Habari

Kamati ya Richmond yapewa wiki nne

Kamati teule iliyoundwa na Bunge kuchunguza mkataba wa Richmond, imepewa wiki nne kukamilisha kazi yake.

Na Beatrice Bandawe, Dodoma



Kamati teule iliyoundwa na Bunge kuchunguza mkataba wa Richmond, imepewa wiki nne kukamilisha kazi yake.


Naibu Spika wa Bunge, Bi. Anne Makinda aliliambia Bunge jana asubuhi baada ya kipindi cha maswali na majibu kuwa, Kamati hiyo inatakiwa kuwasilisha taarifa yake ifikapo Desemba 15, mwaka huu.


Aidha, kamati hiyo ya watu watano, leo inatarajiwa kukutana na Spika wa Bunge, Bw. Samuel Sitta.


Kamati hiyo inayojumuisha Wabunge, Dk. Harrison Mwakyembe, Bi. Stella Manyanya, Bw. Mohamed Mnyaa, Bw. Lucas Seleli na James Mtangi, ilitangazwa juzi usiku na Spika Sitta.


Aliitangaza baada ya Wabunge kushinikisha kuundwa kwa chombo hicho kitakachokuwa na uwezo wa kisheria wa kupata mkataba wa kampuni ya Richmond na kuchunguza mchakato mzima ulifanywa hadi kuteuliwa kwake.


Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na Biashara, Bw. William Shellukindo, juzi asubuhi aliwasilisha taarifa ya kamati hiyo iliyokuwa inazungumzia utata wa kampuni hiyo ya Richmond ilivyopata zabuni ya kuingia mkataba wa uzalishaji umeme nchini.


“Waheshimiwa wabunge, napenda kuwatangazia kuwa Kamati Teule, iliyoteuliwa kuchunguza mkataba wa Richmond itafanya kazi hiyo kwa wiki nne ambapo Desemba 15, mwaka huu, wanatakiwa wawe wamemaliza,“ alisema Bi. Makinda.


Baadhi ya majukumu ambayo Kamati imepewa, ni kufuatilia ni nani Richmond na ni mali ya nani, ilipataje zabuni ya kuzalisha umeme na kama njia iliyotumika kuipa kampuni hiyo zabuni ilikuwa halali.


Kamati hiyo pia itatathmini mkataba kati Richmond na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO).


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents