Habari

Kenya: Mwanamke asimulia alivyonusurika kuuawa na mume wake

Tahadhari…maelezo katika huenda ikawa na athari kwa baadhi ya wasomaji

Bi Diana Wanjiku Kamande kutoka nchini Kenya ni mama ya watoto wawili ,Anapokumbuka yaliyomkuta tarehe 13 mwezi Aprili 2013, hupatwa na hisia majonzi pamoja na furaha.

Kwa mujibu wa BBC. Hii ni kutokana na tukio la siku hiyo ambapo alinusurika na mauaji ya mtu aliyempenda…mumewe.

Alikutana vipi na mumewe?

“Jina langu ninaitwa Diana Wanjiku …nilikutana na mume wangu kwa jina, Richard Machio, mwaka wa 2003. Nilikuwa nasubiri basi la abiria (matatu) ili linipeleke katika shule niliyokuwa ninasomea. Alikuwa ni mwanaume mrefu wa miraba minne”, anasema Diana.

“Habari, jina langu ni Richard,” alisema .”Mimi ni dereva wa matatu kisha akasita mara mmoja kana kwamba alikuwa hawezi kuzungumza tena “alijitambulisha

Diana anasema kuwa moyo wake ulianza kumdunda dunda, na mara moja aligundua kuwa alikuwa amenaswa kwenye lindi la mapnezi na mtu yule.

Tangu siku hiyo uhusiano wao wa kimapenzi uliiimarika kwa kasi sana, na tangu walipokutana mwezi huo, wakaendelea kukutana walau kila siku, kwa kuwa mpenzi wake alikuwa dereva wa matatu ukipenda daladala alikuwa anambeba kila siku akielekea masomoni.

Baada ya kuchumbiana kwa miezi mitano siku mmoja aliamuwa kumtembelea mpenzi wake nyumbani na kwanzia ile siku hakurejea tena kwao akaanza maisha ya unyumba na hapo ndipo ndoa yake ilipoanzia.

“Nilikuwa msichana mdogo mwenye umri wa miaka 24 tulipoanza maisha ya kuishi pamoja sikufahamu mengi kuhusu ndoa” Diana alieleza.

Diana Kamande na mumewe walianza maisha yao kwa kuishi kwenye nyumba ya chumba kimoja , na wakati huo tayari alikuwa na ujauzito wa miezi 5 wa binti yake Praise ambaye sasa ana umri wa miaka 10.

Mwaka wa 2004 Disemba ,Mume wake Richard alikwenda nyumbani kwa wazazi wa Bi Diana kukutana na wazazi wake na hapo hapo walipokea baraka za wazazi za kuishi kama mume na mke hali kadhalika walisafiri hadi nyumbani kwa mume wake magharibi mwa Kenya na kukutana na mama yake mzazi aliyewapa baraka pia.

Diana anakiri ya kuwa japo hawakuwa na fedha nyingi walijizatiti sana kwa kufanya kazi kwa bidii iliyowawezesha kununua kipande cha ardhi mjini Nairobi na walikuwa na mipango ya kijenga nyuma yao.

Wakati huo walikuwa hawana siri na mume wake alikuwa anafunguka kuhusu shida zote za kikazi na za binafsi.

Miaka kadhaa baada ya kufunga ndoa mume wake aliamua kustaafu katika kazi ya kuwa dereva wa matatu , na akaajiriwa kazi kama dereva wa kampuni moja mjini Nairobi.

Diana anasema kipindi chote cha ndoa yake mume wake Richard hakuwahi kumpiga wala kunitusi, kabla ya kumuuaDiana anasema kipindi chote cha ndoa yake mume wake Richard hakuwahi kumpiga wala kunitusi, kabla ya kumuua

“Kipindi chote cha ndoa yetu mume wangu Richard hakuwahi kunipiga wala kunitusi, hakuwa mlevi wala mwanaume wa kutangatanga, kama ndoa za kawaida tulikuwa na changamoto zetu za kawaida, lakini tulipendana sana” Diana aliongeza.

“Mambo yalibadilika tarehe 14 Aprili Jumapili hio,kama saa tano hivi za usiku , Richard aliwasili nyumbani akiwa mlevi, ilikuwa mara yangu ya kwanza kumuona akiwa amelewa… alikuwa anatabia ambazo zilinichanganya sana, alisema…mpenzi nimerudi akijirudia rudia, pole nimechelewa ” Anakumbuka huku akishusha pumzi.

Sikutilia maanani sana nikasema…labda amelewa tu kama wanaume wengine.

Hata hivyo siku iliyofuata nilishangaa sana maana pia alirudi akiwa amelewa, ndipo nilipoanza kujiuliza ni nini ambacho kimembadilisha mume wangu?, anasema Diana.

Tarehe 16 Aprili, ilikuwa siku ya Jumanne, anakumbuka Diana. Mumewe aliingia chumbani alipokuwa ananyoosha nguo huku akiandamana na watoto wake wawili: ”Katika chumba hicho kuliwa na picha yake, akaitoa kwenye ukuta na kusema akifa angependelea hiyo picha itumiwe wakati wa mazishi yake”.

Diana anasema tukio hilo lilimshangaza sana na mumewe aliporudi usiku siku iliyofuata alimuuliza mumewe mbona alitamka maneno hayo mbele ya watoto wao?…jibu lake lilikuwa ni kicheko tu.

Siku ya mkasa Richard alirejea nyumbani saa mbili usiku na kuelekea katika chumba chake huku watoto wetu wakimfuata nyuma, Diana anasema kuwa mumewe hakuzungumza na mtu yeyote.

Diana alienda chumbani kuwaita watoto wake ili wale chakula cha jioni, naye Richard aliondoka tu ghafla, cha ajabu Diana anasema mumewe alibeba funguo zote za milango ya nyumba yao.

Jaribio lake kumpigia simu liliambulia patupu kwani mumewe hakujibu, alimwandikia arafa fupi ya kumuuliza yuko wapi?, lakini hakupata jibu. Akaamua kwenda kulala kama kawaida baada ya kuwalalisha watoto.

Ghafla aliamshwa na maumivu makali niliyoyahisi kichwani mwake: “Damu ilikuwa inatiririka kama maji huku mume wangu akinikatakata kwa panga mkononi… alikuwa na panga mkono mmoja na kisu mkono mwengine huku akiwa mlevi “Diana anasema na kuongeza kuwa, kutokana na maumivu hayo Diana alianguka kutoka kitandani hadi sakafuni, na mumewe aliondoka chumbani huku akidhani kuwa alikuwa amefariki.

Diana anasema kuwa alimsikia akimpigia mama yake mzazi simu akimueleza kuwa tayari amenitoa uhai na sasa anapanga kuwatoa uhai watoto wangu kisha yeye ajimalize, Ujumbe huo pia alimpatia babake Diana kamande kwa njia ya simu.

“Mume wangu aliemueleza baba yangu :”Utayalishe majeneza manne…kuna mazishi hivi karibuni “.

Baada ya kukamilisha mazungumzo yake kwa siku, Diana anakiri kuwa alisikia binti yake akipiga mayowe na kuangua kilio akisema: “baba usituue ”

Hapo ndipo Diana alipata nguvu na kuinuka kukimbia katika chumba cha watoto, anasema kuwa mume wake alikuwa amemshika binti yake Cathrine ambaye alikuwa anang’ang’ana kutoka mikononi mwake, huku binti yake wingine Praise akiwa amelala chali kitandani, mume wake akijiandaa kumdunga kisu.

Nilipaza sauti na kumuita “Richard!” anasema Richard ni kama sauti hiyo ilimshitua mumewe kwani aliangusha kisu alichokuwa amekishika mkononi, na watoto kuona hali hiyo wakatoroka.

Mume wake kwa haraka aliokota kisu kile na kumsukuma Diana kwenye ukuta alipomdunga kisu mkononi alipokuwa anajaribu kujikinga, katika hali ile Diana alifaulu kutoroka hadi nje.

Diana anakumbuka matamshi ya mumewe ya mwisho alipokuwa anamsihi arejee ndani ya nyumba :”Afadhali tufariki humu ndani, lakini kama hutaki, basi nenda ukafe huko nje; mimi nitakufa humu ndani.”

Majirani zake walimpeleka hospitalini, baadae Diana alipokea simu kutoka kwa majirani zake waliomueleza kuwa mumewe alijitoa uhai kwa kutumia kisu kile kile alichomdunga Diana. Kwa bahati alitoka hospitalini baada ya kupata matibabu kwa muda wa wiki mbili.

Kipindi kizito kilifuatia baada ya mazishi ya mumewe , Diana anasema kuwa alijihisi mpweke na aliyevunjika moyo .Alikuwa mwenye huzuni na simanzi kubwa na muda wote alijiuliza ni kwanini yote haya yalitokea kwake?.

”Watoto wangu walikuwa wananiuliza ni kwanini baba yetu alijitoa uhai? Na je atarudi tena?”, anasema Diana.

Siku hizo Diana anasema kuwa wengi wa miongoni mwa marafiki zake na hata jamaa kutoka familia ya mumewe walikuwa hawataki kujihusisha nae na huku wengine wakimshutumu kuwa yeye ndio chanzo cha kifo cha mume wake Richard.

Anasema: “Nakumbuka nikiwa nimelala kitandani hospitalini nikijiuliza iwapo ningefariki , watoto wangu wangeishia wapi?”.

Baada ya kupona, Diana kamande alianza shirika lisilokuwa la kiserikali ambalo limewaleta pamoja wajane na yatima.

Diana anasema kuwa ni rahisi kwa mtu anapotokewa na jambo kama hilo kujiona kama muathiriwa na kusalia katika lindi lile la hofu na huzuni , lakini yeye ameamua kuendeleza maisha yake na kutumia tukio hilo kuhamasisha jamii.

Pia aliweza kumsamehe mume wake ambaye anaamini kuwa kuna jambo ambalo lilimchochea kuchukua hatua ya kujiua, huenda asijue nini kilichomtoa uhai, lakini kwake yeye anamkumbuka mumewe wake kama mpenzi.

Chanzo BBC

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents