Habari

Katakata umeme Tanesco yaja tena

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) ambalo kwa kipindi kirefu limekuwa katika hali mbaya ya fedha, limetangaza kuanza kata kata ya umeme kwa wadaiwa wake wote ambao wanadaiwa Sh bilioni 217.

Shadrack Sagati

 

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) ambalo kwa kipindi kirefu limekuwa katika hali mbaya ya fedha, limetangaza kuanza kata kata ya umeme kwa wadaiwa wake wote ambao wanadaiwa Sh bilioni 217. Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 100 ni deni halisi wakati Sh bilioni 117 ni riba wanayodaiwa wateja ambao wamekuwa wanalimbikiza madeni yao.

 

Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dk Idris Rashid jana alitangaza kampeni maalumu ya kukusanya Sh bilioni 100 itakayofanywa kwa miezi sita kuanzia mwezi ujao hadi Oktoba mwaka huu.

 

Alisema shirika lake linahitaji fedha nyingi kwa ajili ya kukarabati na kuboresha mifumo ya usambazaji umeme, hasa kwenye miji mikubwa ambayo ina matatizo ya kukatika umeme. Dk Rashid alisema kampeni maalumu ya ukusanyaji madeni ni mkakati wa shirika hilo wa kukusanya fedha zake yenyewe zitumike kwenye matengenezo na ukarabati. Pamoja na ukusanyaji huo wa madeni, shirika hilo limeomba Serikali iweze kusaidia katika juhudi hizo.

 

Kutokana na kuwa katika hali mbaya ya fedha, Tanesco imeanza kukopa katika benki za ndani, na kwa wafadhili kama Benki ya Dunia na mashirika mengine ya kimataifa, liweze kuboresha mfumo wa usambazaji wa umeme ambao kwa sasa una matatizo makubwa ya kukatika mara kwa mara.

 

“Tumelazimika kuwaendea wafadhili wa nje kutusaidia, Serikali na tumekopa katika benki za ndani,” alisema Dk Rashid ambaye alitumia muda huo kukiri kuwa kukatika kwa umeme mara kwa mara kunatokana pia na uchakavu wa mfumo wa umeme.

 

Kuhusu kampeni ya ukusanyaji madeni, Dk Rashid alisema wateja ambao watalipa madeni yao ndani ya wakati huo watasamehewa kulipa riba ya asilimia 2 ambayo anatozwa mteja anayelimbikiza deni kila mwezi. Katika kipindi hicho cha kampeni ya ukusanyaji wa madeni, shirika hilo pia limewataka wale ambao wamejiunganishia umeme wenyewe bila kufuata utaratibu uliowekwa, wajisalimishe katika ofisi za Tanesco wawekwe kwenye utaratibu.

 

Alisema mwishoni mwa kampeni kutakuwa na ukaguzi wa nyumba hadi nyumba wenye madhumuni ya kuwanasa wateja ambao walikatiwa umeme kwenye kampeni, lakini wakaamua kujiunganishia wenyewe. Mkurugenzi huyo alisema sababu nyingine ni vituo vingi kujaa mzigo wa matumizi ya wateja.

 

Tatizo jingine ni lile la hujuma kwenye miundombinu ya umeme hasa wizi wa mafuta ya transfoma, nyaya za umeme pamoja na wizi wa vyuma kwenye laini kubwa.

 

Source: Daily News

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents