Siasa

JK: Sijashindwa

WAKATI baadhi ya Watanzania wakionyesha kukata tamaa kwa utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Nne, Rais Jakaya Kikwete, amesema kuwa hawajashindwa kutekeleza alichokiahidi miaka miwili iliyopita.

na Martin Malera


WAKATI baadhi ya Watanzania wakionyesha kukata tamaa kwa utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Nne, Rais Jakaya Kikwete, amesema kuwa hawajashindwa kutekeleza alichokiahidi miaka miwili iliyopita.


Rais Kikwete ambaye leo anatimiza miaka miwili kamili ya kukaa Ikulu tangu alipoapishwa rasmi Desemba 21 mwaka 2005, alitamba kwamba, katika kipindi hicho, serikali yake imeweka misingi imara katika nyanja zote ili kuhakikisha kuwa azima ya kuwapatia Watanzania maisha bora inafanikiwa.


Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, Ikulu Dar es Salaam kuhusu maadhimisho hayo, Kikwete aliyekuwa akizungumza kwa utulivu, alitaka watu watambue kuwa bado walikuwa na muda wa kutosha kukamilisha yote waliyoahidi.


“Kumbukeni kwamba utekelezaji wa ahadi zetu ni hadi mwaka 2010. Sina wasiwasi na mafanikio tuliyofikia kwa hii miaka miwili na tukayofikia mwaka 2010 na wananchi watatupima kwa mafanikio hayo,” alisema.


Alisema msingi huo uliosimikwa kwa juhudi za Serikali yake, utasaidia sasa kujenga matofali na kutamba kuwa mwaka 2010 hana wasiwasi kwani wananchi wataweza kuwapima kwa mafanikio yatakayofikiwa na serikali yake.


Alitaja baadhi ya mafaniko hayo kuwa yapo katika sekta ya afya, maji, elimu, na ujenzi wa barabara, ambapo katika kipindi cha miaka miwili, serikali yake imefanikiwa kujenga kilomita 1,174 za barabara ya lami na mipango imekamilika kuanza ujenzi wa barabara kadhaa zikiwemo barabara za Tunduru-Songea-Mbambabay, Tanga-Horohoro na Manyoni-Kigoma.


Kutokana na hali hiyo, Rais Kikwete aliwataka wananchi kuendelea kuiunga mkono na kuiamini serikali akisema alikuwa ana uhakika kuwa wakati utakapofika mwisho, watakuwa wamefanikiwa kutekeleza miradi mingine iliyoahidiwa.


Akielezea serikali yake, Rais alisema kuna watu ambao wamekuwa wakiwaona baadhi ya viongozi kuwa ni watu wasio na uchungu na nchi yao, jambo alilosema si la kweli hata kidogo.


Kuhusu hili, aliwataka wananchi kuwaamini kwani serikali yake ilikuwa ikiundwa na watu wasikivu na ambao wako tayari kulifanyia kazi jambo lolote kwa masilahi ya taifa.


“Wapo watu wanaodhani kuwa serikali hii ni mkusanyiko wa majitu yasiyo na uchungu na nchi yao, si kweli. Serikali yangu ni sikivu, tunasikiliza kila jambo na kulifanyia kazi.


Hata mtu akinitumia ujumbe kupitia simu yangu ya mkononi juu ya tatizo lolote, nalifanyia kazi, ndiyo maana nimeunda kamati ya madini ili kuondoa kelele za madini,” alisema.


Alisema kutokana na dhamira hiyo hiyo ya kujali na kukisikia kilio cha wananchi ndiyo maana alifikia uamuzi wa kuunda kamati ya kupitia upya mikataba ya madini.


Kuhusu hilo, Kikwete alitumia fursa hiyo kukanusha madai kwamba alilazimika kuunda kamati hiyo inayoongozwa na Jaji mstaafu, Mark Bomani kutokana na shinikizo la wapinzani.


“Nilichotaka hapa ni kuondoa kelele. Sijaunda kamati hii kutokana na kelele za wapinzani. Nakumbuka mara ya kwanza kuelezea nia ya kutaka kuunda kamati ni pale nilipokuwa Afrika Kusini, na nilizungumzia tena Dodoma kwenye Mkutano Mkuu (wa CCM),” alisema.


Alirejea kauli yake ya mara kwa mara kwamba, kazi ya kamati hiyo si kumtafuta mchawi bali ni kurekebisha makosa yaliyofanyika miaka ya nyuma ili kuhakikisha madini yanawanufaisha pia Watanzania.


Hata hivyo wakati akizungumzia mafanikio, rais alieleza kuguswa na kusononeshwa na tatizo la mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali linaloendelea kulikabili taifa.


“Mfumuko wa bei hata mimi unanikera unaniumiza kichwa. Hata hivyo bado sijajua kiini cha tatizo hilo, na serikali inalifanyia kazi, maana wapo wanaosema mfumuko wa bei umeongezeka kwa nguvu na kasi mpya,” alisema.


Alisema sababu kubwa ya hali hiyo kwa haraka haraka inaweza kuwa ni kupanda kwa bei ya mafuta, suala ambalo alisema serikali yake ilikuwa ikiangalia namna ya kukabiliana nalo.


Wakati Kikwete akisema hivyo, taarifa rasmi ya Benki Kuu ya Tanzania iliyotoka katikati ya mwaka jana ilikuwa ikionyesha kuwa, matatizo ya ukame, umeme na ukosefu wa chakula cha kutosha, ni mambo ambayo yalisababisha mfumuko wa bei kupanda kutoka asilimia 4.2 mwaka 2005 hadi kufikia 6.9.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents