Habari

Kampeni ya wanandoa watarajiwa kupima ukimwi yaanza Z`bar

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imesema ofisi ya Mufti Zanzibar imeanza kampeni kwa wanandoa watarajiwa kuhakikisha wanapima virusi vya Ukimwi kabla ya kufunga ndoa.

Na GodMwinyi Sadallah, Zanzibar



Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imesema ofisi ya Mufti Zanzibar imeanza kampeni kwa wanandoa watarajiwa kuhakikisha wanapima virusi vya Ukimwi kabla ya kufunga ndoa.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba na Utawala Bora, Bw. Ramadhan Abdalla Shaaban, alisema hayo alipokuwa akiwasilisha Bajeti ya Wizara huyo kwa mwaka wa fedha 2007/08, katika kikao cha Baraza la Wawakilishi mjini hapa.


Alisema mpango huo umeanza utekelezaji wake mwaka 2006/2007 kwa kuwaelimisha Masheikh wanaofungisha ndoa umuhimu wa kupima virusi vya Ukimwi kabla ya kufunga ndoa hizo.


“Ndoa zinazofanyika hivi sasa Zanzibar maharusi wengi wanapima kabla ya kuoana,“ alisema Waziri Shaaban.


Alisema Ofisi ya Mufti imeanzisha utaratibu wa kuwasomesha wanawake wa Kiislamu juu ya kutoa huduma za majumbani kwa watu walioathirika na ugonjwa wa Ukimwi, ili kuwaepusha kuathirika na maambukizo hayo.


“Kwa kuitikia wito wa mpango wa kuzuia maambukizi mapya ya ukimwi, ofisi imeweka utaratibu wa kuwafunza watu nyumba hadi nyumba kwa kutumia walimu wa vyuo vya Kurani mijini na vijijini“, alisema Waziri Abdalla Shaaban.


Alisema kwamba ofisi ya Mufti katika mwaka ujao wa fedha itaendelea na mpango wake wa kupambana na maradhi ya Ukimwi kwa kufuata taratibu za Kiislamu ili kuiepusha jamii na maradhi hayo.


Waziri Shaaban alisema ili ofisi hiyo iweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu, aliomba Baraza hilo kuidhinisha matumizi ya Sh. 98,601, 000 kwa kazi za kawaida na Sh. milioni 25 kwa kazi za maendeleo.


Katika hatua nyingine Waziri Shaaban alisema serikali imeamua kuifanyia marekebisho sheria namba saba ya makosa ya jinai ili wahalifu wa makosa madogo madogo wahukumiwe adhabu ya kutumikia jamii, badala ya kufungwa magerezani.


Alisema kwamba mpango huo unatarajiwa kuanza kufanyika katika mkoa wa Mjini Mgharibi na Kusini Pemba na baadaye utaendelea katika mikoa mingine ya Zanzibar.


Alisema kanuni zimeanza kutumika tangu sheria hiyo ilipofanyiwa marekebisho mwaka 2004.


Waziri huyo alisema katika mwaka uliopita mahakama ilipokea kesi 5,850 za makosa ya jinai na 1,276 za madai, ambapo kesi 3,271 za jinai zimetolewa uamuzi pamoja na kesi 713 za madai.


Hata hivyo, alisema kwamba majengo ya mahakama karibu yote Zanzibar yanakabiliwa na uchakavu mkubwa, ikiwemo lile la Mahakama Kuu liliopo Vuga.


Alisema serikali imeanza kuchukua hatua kwa kulifanyia matengenezo jengo hilo kuepusha maafa yanayoweza kutokea kutokana na ubovu wake.


Alisema benki ya maendeleo ya Afrika imekubali kugharamia matengenezo ya jengo hilo na imetenga Dola za Marekani 90,000.


Kuhusu mpango wa kuanzishwa Mamlaka ya kuzuia rushwa na kusimamia maadili ya viongozi Zanzibar alisema kwamba mpango huo hivi sasa umesimama, ili kutoa nafasi kwa watalaamu kuangalia uzoefu uliotumika katika kuanzisha chombo kama hicho katika nchi mbali mbali duniani.


Alisema Wizara yake iliandaa rasimu ya sheria na kuwasilisha serikalini, lakini imeshauriwa kurudi tena kutafuta uzoefu unaotumiwa na taasisi mbali mbali kama hizo duniani.


Kufuatia maelekezo hayo Wizara yangu imeona ni busara zaidi kutoharakisha uundwaji wa Mamlaka hiyo na badala yake kuendelea na uimarishaji wa Idara ya Uratibu ya Utawala Bora.


Kwa mujibu wa rasimu ya kuanzishwa Mamlaka hiyo, viongozi serikalini walipendekezwa watangaze mali zao baada ya kuteuliwa na wanapomaliza muda wao pamoja na watoto wao.


Aliomba Wizara hiyo iidhinishiwe Sh. bilioni 4.1 kwa ajili ya kazi za kawaida na Sh. milioni 383 kwa kazi za maendeleo.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents