Habari

Kenya yalegeza vizuizi vya Virusi vya Corona kunusuru uchumi

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametangaza leo (Julai 6. 2020) mpango wa kufungua tena shughuli za kawaida nchini humo kwa kulegeza vizuizi vilivyowekwa kukabiliana na virusi vya corona.

Kenia Coronavirus Uhuru Kenyatta (PSCU)

Katika hotuba yake kwa taifa Rais Kenyatta amesema mpango huo utafanywa kwa awamu na utajumuisha kuruhusiwa kuanza tena kwa safari za ndege za kimataifa kuanzia Agosti mosi pamoja na kuondoa marufuku ya kusafiri ndani ya nchi.

Uamuzi huo unakuja wakati shinikizo linaongezeka nchini Kenya la kutaka shughuli za uchumi ziruhusiwe baada ya kudorora miezi minne tangu nchi hiyo ya Afrika Mashariki ilipoweka vizuizi vikali vya kukabiliana na virusi vya corona.

Vizuzizi vilivyopo vimeathiri kwa kiwango kikubwa sekta muhimu ikiwemo utalii ambao unaajiri mamilioni ya watu nchini Kenya na chanzo kikubwa cha fedha za kigeni.

Rais Kenyatta amesema “safari za ndege za kimataifa za kuingia na kutoka nchini Kenya zitarejea Agosti Mosi 2020” huku marufuku ya kuingia na kutoka mji mkuu Nairobi, mji wa pwani wa Mombasa na ule wa kaskazini mashariki wa Mandera inatondolewa mara moja kuanzia Jumanne ya Julai 7.

Kenyatta aonya vizuizi vinaweza kurejeshwa

Kenia Corona-Pandemie (picture-alliance/AP Photo/B. Inganga)

Hata hivyo rais Kenyatta amerefusha kwa siku 30 zaidi amri ya kutotoka nje usiku.

Kiongozi huyo ameonya kuwa hatosita kurejesha vizuizi vilivyopo iwapo hali ya mamabukizi ya COVID-19 itakuwa mbaya.

“Katika siku 21 zijazo tutatizama mwenendo wa muingiliano na kusambaa kwa virusi. Ikiwa kuna ishara zozote kuwa hali ya ugonjwa inakuwa mbaya hatutakuwa na uamuzi mwingine isipokuwa kurejesha vizuizi” amesema rais Kenyatta katika sehemu ya hotuba yake.

Hadi Jumatatu ya Julai 6,  Kenya imethibitisha karibu visa 7,900 vya virusi vya corona na vifo 160.

Mlipuko huo umeutikisa uchumi wa nchi hiyo huku wizara ya fedha ikisema janaga la COVID-19 litasababisha kuanguka kwa ukuaji wa uchumi hadi asilimia 2.5 mwaka 2020 kutoka ukuaji wa asilimia 5.4 mwaka uliopita.

Chanzo DW Swahili

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents