Siasa

Kampuni iliyoiuzia Tanzania rada yabwagwa mahakamani

KAMPUNI ya British Aerospace (BAE Systems) inayoendelea kuchunguzwa kwa tuhuma kadhaa za kutumia rushwa kupata mikataba sehemu mbalimbali duniani ikiwemo sakata la ununuzi wa rada hapa nchini, imebainika kuwa sasa inatumia ‘mchezo mchafu’ kuwanyamazisha wanaoifuatilia.



Na Hassan Abbas


KAMPUNI ya British Aerospace (BAE Systems) inayoendelea kuchunguzwa kwa tuhuma kadhaa za kutumia rushwa kupata mikataba sehemu mbalimbali duniani ikiwemo sakata la ununuzi wa rada hapa nchini, imebainika kuwa sasa inatumia ‘mchezo mchafu’ kuwanyamazisha wanaoifuatilia.


Kampuni hiyo imehusishwa na matumizi ya ujasusi dhidi ya taasisi au watu wanaoonekana kufuatilia kwa karibu tuhuma za rushwa zinazoikabili.


Hali hiyo imebainika kufuatia taasisi moja ya mjini London inayojihusisha na kampeni dhidi ya Biashara ya Silaha (CAAT) Kubaini kuwa maofisa wa BAE walipata taarifa za siri za asasi hiyo iliyokuwa ikijiandaa kufungua kesi kuhoji uhalali wa Waziri Mkuu wa Uingereza, Bw. Tony Blair kusimamisha uchunguzi wa kashfa ya BAE nchini Saudi Arabia.


Mwenendo huo mpya wa BAE umevishtua hata vyombo mbalimbali vya habari nchini Uingereza vinavyoripoti zaidi kashfa za ununuzi wa silaha na rada.


BAE wamekutwa na taarifa ya barua pepe inayohusu mawasiliano kati ya CAAT na mawakili wao kuhusu mbinu za kufungua kesi kuhoji mwenendo wa Serikali ya Blair inayoonekana kuiunga mkono kampuni hiyo ya silaha.


Kutokana na hali hiyo juzi, Jumatatu, Mahakama Kuu ya Uingereza ililazimika kutoa hukumu ya kwanza na ya kihistoria kuhusiana na masuala ya rada, rushwa na siasa, kwa kuibwaga BAE, kitendo kilichopokewa kama mwanzo mwema na wanaharakati wa masuala ya rushwa.


Kwa mujibu wa mtandao wa Forbes, katika hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji King, BAE imepata pigo la kwanza katika harakati zake za kujisafisha na tuhuma za rushwa kwa kuamuriwa itoe hadharani jina la mtu aliyewapatia barua pepe inayoonesha mawasiliano binafsi katika ya CAAT na wakili wao.


” Jaji King ameipa BAE hadi Machi 12 mwaka huu ikabidhi maelezo yote na jina la mtu aliyewapatia barua pepe,” ilinaeleza Forbes kuhusu hukumu hiyo.


Jaji alieleza kuwa barua pepe ambayo BAE walikutwa nayo, ilikuwa na taarifa ambazo zinakinga ya usiri ya kisheria na ilikuwa ikihusu masuala ya malipo na mbinu za kufungua kesi ambapo CAAT ingehoji uamuzi wa Taasisi ya Kuchunguza Makosa ya Ulaghai (SFO) wa kupokea maagizo serikalini na kusimamisha uchunguzi wa rushwa katika mauzo ya silaha kwa Serikali ya Saudia.


Hukumu hiyo pia imesisitiza kuwa BAE lazima wanajua waliipataje barua pepe hiyo ya watu ambao ni wapinzani wao kiutendaji, hivyo lazima watoe maelezo ya kina kuhusu hilo.


Wakili wa CAAT, Dinah Rose, alisisitiza kuwa kuhujumiwa kwa mawasiliano hayo na kuwafikia BAE katika mazingira ya kutatanisha, kumeibua hisia kuwa sasa majasusi wameanza kutumiwa kuzifuatafuata taasisi zinazopinga vitendo vya BAE.


” Kuna ushahidi mzito kuwa BAE imekuwa ikitumia majasusi kuifuatilia CAAT na imekuwa ikitumia pauni 120,000 kwa mwaka kwa kazi hiyo,” alisema wakili huyo.


Katika hatua nyingine, imeelezwa kuwa wakati sakata la BAE na uuzaji wa silaha nchini Saudi Arabia likiendelea kuibua tafrani, SFO imekuwa ikiendelea na uchunguzi katika kashfa nyingine ikiwemo ya mawakala nchini Tanzania kulipwa kiasi cha sh. bilioni 12, kufanikisha uuzwaji wa rada ambayo hata hivyo imekuwa ikielezwa kuwa ni ya kizamani.


Rais Jakaya Kikwete tayari amekwishaweka msimamo wake bayana kuwa atalazimika kupeleka maombi rasmi kudai fedha iliyozidi iwapo itaonekana ununuzi wa rada uliofanyika mwaka 2001, uliongezewa ‘cha juu.’


Pia Taasisi ya Kuzuia Rushwa hapa nchini (TAKURU) nayo imepewa jukumu la kuchunguza kama kuna maafisa wa hapa waliopokea rushwa kuchagiza ununuzi wa rada hiyo.


Kumekuwa na hisia kwamba kutokana na urafiki wa kidiplomasia ulioimarika hivi karibuni kati ya Tanzania na Uingereza, upo uwezekano wa uchunguzi huo nao kusimamishwa kama ilivyotokea Saudi Arabia.


Bw. Blair aliwahi kubanwa kwenye Bunge la Makabwela lakini akakwepa kujibu swali la kama anaweza kuzuia uchunguzi kuhusu rada ya Tanzania au la.


Hoja kama hiyo iliibuka tena kwenye Bunge la Mamwinyi lakini nako Waziri wa sasa wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Bw. Hilary Benn alikataa kuzungumzia kwa kina akiwaambia wabunge; ” Masuala hayo yako chini ya uchunguzi wa SFO.”


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents