Habari

Kenyatta: “Hatuwezi kuendelea kusema Wakenya tukae ndani kwa ajili ya Corona, Uchumi wetu utazorota”

Rais Uhuru Kenyatta ametangaza mipango ya kusaidia biashara na raia kusonga mbele katika kipindi hiki cha mdororo wa kiuchumi kwasababu ya janga la virusi vya corona.

Rais amehutubia taifa kutoka Ikulu ya rais, Nairobi na kusema kwamba mipango hiyo itagharimu shilingi bilioni 53.7.

Katika hotuba yake, rais alisema pesa hizo zitagawanywa katika sekta muhimu kama vile miundo mbinu, elimu, biashara ndogo ndogo na za wastani, afya, kilimo, utalii, mazingira na viwanda vya uzalishaji.

Aidha, rais amesema kuwa taifa hilo haliwezi kuendelea kuchukua hatua za kusalia ndani milele.

”Sisi kama serikali, kama serikali zingine, mataifa yote dunia zimeanza kuona, hatuwezi kuendelea kusema wakenya tukae nyumbani, hatuwezi kuendelea kusema tu wakenya msiende kufanya biashara, musiende makazi, namna hio. Lakini, ile kitu ambayo itatusaidia pia kwa kikamilifu kuhakikisha ya kwamba tumeweza tena kufungua uchumi wetu na wananchi waweze kuendelea na maisha yao ya kawaida. Nimewaambia wenzangu, hii haitakuwa kwa sababu ya yale serikali itatenda, itakuwa kwa sababu ya yale kila mmoja wetu kwa kibinafsi atafanya”.

Kenya inachukua hatua sawa na zile ambazo pia zimechukuliwa na nchi nyengine kama hatua ya kuchechemua uchumi unaoendelea kudidimia.

Uhuru amesema hayo wakati ambapo pia alitangaza kuwa Kenya maambukizi 31 ya virusi vya corona na kufikisha idadi hiyo hadi 1192.

“Hadi kufikia sasa tumepima watu 57,640 ambapo 1192 wamethibitishwa kuambukizwa na wengine karibia 50 wakipoteza maisha yao kwasababu ya ugonjwa huu,” rais alisema.

”Mimi sina shaka Wakenya tukishirikiana, tuungane pamoja, tutashinda huu ugonjwa. Lakini tena leo wakati natoa hii hotuba ambayo tumetoa sasa ya kusema lengo mbali mbali ambayo serikali inachukua kurahisisha maisha ya wananchi wa kawaida na kuhakikisha ya kwamba wananchi bado wanaweza kuendelea na maisha yao kupitia hio stimulus package ambayo nimeitaja, lazima tukumbuke ya kwamba jukumu ni letu sisi sote”.

Alieleza raia wa Kenya kwamba ikiwa wataendelea kutekeleza masharti yaliyowekwa bila shaka taifa hilo litafanikiwa kukabiliana na changamoto zilizopo kwa sasa.

Kama hatua moja ya kuhakikisha usalama wa kila mmoja, wadau mbalimbali ikiwemo mawaziri na maafisa wa afya, wameagizwa kuanza kuwaeleza wakenya kwamba hawatasalia ndani milele.

Rais aliendelea kusihi raia kuwa kila mmoja anajukumu la kuhakikisha usalama wake na wengine.

”Wewe uko na jukumu la kuhakikisha umechunga mwenzako, tukianza kupanua na kufungua uchumi wetu, wewe ujue ya kwamba, usipotii masharti ambayo tumepatiwa, sio wewe pekee yako utaumia, unaumiza pia mwenzako kwa kazi ambayo unafanya. Ukienda nyumbani umeumiza mama, umeumiza mtoto”.

”Itafika wakati tutafungua taifa letu na wakati wa kufungua, jukumu sasa itarudi kwako, itarudi kwangu kibinafsi. Kuhakikisha ya kwamba umejilinda, umelinda wale unapenda, na unalinda wale mnafanya kazi pamoja na wao”.

Rais Uhuru Kenyatta ameonyesha kwamba njia moja ya kukabiliana na changamoto hii kwa muda mfupi, nchi hiyo inapanga kurekebisha barabara na miundo mbinu mingine.

Aliongeza kwamba bilioni 5 zimetengwa kwa ajili ya wenyeji kupata ajira zitakazoibuka katika utekelezaji wa mipango hiyo.

Pia serikali imetoa bilioni 6.5 kwa Wizara ya Elimu kuajiri waalimu zaidi 10,000 huku akitangaza kuwa serikali itanunua magari yaliyotengenezwa ndani ya nchi hiyo kiasi cha milioni 600 kukuza viwanda vya utengenezaji magari nchini humo.

Aprili mwaka huu, rais Uhuru Kenyatta alitangaza kusitishwa kwa shughuli za usafiri katika kauni za Nairobi, Kilifi, Kwale na Mombasa. Hatua nyengine iliyochukuliwa ni kusalia ndani kuanzia saa moja usiku hadi kumo na moja asubuhi.

Rais amesema asilimia 82 ya ugonjwa wa Covid-19 ni kutoka Nairobi huku kaunti zingine za Mombasa zikirekodi asilimia 14.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents