Habari

Kasusura aenda jela miaka 35

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemhukumu, Bw. Justine Kasusura, kifungo cha jumla ya miaka 35 jela na viboko 12 baada ya kupatikana na hatia katika makosa ya wizi wa mabilioni ya fedha kwa kutumia silaha.

Na Grace Michael

 

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemhukumu, Bw. Justine Kasusura, kifungo cha jumla ya miaka 35 jela na viboko 12 baada ya kupatikana na hatia katika makosa ya wizi wa mabilioni ya fedha kwa kutumia silaha.

 

Mbali na kifungo hicho, pia mahakama iliwaachia huru washitakiwa wanne waliokuwa wanashitakiwa pamoja naye ambao ni Bw. Leonard Urasa, Bw. Wicklif Urasa, Bi. Ruth Urasa na Bw. Libenti Lukundwa.

 

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkuu Mfawidhi, Bw. Sivangilwa Mwangesi, ambaye kabla ya hukumu alipitia maelezo yote ya mashahidi ili kuonesha jinsi ushahidi ulivyomwelemea zaidi Bw. Kasusura.

 

Bw. Mwangesi alianza kusoma hukumu hiyo saa 5.05 adhuhuri mpaka saa 6.05 mchana ambapo alisema hakuna ubishi wowote kuwa Bw. Kasusura siku ya tukio alitumwa kwenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam (leo Mwalimu JK Nyerere) kuchukua mzigo ambao ulikuwa na uzito wa kilo 20.

 

Kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo, mzigo huo ulikuwa na fedha ambazo hazikujulikana idadi na Kasusura alitajwa kuuchukua na kuuweka ndani ya gari la kampuni ya Night Support lakini hakuupeleka sehemu husika.

 

Ushahidi uliombana zaidi Bw. Kasusura ni wa shahidi namba moja wa upande wa mashitaka, ambaye alisema walipofika makutano ya barabara ya Uwanja wa Ndege na Nyerere, mshitakiwa alimwambia shahidi huyo waliyekuwa naye kwenye gari kuwa: “Uhusiano wangu na wako unaishia hapa,” na kisha akamtishia kwa bastola na kufanikiwa kuuhamisha mzigo huo na kuuweka kwenye gari nyingine na kutoweka nao.

 

Katika utetezi wake, Bw. Kasusura alidai kuwa baada ya kuchukua mzigo huo aliondoka na gari na alipofika nje alikutana na mkuu wake ambaye alimtaka kukabidhi ufunguo wa gari kwa mtu mwingine na yeye kupewa gari nyingine, ambapo alipangiwa kazi ya kufanya tofauti na ya kurudisha mzigo waliokuwa wameuchukua Uwanja wa Ndege.

 

Baada ya Mahakama kuangalia maelezo ya pande zote mbili, iliona kuwa maelezo ya mshitakiwa hayakuwa na mvuto na yalishindwa kutengua ushahidi mzito wa upande wa mashitaka, hivyo mahakama haikuwa na shaka kuwa yeye ndiye aliondoka na mzigo huo.

 

Kasusura pia katika utetezi wake, alikana kuwa na silaha siku ya tukio na kujitetea kuwa akiwa dereva wa gari, asingeweza kumtishia shahidi namba moja wa upande wa mashitaka.

 

Hata hivyo Hakimu Mwangesi aliyaona maelezo hayo kukosa uzito kwa sababu ushahidi uliotolewa mahakamani hapo ukijumuisha wa kiapo chake mwenyewe, mshitakiwa alipohojiwa na Polisi na ule uliotolewa na upande wa mashitaka, ulithibitisha bila kuacha shaka, kuwa mshitakiwa kabla ya kwenda uwanja wa ndege, alikabidhiwa bastola wakiwa ofisini kwake.

 

Kutoka na ushahidi huo, Hakimu Mwangesi alisema ni dhahiri, kuwa mshitakiwa siku ya tukio alikuwa na silaha na aliitumia kutishia kabla ya kuondoka na mfuko uliokuwa na fedha, hivyo akamkuta na hatia ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

 

Wakati Bw. Kasusura akibanwa na kutiwa hatiani kwa ushahidi huo, wenzake wanne waliachiwa huru kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka yaliyokuwa yakiwakabili, yakiwamo ya kula njama na kupokea mali ya wizi.

 

Kabla ya kutolewa hukumu, upande wa mashitaka uliokuwa unaongozwa na wakili wa Serikali, Bw. Angaza Mwaipopo, ulisema pamoja na mshitakiwa kutenda kosa hilo kwa mara ya kwanza, lakini aliiomba mahakama izingatie uzito wa makosa hayo, kutokana na kuwa ni ya hatari kwa jamii na kutaka adhabu kali itolewe.

 

Naye wakili wa mshitakiwa, Bw. Majura Magafu, hakuwa na la kusema zaidi ya kuiachia mahakama ifanye kazi yake, kulingana na adhabu iliyotajwa kwenye sheria.

 

Akitoa adhabu, Bw. Mwangesi alisema: ” Baada ya kuwa na hatia katika makosa ya wizi na unyang’anyi wa kutumia silaha na kama alivyosema wakili Magafu, ni kweli mikono yangu imefungwa na sheria, hivyo katika kosa la wizi mshitakiwa atatumikia kifungo cha miaka mitano na katika lile la unyang’anyi wa kutumia silaha, atatumikia kifungo cha miaka 30 jela na viboko 12.”

 

Wakili wa Kasusura, Bw. Magafu aliwaambia waandishi wa habari kuwa hajaridhika na hukumu hiyo na atakata rufaa. Alisikika akilalamika kuwa upande wa Serikali uliichelewesha mno kesi hiyo.

 

“Sina mengi ya kuzungumza kwa sasa. Nitaeleza malalamiko yangu katika rufaa nitakayoikata,” alisema.

 

Akiondoka mahakamani hapo, Bw. Kasusura aliibua kituko baada ya kumshukuru hakimu kwa kumpa adhabu hiyo: “Ahsante sana Mheshimiwa,” alisikika akisema wakati hakimu akitoka huku mshitakiwa huyo akishindwa kuzuia kijasho chembamba kilichokuwa kikionekana dhahiri kumtoka.

 

Bw. Kasusura aliibua vituko zaidi wakati akiwa amepandishwa kwenye gari la Polisi aina ya Land Rover Defender namba PT 0881 tayari kwenda gerezani, aliposikika akiwaaga waandishi wa habari akisema:

 

“Waandishi kwaherini kesi ndiyo hiyo imekwisha na mimi nimeonewa, naambiwa nilikuwa na silaha, kwani mimi mlinzi? Na wakati miye nilikuwa dereva tu…Basi, Bwana Mungu ndiye kapanga.”

 

Awali washitakiwa walifikishwa mahakamani wakidaiwa kuwa Agosti 2, 2001 wakiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam, waliiba dola za Marekani milioni mbili, mali ya Citibank kwa kutumia silaha.

 

Bw. Kasusura mbali na kufungwa kifungo hicho, hukumu hiyo ilitolewa ikiwa ameshakaa gerezani zaidi ya muda wa miaka sita tangu alivyokamatwa.

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents