Siasa

Karamagi agoma kujiuzulu

HOMA ya hoja ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa ya kuwatuhumu viongozi 11 wa serikali na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa vitendo vya ufisadi, inaendelea kuchukua sura mpya kila kukicha.

na Irene Mark


HOMA ya hoja ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa ya kuwatuhumu viongozi 11 wa serikali na wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa vitendo vya ufisadi, inaendelea kuchukua sura mpya kila kukicha.


Jana, mtuhumiwa wa tatu, Waziri wa Madini na Nishati, Nazir Karamagi, aliibuka na kutangaza azima yake ya kuchukua hatua za kisheria kufanya kile alichokiita kutafuta haki na kusafisha jina lake dhidi ya tuhuma hizo alizozikanusha.


Karamagi alitangaza uamuzi wake huo wa kumshitaki Dk. Slaa, gazeti la MwanaHalisi na Kampuni ya uchapishaji ya Printech, huku akiweka kiporo masuala mengine hadi Jumamosi wiki hii, mbele ya waandishi wa habari, ofisini kwake jijini Dar es Salaam.


Uamuzi wa Karamagi kuitisha mkutano huo wa waandishi wa habari umekuja wakati kukiwa na taarifa kwamba, Rais Jakaya Kikwete ambaye yuko nje ya nchi kikazi, amewaagiza viongozi wote wa serikali na CCM waliotajwa katika tuhuma hizo kujitokeza na kujibu tuhuma zao zote, kila mmoja kwa wakati na kwa namna yake.


Aidha, uamuzi huo wa Karamagi unakuja wakati kukiwa na taarifa nyingine zinazoeleza kuwa, waziri huyo alikuwa akitarajiwa kutoa tamko zito kuhusu hatima yake Jumamosi wiki hii.


Hata hivyo Karamagi hakuwa tayari kuweka bayana iwapo katika mkutano wake wa Jumamosi hii, atafikia uamuzi wa ama kujiuzulu uwaziri, au kukanusha taarifa mpya zinazohusisha kuvuja kwa mkataba wa uchimbaji wa madini wa Buzwagi, ambao aliusaini Februari mwaka huu katika mazingira yanayoliacha taifa likiwa katika mvutano mkubwa kimtazamo.


“Naenda mahakamani kwa kuwa mimi siyo mbadhirifu… Nimeteuliwa na rais. Hivi rais anaweza kumteua waziri mbadhirifu? Unayesema nijiuzulu, kwani ni nani anayemteua waziri?” alisema Karamagi nje ya chumba cha mikutano wakati akijibu swali la mwandishi mmoja wa habari aliyetaka kujua iwapo alikuwa akifikiria kujiuzulu baada ya sakata hilo.


Kujitokeza kwa Karamagi kujibu tuhuma hizo, mbele ya wanahabari na kuweka bayana msimamo wake, kunamfanya awe mtuhumiwa wa pili kufanya hivyo baada ya hivi karibuni Mbunge wa Musoma Vijijini na wakili maarufu nchini, Nimrod Mkono, naye kukana kufuja fedha za BoT kupitia kampuni yake ya uwakili ya Mkono Company and Advocates.


Nje ya utaratibu huo wa kuzungumza na wanahabari, mtu mwingine pekee aliyekanusha tuhuma dhidi yake ni Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, aliyekaririwa na gazeti moja akikiri kuwa na hisa katika Kampuni ya Tangold inayohusishwa na tuhuma za upatikanaji na fedha isivyo halali kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na akakana kufanya jambo lolote lenye harufu ya ufisadi.


Akizungumza jana, Karamagi alisema ameamua kwenda mahakamani kusafisha jina lake lililochafuliwa na Dk. Slaa katika mkutano wa hadhara, Mwembe Yanga, akiamini kuwa yeye ni mtu safi.


“Kwa sababu ninayo heshima ya kulinda jina na kulisafisha, na nina amini kuwa mimi ni muadilifu, nimeamua kwenda mahakamani ili kutafuta haki yangu dhidi ya wote walioshiriki na wanaoendelea kushiriki katika vitendo vya kunipaka matope na kunihukumu kwa ufisadi.


“Nimewaagiza mawakili wangu kufungua kesi mahakamani mara moja dhidi ya Dk Slaa, gazeti la MwanaHalisi na Kiwanda cha Printech kinachochapisha gazeti la MwanaHalisi,” alisema Karamagi.


Alisema tuhuma zilizotolewa na Dk. Slaa zililenga kuchafua jina lake na kuonyesha kwamba yeye (Karamagi) ni fisadi na mtu asiyestahili kukabidhiwa madaraka yoyote katika jamii.


Waziri Karamagi alisema Dk. Slaa na wenzake (ambao hakuwataja kwa majina) wamezitangaza kwamba si tuhuma bali ni ukweli, hivyo hawakuona sababu ya kufuata mkondo wa sheria.


Katika hilo, Waziri Karamagi alisema amechukua hatua hiyo bila kujali wadhifa wake kwa taifa akiwa na ushahidi wa kutosha wa kuwafikisha mahakamani wote wanaomtuhumu kwa ufisadi.


“Nitawashitaki kama Nazir Karamagi na siyo Waziri wa Nishati na Madini… ninao ushahidi wa tape (kanda) ya video na nakala ya gazeti la MwanaHalisi,” alisema waziri huyo.


Mara tu baada ya kusoma tamko lake hilo, Waziri Karamagi alisimama na kuanza kuondoka kutoka ndani ya chumba cha mikutano, kabla ya kujibu maswali yaliyoanza kuelekezwa kwake na waandishi wa habari.


Hatua hiyo ilipingwa na waandishi wa habari waliotaka arejee kujibu maswali yao, wakisema walikuwa hawajaridhishwa na maelezo yake, na akakubali kurejea akitaka aulizwe maswali matatu tu, huku akiahidi kuzungumza kwa ufasaha Jumamosi wiki hii wakati atakapozungumzia kuhusu mkataba wa madini wa Buzwagi.


“Sihitaji maswali jamani, mnatakiwa mfahamu kwamba nitafungua kesi, basi, hayo maswali nitayajibu Jumamosi… mpo wengi sana, nitaruhusu maswali matatu tu.


“…Mnielewe… hapa sitazungumza issue (suala la) ya Buzwagi, mkiyataka hayo tutakutana Jumamosi, na yule aliyeniuliza kama nilikwenda London kusaini mkataba si kweli,” alisema mara baada ya kurejea katika kiti chake.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents