Habari

Kashfa nzito HakiElimu

KASHFA imeibuka ndani ya shirika la HakiElimu ambapo wafanyakazi wametoa madai dhidi ya uongozi kwamba umekithiri kwa manyayaso na kushindwa kujali maslahi yao.

Na Mwandishi Wa Uhuru


KASHFA imeibuka ndani ya shirika la HakiElimu ambapo wafanyakazi wametoa madai dhidi ya uongozi kwamba umekithiri kwa manyayaso na kushindwa kujali maslahi yao.
Malalamiko ya wafanyakazi hao, yamo kwenye ripoti ya kamati maalumu ya maboresho ya mikutano ya wafanyakazi wa HakiElimu ambayo Uhuru inayo nakala na nyaraka nyingine zinazomtuhumu mmoja wa ‘vigogo’ ndani ya shirika hilo.
Shirika hilo lenye wafanyakazi 36, lilianzishwa mwaka 2001 na tangu kipindi hicho limekuwa likifanya kazi ya kuikosoa serikali bila kutoa majibu mbadala kwa serikali. Mwaka jana serikali ililifungia shirika hilo, lakini baadaye ililifungulia.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wafanyakazi 33 kati ya 36 ndiyo walikubali kuhojiwa na kamati hiyo, wengine walikataa kutokana na sababu wanazofahamu wenyewe.
Kamati hiyo yenye wajumbe watano (majina yanahifadhiwa) iliibua mambo kadhaa ambayo yanalalamikiwa na wafanyakazi dhidi ya menejimenti ya shirika hilo.
Miongoni mwa mambo ambayo wafanyakazi wanayalalamikia ni kutoaminiwa, kutopewa heshima kwa utaalamu binafsi wa mtu, kutojali hisia za watu na pia kukaripiwa bila sababu na kiongozi mmoja mwandamizi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wafanyakazi wanalalamika kwamba mmoja wa viongozi amekuwa hana uzalendo, mbinafsi na hapendi kupingwa wala kuulizwa maswali huku madai mengine yakisema ni mbaguzi wa rangi.
“…Hakuna mtu aliye na uwezo wa kufanya uamuzi katika jambo lolote bila kumhusisha mmoja wa vigog hao (jina linahifadhiwa). Kweli huo ndiyo utaratibu, lakini yeye kazidi. Hata vitu vidogo vidogo tumsubiri yeye, ilisema moja ya nyaraka ikiwakariri wafanyakazi.
Ni mbinafsi wa mali na fikra. Wafanyakazi waliokwisha thuhubutu kumuuliza maswali au kumpinga, aliwanyanyasa na kuwajengea mazingira magumu ya kazi.
“Baadhi yao aliwafukuza ‘kijanja’ na wengine hawakusubiri aibu hiyo, waliacha wenyewe. Nyakati nyingine hutumia uongo wowote ule ilimradi kunusuru nafsi yake,” ilidai nyaraka hiyo.
Katika shirika hilo la HakiElimu, ambalo ni maarufu kwa kutetea haki za binadamu, demokrasia na elimu, kuna madai kuwa mmoja wa vigogo amekuwa hafanyi hivyo kwa vitendo mahali pa kazi na badala yake, amewahi kumpiga kibao sekretari wake kwa madai ya kutofanya kazi kama alivyoelekezwa.
“Hachelewi kuwatukana wafanyakazi na kuwagongea meza kwa kudhihirisha hasira yake hata kwa makosa madogo ya kibinadamu. Pia alikwishamtia kabari mama mmoja, eti tu alichelewa kumpelekea kazi,” ilidai moja ya nyaraka.
Madai mengine ni kwamba mikutano ya wafanyakazi imekuwa haithaminiwi na uongozi hata uanzishwaji wa chama cha wafanyakazi umekuwa mgumu.
“Kwa kuwa shirika na wafanyakazi waliridhia kuanzishwa kwa kamati maalum ya maboresho, wajumbe wa kamati hii wanaamini kuwa shirika lina nia ya kuboresha mikutano ya wafanyakazi ili iweze kuwa na manufaa kwa shirika na wafanyakazi wake,” iliendelea kudai.
Kwa mujibu wa ripoti, ilidaiwa kuwa matarajio ya wajumbe ni kuona shirika linaafiki na kuyatumia baadhi ya mapendekezo (si yote) na pia wafanyakazi wajibidiishe kuelewa sera za kiutawala za shirika na waelewe mipaka na uwezo wa mikutano hiyo.
Kamati ya maboresho ilitoa maoni yake kwamba haitakuwa vizuri kwa wafanyakazi na uongozi wa shirika kudumu katika mivutano kwa muda mrefu, ambapo wafanyakazi wanaona shirika halijali maslahi yao.
Pia imelitaka shirika kuwasilikiza wafanyakazi ili nao wajisikie kuwa shirika linawajali na kutoa tuzo ya mfanyakazi bora ili kuleta ushindani na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali.


Source: Uhuru

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents