

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents