Siasa

JK awakutanisha viongozi kuijadili Zimbabwe

Rais Jakaya KikweteMwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Kikwete, amekutana na viongozi mbalimbali duniani kujadili masuala makubwa likiwepo la Zimbabwe na kuchelewa kutangazwa kwa matokeo ya kura za urais

Rais Jakaya Kikwete


 


Na Mwandishi Maalum, New York


Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Kikwete, amekutana na viongozi mbalimbali duniani kujadili masuala makubwa likiwepo la Zimbabwe na kuchelewa kutangazwa kwa matokeo ya kura za urais kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika Machi 29 mwaka huu.

Siku 20 zimepita tangu Zimbabwe ilipofanya uchaguzi mkuu wa Rais na wabunge.

Katika mkutano wa awali uliotangulia mwingine wa masuala ya migogoro ya Afrika, Rais alikutana na Waziri Mkuu wa Uingereza Bw. Gordon Brown na suala la Zimbabwe ndilo lililotawala mkutano huo wa nusu saa.

Na katika hatua nyingine Mwenyekiti AU ametoa changamoto kadhaa kwa Umoja wa Mataifa (UN) za kuongeza mahusiano yake na AU , ili kwa pamoja vyombo hivyo vifanikiwe kutatua migogoro ya Afrika.

Rais Kikwete alitoa mapendekezo hayo mahsusi wakati anahutubia kikao maalum cha ngazi ya juu cha pamoja kati ya Baraza la Usalama la UN na Baraza la Amani na Usalama la AU.

Akizungumza mjini New York Marekani juzi, Rais alisema kuna umuhimu wa taasisi hizo mbili kuweka utaratibu wa jinsi UN inavyoweza kuingilia migogoro ya Afrika bila kusababisha mgongano na AU.

Kikao hicho kilikuwa kinatafuta njia za jinsi taasisi hizo zinavyoweza kushirikiana katika kutatua migogoro ya kisiasa ya Afrika.

Alisema kuna wakati AU inaona umuhimu wa kuingilia haraka na kumaliza tatizo katika nchi ya Afrika na inafanya hivyo, hata kama wajibu mkuu wa kumaliza migogoro duniani ni wajibu wa UN.

Alisema hilo linaweza kusababisha mgongano kati yake na AU kama halikuwekewa taratibu na mipaka inayojulikana na kukubaliwa na kila taasisi na UN na kuendeshwa na taasisi za kikanda kama AU, kugharimiwa na UN.

Kwa sasa taratibu za UN hairuhusu Umoja huo kugharimia shughuli hizo, hata kama zimeidhinishwa na Baraza la Usalama la UN.

Kikao hicho cha aina yake kimeitishwa na Afrika Kusini ambayo ndiyo Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la UN kwa mwezi huu.

Rais Kikwete pia alikutana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Marekani anayeshughulikia masuala ya Afrika, Jendayi Fraser, suala kubwa katika mkutano huo lilikuwa ni hali ya Zimbabwe na jinsi AU na Marekani zinavyoweza kuchangia katika kuhakikisha uchaguzi katika nchi hiyo unakamilika na kutangazwa matokeo ya urais.


 


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents