Habari

Karume akoswakoswa kugongwa na daladala

GARI alilokuwa amepanda Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume mwishoni mwa wiki lilinusurika kugongwa na basi la abiria, maarufu kwa jina la daladala katika eneo la Kilimani, visiwani hapa.

na Mwandishi Wa Tanzania Daima

 

GARI alilokuwa amepanda Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume mwishoni mwa wiki lilinusurika kugongwa na basi la abiria, maarufu kwa jina la daladala katika eneo la Kilimani, visiwani hapa.

 
Tukio hilo la aina yake, lilitokea wakati Karume aliyekuwa katika msafara wake, alipokuwa akitokea nyumbani kwake Mbweni akielekea ofisini Ikulu.

 
Watu walioshuhudia tukio hilo, waliieleza Tanzania Daima kwamba, magari yaliyokuwa katika msafara huo, likiwamo gari la Karume, yalilazimika kulikwepa daladala hilo lililoingia ghafla barabarani.

 
Gari hilo la daladala lenye namba za usajili ZNZ 46224 aina ya Ford, lililokuwa limebeba abiria, lilikuwa likitokea Chukwani, na kuelekea kituo kikuu cha Darajani.

 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Bakar Khatib Shaaban, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, lakini akasema msafara huo uliendelea na safari ukiwa salama.

 
Alisema tukio hilo lilisababishwa na uzembe wa askari wa usalama barabarani katika eneo hilo na hatua za kinidhamu zimechukuliwa dhidi yake.

 
Hata hivyo, Kamanda Shaaban hakufafanua ni hatua gani za kinidhamu zilizochukuliwa kwa askari huyo. Alisisitiza hayo ni mambo ya ndani ya Jeshi la Polisi.
“Ni kweli dereva wa gari la abiria ameachiwa kwa vile kwa upande wake hakuwa na kosa, hasa kwa kuzingatia msafara ulitokea nyuma ya gari yake,” alisema Kamanda Shaaban.

 
Tukio hilo lilitokea katika eneo la Kilimani kwenye makutano ya barabara itokayo Uwanja wa Ndege, Maisara na ile inayoelekea katika eneo la Kariakoo.

 
Watu walioshuhudia tukio hilo, walisema msafara huo ulilazimika kugawanyika mara mbili baada ya magari mengine kupita upande wa kulia na mengine kushoto likiwemo la rais, huku gari la daladala likiwa katikati ya barabara.

 
Walisema gari ya polisi tayari ilikuwa imepoteza mwelekeo na bila ya umakini wa watu wa usalama, ajali mbaya ingeweza kutokea kwa vile rais alikuwa nyuma ya magari ya usalama wa taifa, ambayo yalilazimika kukwepa na kupita kushoto.

 
“Kama wangefuata gari ya polisi iliyokuwa ikiwaongoza na king’ora, ingeweza kutokea ajali mbaya kwa vile gari yetu sisi abiria tulikuwa katikati ya barabara,” alisema mmoja wa abiria aliyekuwa katika daladala hilo.

 
Abiria huyo alisema askari aliyekuwa amepangiwa kazi katika eneo hilo hakuonekana kushughulika kuyaweka pembeni magari mapema na kujikuta daladala hilo likiwa katikati ya barabara likijiandaa kupinda kuekelea eneo la Magereza wakati msafara huo unakatiza eneo hilo.

 
Baada ya kosakosa hiyo, daladala hilo lilikamatwa katika kituo cha Michenzani na abiria wote waliokuwemo kutakiwa kushuka na gari hilo kupelekwa makao makuu ya kikosi cha Usalama Barabarani kilichopo Malindi.

 
Hata hivyo, baada ya dereva wa gari hilo kuhojiwa na kueleza ramani ya tukio, aliachiwa kwa vile alionekana hana makosa.

 
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Hassan Nasir, alisema yeye hawezi kuzungumzia lolote kuhusu tukio hilo kwa vile msemaji ni Kamanda wa Polisi Mkoa.
“Nilipokea taarifa za askari wangu kuwekwa ndani, lakini msemaji wa tukio hilo ni Kamanda wa Polisi, kwa mujibu wa utaratibu wetu,” alisema.

 
Hivi karibuni, msafara wa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ulikumbwa na ajali wakati ukitokea mkoani Kilimanjaro kuelekea Arusha, baada ya dereva wa basi la abiria kugongana na gari dogo la polisi lililokuwa likiongoza msafara huo.

 
Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents