Siasa

Kanisa lamtaka JK kuwashughulikia wala rushwa

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwashughulikia wala rushwa na mafisadi wakubwa ambao wengi wao ni vigogo.

Na Simon Mhina


Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwashughulikia wala rushwa na mafisadi wakubwa ambao wengi wao ni vigogo.


Hayo yalisemwa na Mkuu wa Kanisa hilo aliyestaafu Dk. Samson Mushemba katika hotuba yake aliyoisoma mbele ya Rais Kikwete katika misa iliyofanyika Kanisa Kuu la Azania Front, jijini Dar es Salaam jana.


Dk. Mushemba alisema ni vema Rais akatimiza ahadi yake aliyoitoa wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma.


Alisema rushwa na ufisadi hapa nchini, vimeshamiri na dalili zinaonyesha kwamba, mambo hayo yatazidi kudidimiza uchumi iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.


Alisema Kanisa linamuombea Rais Kikwete ili awe jasiri kukabiliana na wala rushwa na mafisadi kwa nguvu zaidi.


`Tunakuomba kukomesha mambo haya hata kwa wale wanaoitwa vigogo,` alisema.


Alisema rushwa na ufisadi ni mbaya kwa vile licha ya kudidimiza uchumi, pia inafanya watu wengi waporwe haki zao.


Dk. Mushemba alimuomba Rais Kikwete kuhakikisha serikali inatunga mbinu mpya na za kisasa zaidi kupambana na ufisadi.


Alisema rushwa ni kikwazo kikubwa mno katika nchi zinazoendelea, kwani wenye nacho huzidi kujilimbikizia.


Naye Mkuu mpya wa KKKT, Askofu Alex Malasusa alisema anashangaa kuona kila mtu anadai kukerwa na rushwa.


Alisema kila kiongozi awe wa kisiasa au kijamii, anadai kukerwa na rushwa, lakini akahoji, `kama kila mtu anakerwa na rushwa kama wanavyosema, mbona rushwa bado inashamiri.`


Alitaka Bunge litunge sheria mpya ya kupambana na tatizo hilo, ikiwa ni pamoja na kuongeza adhabu kwa wanaopatikana na hatia ya kujihusisha na rushwa na ufisadi.


Alishauri adhabu ya kosa hilo izidishwe mara 10.


Alisema jibu la suala hilo ni kwamba, baadhi ya wala rushwa na mafisadi ni wale wale wanaodai kukerwa na mambo hayo.


Awali, Dk. Mushemba alimtaka Rais aingilie kati suala la mfumuko wa bei nchini.


Alisema hivi sasa kila kitu kipo bei juu, hali inayowapa wakati mgumu wananchi wa kipato cha chini.


`Tunakuomba Rais uingilie kati tatizo hili, jamii inateseka, kwa vile kila bidhaa imepanda bei, hata nauli zimepanda sana,` alisema.


Hata hivyo, kiongozi huyo alisema wafanyabiashara wengine hupandisha bei za bidhaa zao kutokana na tamaa ya kujipatia fedha tu.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents