Siasa

JK hapo sawa!

Baadhi ya wanasiasa na wasomi hapa nchini, wameunga mkono hatua ya Rais Jakaya Kikwete ya kutaka kutungwa sheria itakayowazuia wanasiasa kuwa na kazi mbili ya siasa na biashara kwa wakati mmoja.

Na Richard Makore

 
Baadhi ya wanasiasa na wasomi hapa nchini, wameunga mkono hatua ya Rais Jakaya Kikwete ya kutaka kutungwa sheria itakayowazuia wanasiasa kuwa na kazi mbili ya siasa na biashara kwa wakati mmoja.

 

Walitoa maoni hayo jana walipokuwa wakizungumza na Nipashe kwa nyakati tofauti.

 

Akizungumzia hatua hiyo, Naibu Waziri wa Miundombinu, Dk. Makongoro Mahanga alisema, hatua hiyo ya Rais itasaidia sana hata ndani ya CCM.

 

Alisema ikiwa wanasiasa watazuiwa kujihusisha na biashara, itasaidia viongozi kufanya kazi kwa uwazi na kuondoa hisia za watu kwamba wanatumia madaraka yao katika kufanikisha biashara wanazofanya.

 

Dk. Mahanga alisema, wafanyabiashara kuvamia siasa ni hatari kwa sababu wapo watu wanaopata ubunge wakati hata hawajui kutamka kidumu Chama Cha Mapinduzi.

 

Aidha, Dk. Mahanga alisema, rushwa imezidi katika kipindi hiki baada ya wafanyabiashara kuvamia siasa kuliko wakati wowote hapa nchini.

 

Alisema mfanyabiashara akiambiwa kuacha biashara na kuingia katika siasa, hawezi kukubali jambo linaloonyesha kwamba wanataka wafanikiwe vyote kwa maslahi yao binafsi.

 

Kadhalika, Dk. Mahanga alisema, mfanyabiashara kuwaambia wananchi kwamba endapo akichaguliwa atawaletea maendeleo, ni uongo kwa sababu maendeleo ni mchakato mrefu.

 

Naye Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe cha mjini Morogoro, Bw. Ibrahim Kaduma alisema, anampongeza Rais japo amechelewa lakini anaamini hatua hiyo italisaidia taifa.

 

Alisema awamu ya kwanza ya uongozi ilikuwa na misingi kama hiyo na kwamba Rais Kikwete anataka kuwarudisha wananchi katika mfumo unaowawezesha wananchi wote kupata haki.

 

Aliwataka viongozi wote wanaojijua ni wafanyabiashara, kujiondoa haraka katika nafasi zao kabla ya Rais kuwaondoa.

 

Aidha, alitahadharisha kwamba, viongozi wa serikali ya sasa wasihusishwe katika kutunga sheria hiyo aliyopendekeza Rais Kikwete kwa sababu wanaweza kuihujumu.

 

“Hawawezi kutunga sheria ambayo wanajua inawahusu kwa sababu viongozi wengi ni wafanyabiashara,“alisema.

 

Alisema sheria hiyo iwalenge viongozi wote wanaowania madaraka bila kujali vyama wanavyotoka iwe CCM au upinzani.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TLP, Bw. Augustine Mrema alisema, kuwazuia viongozi wa umma kufanya biashara ndiyo ilikuwa misingi ya Azimio la Arusha.

 

Alisema kunatakiwa kuwepo na nia ya kweli katika kulitekeleza jambo hilo ili liweze kupata manufaa.

 

Alihoji kama Rais ana uwezo wa kutekeleza kauli yake kwa sababu amezungukwa na viongozi wengi wafanyabiashara.

 

Akitoa maoni yake alipozungumza na Nipashe, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mwesiga Baregu alisema, hatua ya wafanyabiashara kuacha kujihusisha na siasa, ni jambo ambalo haliwezi kuepukika hivi sasa.

 

Profesa Baregu alisema, wapo watu wengi wenye nia njema na moyo thabiti wanaoweza kuongoza wananchi pamoja na kuwaletea maendeleo, hivyo ni bora wafanyabiashara wakajiondoa wakabaki na biashara zao.

 

Aliwashauri Watanzania kujiangalia upya ili kupata mfumo unaomwezesha mwananchi wa kawaida akiwemo mkulima, kupata fursa ya kufaidi matunda ya nchi yake.

 

Alisema wafanyabiashara wanaong`ang`ania siasa, hawawezi kuwapeleka Watanzania mahali pazuri bali kuwaacha wakiwa hohehahe.

 

Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa Nchini, Bw. John Tendwa alisema, matatizo yote haya yanatokana na Azimio la Zanzibar ambalo lilitoa mwanya kwa viongozi wa umma kuwa na shughuli nyingine za kuwaongezea kipato.

 

Alisema ipo Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo inaangalia mwenendo na shughuli wanazozifanya.

 

Alikiri kwamba, mtu hawezi kuwa waziri halafu akawa mfanyabiashara wakati huo huo mmoja kwa sababu anaweza kutumia nafasi yake kujinufaisha kibiashara.

 

Alitoa mfano kuwa, kiongozi anaweza akaamua kwenda jijini Mwanza kwa madai kuwa anakwenda kukagua miradi ya maendeleo kumbe anakwenda kuangalia biasahara zake.

 

Alifafanua kuwa, Sheria ya Takrima ni moja ya sababu zilizochangia kupata viongozi wafanyabiashara.

 

Alisema mfanyabiashara mwenye fedha, hawezi kushindana na mwananchi wa kawaida katika kugombea nafasi za uongozi.

 

Alisema wengi wa mawaziri wana viwanda jambo ambalo linawafanya washindwe kuwajibika hata katika Baraza la Mawaziri.

 

Alishauri kuwa, hatua hiyo ya Rais lazima ichukuliwe kwa umakini unaostahili ili kuwawezesha viongozi kuwajibika kwa wananchi.

 

Naye Bi. Sarah Hamza mkazi wa Manzese alisema, viongozi wanaotaka kufanya kazi mbili ndiyo chanzo cha kuwafanya wananchi kuendelea kuwa maskini.

 

Bi. Hamza alisema, viongozi wengi wanatumia vyeo vyao katika kuimarisha makampuni wanayomiliki badala ya kuangaliz umaskini unaowakabili watu wanaowatumikia.

 

Bw. Kasongo Mwinyimvua mkazi wa jijini Dar es Salaam alisema, Rais Kikwete inaonyesha anayo nia njema ya kutaka kuwasaidia Watanzania lakini jambo hilo lazima liharakishwe.

 

Alisema wakati wa awamu ya kwanza ya uongozi chini ya marehemu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wafanyabiashara walikuwa wanaogopa siasa kama ukoma.

 

Alisema wakati ule fedha ilikuwa ni moja ya sifa za kumuondoa mtu kugombea uongozi lakini sasa imekuwa kinyume chake.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents