Habari

Kauli ya Makamu wa Rais siku ya walemavu duniani

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameitaka jamii kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu hawaachwi nyuma kwenye nyanja zote za maendeleo.

Makamu wa Rais ameyasema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Watu wenye ulemavu duniani iliyofanyika mkoa wa Kusini, Unguja, Zanzibar.

Akihutubia mamia ya watu wenye ulemavu na wasio na ulemavu kwenye kwenye viwanja vya Skuli ya Uzini, Makamu wa Rais alisema tumejumuika leo hapa kuungana na wenzetu duniani kote kuadhimisha kilele cha siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemavu Duniani ambayo imebeba kauli mbiu isemayo “Mabadiliko kuelekea jamii Jumuishi na Maendeleo Endelevu kwa wote”­­­­­­ ujumbe huu unalenga kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu wanajumuishwa katika mipango yote ya maendeleo ili kuweza kufikia malengo endelevu ya dunia ifikapo mwaka 2030 pia inakwenda sambamba na Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2020; Ilani ya Chama Tawala na mpango wa kukuza Uchumi na kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA III) ambapo masuala ya watu wenye ulemavu yamezingatiwa.”

Tanzania iliridhia mkataba wa kimataifa wa haki za watu wenye ulemavu ambao umeweka misingi madhubuti wa utekelezaji wa masuala mbali mbali kwa ajili ya watu wenye ulemavu, ikiwemo; Usawa, Ushirikishwaji kikamilifu katika mipango ya hifadhi ya jamii na kupunguza umasikini na kuwapatia huduma pamoja na kufanya kazi na taasisi zinazoshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu,” alisema Makamu wa Rais.

Makamu wa Rais alitoa rai kwa kusema “kuanzia leo(jana) kila mmoja miongoni mwetu awe askari wa mwenzie katika kuhakikisha kuwa tunalinda haki na usawa wa watu wenye ulemavu”.

Makamu wa Rais aliwaasa wanafamilia kutoficha maovu wanayofanyiwa watu wenye ulemavu, alisema Serikali kwa nguvu zote inakemea vitendo vya ubakaji na udhalilishaji kwa watu wenye ulemavu kwani si vitendo vya kiungwana hata kidogo na kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwashughulikia kikamilifu wahalifu hawa na wakithibitika wafikishwe kwenye vyombo vya sheria ikiwemo mahakama na kutoa adhabu kali dhidi ya wale watakaobainika.

Makamu wa Rais alisema Serikali kwa kushirikiana na Wadau wengine wa Maendeleo pamoja na wananchi itaendelea kuhakikisha kuwa ‘digital technology’ inakuwa rafiki kwa walemavu hususan katika kuwawezesha kupata elimu, vitendea kazi katika maendeo yao pamoja na kuhakikisha wanafikia kirahisi huduma zote za kijamii.

Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ilisema itaendelea kuweka mipango thabiti na mathubuti yenye kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki za kisiasa, kiuchumi, kijamii na fursa sawa kama wengine na kuahikisha watu wenye ulemavu wanashiriki kikamilifu katika ngazi mbali mbaliza uongozi za kitaifa.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents