Siasa

JK:Nitatekeleza ahadi zangu zote

RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) itazitekeleza ahadi zote ilizowaahidi wananchi na kwamba wale wanaosema itashindwa, walie tu.

Mwandishi Maalumu, Rombo


RAIS Jakaya Kikwete amesema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) itazitekeleza ahadi zote ilizowaahidi wananchi na kwamba wale wanaosema itashindwa, walie tu.


Amewahakikishia maelfu ya wananchi waliohudhuria mkutano wake wa hadhara katika mji mdogo wa Tarakea jana, kuwa serikali yake imejiandaa kikamilifu kuzitekeleza ahadi hizo hatua kwa hatua kama ambavyo imeshaanza kuzitekeleza ahadi hizo.


Rais aliyewasili wilayani Rombo akitokea wilayani Mwanga, katika vijijini vyote alivyopita akiwa njiani kwenda Tarakea, alilakiwa na mamia ya wananchi waliofunga barabara wakimtaka asimame na kusalimiana naye na yeye alifanya hivyo.


“Ndugu wananchi nimekuja kuwasalimia, kwanza nawashukuru kwa mapokezi makubwa ambayo hayajawahi kutokea kote nilikowahi kufika. Nimekuja kuwashukuru kwa kutuchagua, tulikuwa wengi, lakini mkasema mnamtaka Kikwete, vilikuwapo vyama vingi, lakini mkasema mnaitaka CCM.


“Kwa hiyo nimekuja kuwashukuru. Na kuwaambia kwamba tutatekeleza kila tulichoahidi wakati wa kampeni na kwenye Ilani ya CCM,” alisema Rais.


“Wako wale wanaosema wakati wa kampeni tuliahidi mambo mengi lakini hatutawezi kuyatekeleza. Lakini sisi tunatekeleza kile tulichokiahidi na tumeanza kazi, hivyo wao walie tu,” alisisitiza na kushangiliwa na umati wa wananchi.


Katika wilaya hiyo ya Rombo, Rais alipokelewa na makundi ya watu huku wengine wakifunga njia na kumlazimisha asimame na kuwasalimia.


Rais Kikwete alisema ahadi ya kuitengeneza barabara ya kutoka Kilacha kupitia Rombo Mkuu hadi Tarakea itakamilika na kwamba tayari mkandarasi amekwisha kuanza kazi.


“Nimekuja kuwahakikishia kwamba hili vumbi mnaloliona kwenye barabara na kwenye mabati ya nyumba zetu, ni vumbi la mwisho, baada ya muda mfupi litakuwa limekwisha, kwa sababu mkandarasi ameshaanza kazi,” alisema Kikwete.


Alisema kwamba katika mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga asilimia 75 ya bajeti yake kwa ajili ya ujenzi wa barabara nchini, kwa kuwa inatambua kwamba barabara ndiyo mhimili mkuu wa uchumi.


Kuhusu tatizo la maji katika baadhi ya vijiji vya wilaya hiyo, alisema ingawa serikali haina uwezo mkubwa, lakini kwa kushirikiana na marafiki mbalimbali duniani, inao uwezo wa kufanya mengi ya kuboresha huduma muhimu na za msingi kwa maisha ya Watanzania.


Katika mkutano huo, Rais pia aliwasisitiza wananchi kutoacha kupeleka watoto wao shule, kuendelea kujitolea katika ujenzi wa shule za sekondari, zahanati na vituo vya afya na kujihadhari dhidi ya Ukimwi.


Akielezea zaidi kuhusu Ukimwi ambao katika wilaya hiyo kiwango cha maambukizi ni asilimia saba, Rais aliwataka wananchi hao kuwa waangalifu na kujikinga na maambukizi na hasa kwa kuwa Tarakea ni kituo kikubwa cha biashara.


“Tafadhali wananchi, ujumbe wangu mpya leo kwenu ni kuhusu ugonjwa wa Ukimwi, hapa kwenu Ukimwi upo kwa wingi kwa sababu ni kituo cha biashara. Sasa nawaomba mchukue tahadhari zote za kujikinga na maambukizi, lakini pia jitokezeni mkapime na msiwanyanyapae wagonjwa wa Ukimwi,” alisema Rais Kikwete.


Rais aliiagiza Idara ya Wanyamapori kuweka kituo katika eneo ambalo tembo hupita na kwenda kwenye vijiji na kuharibu mazao na kuhatarisha maisha ya wananchi.


Pia amewataka wananchi kuendelea na juhudi za kuhifadhi mazingira ili Mlima Kilimanjaro usipate madhara zaidi.


Rais pia aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa soko la kisasa kwa ajili ya mazao ya wakulima.
Soko hilo ambalo hadi kukamilika kwake litagharimu Sh milioni 237.8, ujenzi wake unagharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB), Serikali Kuu na Halmashauri ya Wilaya ya Rombo.


Soko hilo la kisasa litawapa wakulima mazingira mazuri ya kufanyia biashara zao za mazao ya kilimo, lakini pia litatoa bei nzuri za mazao kwa wakulima, kuongeza mapato kwa halmashauri na mapato kwa Serikali Kuu kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania.


Rais pia alizindua kituo cha kulelea watoto yatima cha Cornel Ngaleku na akaweka jiwe la msingi la ujenzi wa Shule ya Sekondari Shimbi.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents