Siasa

JK akwaa tuzo Marekani

Muungano wa wafanyabiashara wenye asili ya Afrika waishio nchini Marekani (Leon Sullivan), umempa tuzo Rais Jakaya Kikwete kufuatia kukubali kufanyika mkutano huo nchini kwake.

Na Sammy Polly



Muungano wa wafanyabiashara wenye asili ya Afrika waishio nchini Marekani (Leon Sullivan), umempa tuzo Rais Jakaya Kikwete kufuatia kukubali kufanyika mkutano huo nchini kwake.


Hali kadhalika, Sullivan imempa tuzo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Bi. Asha-Rose Migiro kutokana na juhudi alizozifanya kuimarisha amani kwenye eneo la Maziwa Makuu kipindi alichokuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mwaka 2006.


Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Mambo ja Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe alipokuwa akizungumza na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dar es Salaam.


Waziri Membe alikuwa akitoa taarifa kuhusu mkutano wa viongozi wa Nchi za Ulaya (EU) na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika (AU) ambao umemalizika mjini Lisbon Ureno, Desemba 9 mwaka huu pamoja na ziara ya Rais Kikwete nchini Marekani iliyomalizika juzi.


Bw. Membe alisema kwamba Leon Sullivan wamemtunukia heshima hiyo Rais Kikwete kwa kukubali mkutano huo ufanyike mjini Arusha ambapo washiriki takribani 3,000 wanatarajiwa kuhudhuria.


“Tayari tumeshaanza kuunda kamati mbalimbali ili kuweza kuhakikisha kwamba kila kitu kinakamilika kwa wakati kabla ya mkutano huo kuanza mwezi Juni,“ alisema.


Waziri Membe alisema kwamba mkutano wa Lisbon ambao ulifanyika kuanzia Desemba 8 hadi 9, mwaka huu ulikuwa wa mafanikio makubwa kwa pande zote.


Alitaja baadhi ya madhumuni ya mkutano huo kuwa ni uimarishaji mahusiano baina ya mabara hayo, kujenga mikakati ya kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa, uhamiaji haramu, utawala bora, haki za binadamu na biashara.


Alisema kwamba wajumbe wa mkutano huo walijenga mikakati kufuatia Shirika la Biashara Duniani (WTO) kuamuru kwamba ifikapo Desemba 31, mwaka huu bidhaa zote zitokazo Afrika na kupelekwa Ulaya zitozwe ushuru.


Alisema kwamba endapo Afrika itaruhusu bidhaa zitokazo Ulaya zisitozwe ushuru serikali itapoteza mapato, kutaongezeka ukosefu wa ajira na kusababisha viwanda vilivyopo nchini kufungwa kwa kukosa masoko.


Hata hivyo Waziri Membe alisema kwamba bidhaa nyingi za kilimo zitokazo Tanzania zinakosa masoko makubwa Ulaya kutokana na udhaifu wa kuzifunga vizuri.


Alisema kwamba mkutano wa Lisbon haukulipa uzito suala la mgogoro wa Zimbabwe ingawa wawakilishi kutoka nchi za Zimbabwe na Uingereza walishiriki kikamilifu katika kikao hicho.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents