JWTZ watembeza mkong’oto kwa raia

WATU wanaodaiwa kuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), wanatuhumiwa kuwashambulia raia katika mji mdogo wa Mbalizi,
mkoani Mbeya

NA SOLOMON MWANSELE, MBEYA


WATU wanaodaiwa kuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), wanatuhumiwa kuwashambulia raia katika mji mdogo wa Mbalizi,
mkoani Mbeya.


Askari hao walitembeza mkong’oto kwa raia kwa kutumia mikanda na fimbo, hivyo kuwajeruhi baadhi.

Askari hao kutoka 44KJ, wanadaiwa kuwashambulia raia juzi saa 2.30 usiku, akiwa zaidi ya 30.


Baadhi ya wakazi wa Mbalizi wakizungumza na Uhuru jana, walisema hawaelewi chanzo cha askari hao kuwashambulia.

Hata hivyo, inadaiwa kuwa, askari mmoja wa kikosi hicho aliporwa simu ya mkononi, hivyo walikuwa wakilipiza kisasi.

Mfanyabiashara wa nyama Emmanuel Mathayo (20), alisema alishangaa
kuona akivamiwa na kundi la askari alipokuwa katika harakati za kufunga
biashara zake.


Mathayo alisema wakati akiendelea kuhesabu fedha za mauzo ya siku
hiyo, alijikuta akipigwa mkanda shingoni, ambao ulichana sikio lake la
kulia.


"Nilishikwa na bumbuazi… sikutegemea kitendo hicho, nilishika
sikio nikakuta damu zinavuja… kiganja cha mkono wa kulia damu ilikuwa
ikitoka," alisema Mathayo.


Naye Hanifa Mwambope, alisema mume wake Carlos Mboya (28), mkazi
wa eneo la Mtakuja, amejeruhiwa kichwani na vidole viwili vya mkono wa
kulia vimevunjika.


Kwa mujibu wa Hanifa, mumewe aliondoka dukani akiwa na rafiki yake
Fidelis, ambaye ni askari wa JWTZ kutoka kikosi hicho, huku akimtaka
amsubiri.


Hanifa alisema baada ya kuona muda umepita na hajarejea, alimpigia
simu mumewe, ambaye alipokea na sauti yake haikuwa ya kawaida. Alisema
aliporudi dukani saa 2.40 usiku, alikuwa amelowa damu.


Alisema Mboya alipoulizwa kulikoni, alieleza kwamba, alivamiwa na
kundi la askari wa JWTZ, ambao walikuwa wakimpiga kila mtu waliyekutana
naye njiani.

"Kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata alikwenda kutibiwa katika hospitali teule ya Ifisi,” alisema Hanifa.

Kwa upande wake, Elia Jengela (28), alisema alikutana na askari hao
saa 2.30 usiku, akiwa nje ya baa ya Chisambo, alikokwenda kununua
sigara.


Jengela alisema askari hao walimvamia na kuanza kumpiga kwa
kutumia mikanda ya kijeshi na fimbo na alipohoji kulikoni hakupata
jibu.


Alisema amejeruhiwa kichwani na miguuni na alikwenda kutoa taarifa
kituo cha polisi Mbalizi, alikopewa hati ya kumwezesha kwenda kupata
matibabu.


Naye Stella Mwakabenga (30), mmiliki wa ‘saluni’ ya kike ya
Avocado, alisema alisikia kelele za watu kutoka nje na alipotoka
alikuta watu wakikimbia ovyo.


Stella alisema alifunga mlango, lakini ulipigwa teke na kusababisha kioo cha mlango huo chenye thamani ya sh. 40,000 kuvunjika.


Kwa mujibu wa Stella, mwenzake aliyemtaja kuwa Agness, alijeruhiwa
kichwani kwa vipande vya vioo na alikwenda kutibiwa hospitalini.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Zelothe Stephen, hakupatikana
kuzungumzia tukio hilo. Ilielezwa kuwa alikuwa kwenye mapokezi ya mbio
za Mwenge wa Uhuru wilayani Chunya.

 

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents