Habari

Kandoro aburuzwa Mahakama Kuu

Umoja wa Wamiliki wa Baa Wilaya ya Ilala (UMBI), umemburuza kortini Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, kupinga amri yake ya kupiga marufuku muziki kwenye baa nyakati za usiku.

Na Gabriela John



Umoja wa Wamiliki wa Baa Wilaya ya Ilala (UMBI), umemburuza kortini Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Kandoro, kupinga amri yake ya kupiga marufuku muziki kwenye baa nyakati za usiku.


Umoja huo umefungua kesi hiyo katika Mahakama Kuu Tanzania kuweka pingamizi la amri hiyo ya Bw. Kandoro, kwa madai mbalimbali.


Hata hivyo, kesi hiyo namba 85 ya mwaka 2007, bado inasubiri kupangiwa Jaji atakayeisikiliza na imeambatanishwa Hati ya Dharura.


Wadai katika kesi hiyo wanawakilishwa na kampuni ya Uwakili ya Bashaka Co. & Advocates ya jijini Dar es Salaam.
Katika hati ya mashtaka, walalamikaji (UMBI), wameambatanisha madai saba yanayopinga amri hiyo na kudai kuwa, imewaathiri na kwamba ni batili.


Katika dai lao la kwanza, walalamikaji wanadai kwamba, agizo hilo limewanyima haki ya kusikilizwa ili kufikia uamuzi wa haki baada ya kupata malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kama alivyodai wakati anatoa amri hiyo.


Aidha, wanadai kwamba, si kweli kwamba baa zote za Dar es Salaam, zimelalamikiwa kuhusu kupiga muziki ambao unakera wananchi na kwamba wana uhakika kuwa si baa zote zipo katikati ya maeneo wanayoishi watu.


Kadhalika, wanadai kuwa, Mkuu wa Mkoa ametoa amri hiyo bila kutoa kifungu cha sheria kinachompa madaraka hayo.


Vile vile, wanadai kuwa, amri ya Mkuu wa Mkoa haiko wazi kama muziki alioupiga marufuku ni wa kiwango gani kwani katika zama hizi za sayansi na teknolojia, kila kitu kina vipimo ikiwa ni pamoja na sauti za muziki.


Aidha, wanadai kwamba, amri hiyo imewanyima haki wanachi wanaopata burudani ya muziki kwenye baa ambazo hazikulalamikiwa na zinazoendesha shughuli zake kihalali.


`Amri hiyo pia inapingana na Ilani ya CCM na mipango ya kupiga vita umaskini kwa sababu muziki unatoa ajira kwa wanamuziki na kwamba muziki unaongeza ajira kwa wahudumu wa baa kwa sababu unaleta mkusanyiko mikubwa ya watu,` wamedai.


Pia wanadai kuwa, amri hiyo ni ya kibaguzi kwa sababu hakuna kero ya sauti kwa wananchi wa Dar es Salaam kama kero ya mihadhara ya dini hasa ile ya kukashfu dini nyingine ambayo inafanyika hadi usiku wa manane.


Souce: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents