Kawawa ashangaa viongozi kumiliki mabilioni ya fedha

Rashid KawawaWAZIRI Mkuu Mstaafu, Rashidi Mfaume Kawawa, ameitaka serikali kuwasaka viongozi wanaojihusisha na vitendo vya ufisadi nchini na kuwabana waeleze fedha wanazozimiliki namna walivyozipata

Rashid Kawawa


 


Na Muhibu Said


WAZIRI Mkuu Mstaafu, Rashidi Mfaume Kawawa, ameitaka serikali kuwasaka viongozi wanaojihusisha na vitendo vya ufisadi nchini na kuwabana waeleze fedha wanazozimiliki namna walivyozipata.

Kawawa ambaye ni mmoja wa waasisi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kiongozi anayeheshimika kutokana na kushika nyadhifa mbalimbali za kitaifa, alitoa kauli hiyo katika mahojiano maalum na waandishi wa habari, muda mfupi baada ya kuzindua kitabu kiitwacho: ‘CCM na Mustakbali wa Nchi Yetu’, katika hoteli ya Courtyard, jijini Dar es Salaam jana.

Alisema yeye pamoja na watu wengine waadilifu, hawapendi tabia ya kujilimbikizia mali isivyo halali inayoendekezwa na baadhi ya viongozi nchini, ambayo haikuwahi kufanywa na waasisi wa taifa hili, wakiongozwa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

“Hatupendi ulimbikizaji mali wa haramu, hivyo wote wanaojilimbikizia mali kwa njia hiyo, wafuatiliwe, waulizwe, waseme walizipataje,” alisema Kawawa ambaye alipata pia kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema Mwalimu Nyerere ambaye ni kielelezo cha uadilifu na uaminifu kati ya viongozi wachache duniani, hakuwahi hata siku moja kujipatia mali kwa njia zisizo za halali.





 Kawawa enzi zake
  Rashid Kawawa enzi zake za ujana
“JKT (Jeshi la Kujenga Taifa) walimjengea nyumba, alikubali kwa sababu alihitaji nyumba. Sijui kama alikuwa na uwezo au alikuwa hana wa kujenga hiyo nyumba, ila hakuwahi kujipatia mali kwa njia za haramu,” alisema Kawawa ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Mstaafu.

Alisema mbali na Mwalimu Nyerere, hata yeye (Kawawa) hadi anastaafu kazi serikalini na katika chama, hajawahi kujipatia mali kwa njia za haramu.

“Ningeyapata wapi hayo mabilioni ya shilingi?,” alihoji Kawawa ambaye ni Katibu Mkuu wa kwanza wa CCM.

Kuhusu Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge ya kuyaita mabilioni ya shilingi anayotuhumiwa kuyahifadhi katika akaunti ndani na nje ya nchi kuwa ni “vijisenti”, Kawawa alisema: “Hayo ni maoni ya mtu, kila mtu ana maoni yake”.

Alipoulizwa, ni hatari gani inayoweza kukikumba chama baadaye kutokana na ufisadi, alisema kwa ufupi: “si jambo zuri”.

Kauli hiyo ya Kawawa inatokana na kuibuliwa tuhuma za ufisadi na ulimbikizaji wa mabilioni ya shilingi kwa njia za haramu, kunakodaiwa kufanywa na baadhi ya vigogo, wakiwamo viongozi wa serikali na kulisababishia taifa hasara kubwa.

Zaidi ya Sh133 bilioni zilithibitishwa na serikali kupotea katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika mazingira yanayosadikiwa kuwa ni ya kifisadi.

Mbali na hilo, Waziri Chenge, ambaye juzi alikiri kuchunguzwa na vyombo mbalimbali vya kitaifa na kimataifa, anatuhumiwa kumiliki dola 1 milioni (Sh1.2 bilioni) katika akaunti iliyoko katika kisiwa cha Jersey, nchini Uingereza katika mazingira ya kutantanisha, yanayohusishwa rushwa ya ununuzi wa rada ya kijeshi miaka iliyopita.

Awali, akitoa nasaha katika uzinduzi wa kitabu hicho, Makwaia wa Kuhenga, Mhadhiri Mwandamizi Mstaafu wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Issa Shivji alionyesha kushangazwa kwake na mabadiliko ya uongozi nchini, kutoka kwenye utumishi wa umma kuwa mradi kwa baadhi ya watu.

“Kila siku hivi sasa, kwenye magazeti utasikia ufisadi. Lazima tuhoji, kwa nini uongozi umekuwa mradi badala ya utumishi wa umma?,” alihoji Profesa Shivji.

Kawawa ambaye amewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), pia alitoa ushauri kwa wana CCM kudumisha utamaduni wa kujikosoa na kukosoana ili kuleta mabadiliko katika chama na taifa kwa jumla.

Kawawa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa kwanza wa chama hicho, alisema tangu enzi za TANU na ASP hadi sasa, CCM imekuwa na utamaduni wa kuwa na mijadala katika mambo mazito yanayohusu chama na taifa na kwamba, hakiogopi kukosolewa kwa kuwa Mwongozo wa chama hicho wa mwaka 1981 umetamka bayana kwamba kujikosoa na kukosoana ni silaha ya mapinduzi.


 


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents