Kibaki ageukwa

DALILI zimeanza kujitokeza kuonyesha kuwa siku za utawala wa Rais Mwai Kibaki wa Kenya zinahesabika baada ya Jumuiya ya kimataifa, waangalizi wa uchaguzi na baadhi ya makamishna wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK) kubainisha kuwa ushindi wake una mushkeli.

na Peter Nyanje, Irene Mark na Saada Said


DALILI zimeanza kujitokeza kuonyesha kuwa siku za utawala wa Rais Mwai Kibaki wa Kenya zinahesabika baada ya Jumuiya ya kimataifa, waangalizi wa uchaguzi na baadhi ya makamishna wa Tume ya Uchaguzi ya Kenya (ECK) kubainisha kuwa ushindi wake una mushkeli.


Katika hali inayoonyesha kuwa ushindi huo wa Kibaki unaweza kuwa wa muda mfupi tu, waangalizi wa uchaguzi huo kutoka Umoja wa Ulaya (EU), walibainisha jana kuwa uchaguzi huo ulikuwa umeharibika na haukuwa na sifa za kuitwa uchaguzi huru katika viwango vya kimataifa.


Timu hiyo ya waangalizi ilikwenda mbali zaidi na kuanza kudai ukaguzi huru wa matokeo ya uchaguzi, hasa katika nafasi ya urais.


Hayo yanatokea wakati mauaji nchini humo yanaongezeka, kukiwa na taarifa za kuuawa kwa watu waliokuwa wamejificha katika kanisa moja huko Eldoret.


Hayo yanatokea wakati vurugu zinapamba moto na kuongeza idadi ya vifo huku watu wanaokimbia vurugu hizo wakipiga hodi katika Kisiwa cha Pemba.


Mkuu wa waangalizi wa uchaguzi kutoka Umoja wa Ulaya (EU), Alexander Graf Lambsdorff, akiwa amembatana na Graham Elson, waliwaambia waandishi wa habari kuwa ingawa Wakenya walikuwa na matumaini makubwa na uchaguzi huo, lakini haujafikia viwango vya kimataifa.


“Lakini ni juu ya Wakenya kuamua hatua wanazotaka kuzichukua baada ya kupitiwa upya kwa matokeo,” alisema.


Awali, Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, aliwapigia simu Kibaki na mgombea wa upinzani aliyeelezwa kushindwa, Raila Odinga, na kuwataka kutafuta suluhisho la matatizo yaliyoikumba nchi hiyo na kusababisha vifio vya watu kadhaa.


Tayari ushahidi umeshaanza kutolewa unaoonyesha kuwa kulikuwa na tofauti katika idadi ya kura za urais zilizotangazwa na ECK na ile iliyopatikana katika vituo. Kwa mfano, matokeo kutoka Maragwa yalikataliwa kwa sababu idadi ya waliopiga kura ilionekana kuzidi ya waliojiandikisha.


Huko Molo, wasimamizi waliyakataa matokeo yaliyotangazwa na ECK wakidai kuwa idadi ya kura za urais ilikuwa imeongezeka kwa kura 20,000.


Akifafanmua kuhusu hilo, Lambsdorff alisema wakati wasimamizi katika kituo hicho walitangaza kuwa Rais Kibaki alikuwa amepata kura 50,145 matokeo yaliyotangazwa na ECK mjini Nairobi yalionyesha kuwa Kibaki alikuwa amepata kura 75,261 katika kituo hicho.


“Kutokana na kasoro hizi na nyinginezo, kuna mashaka makubwa iwapo matokeo yaliyotangazwa yanawakilisha hali halisi,” alisema.


Wakati huo huo, makamishna wanne wa ECK, nao wameonyesha wasiwasi juu na matokeo hayo ingawa serikakli imekuwa ikisisitiza kuwa hakukuwa na kasoro zozote katika uchaguzi huo.


Walipendekeza kuundwa kwa tume huru itakayochunguza iwapo matokeo ya kura za urais yalichezewa kabla ya kutangazwa.


Walikubaliana na madai yanayotolewa na wasimamizi kuwa kulikuwa na kasoro nyingi katika matokeo na kubainisha kuwa madai yaliyotolewa na ODM kuwa wameibiwa kura yana uzito.


Makamishna hao, Jack Tumwa, Daniel Ndambiri, Samuel arap Ng’eny na Jeremiah Matagaro, walisema kuwa Wakenya wameguswa na kilichotokea na wasingeweza kunyamaza kimya.


Kwa upande wao, waangalizi wa ndani nao walieleza kasoro kadhaa ikiwamo kutofautiana kwa idadi ya kura kati ya zile zilizotangazwa na ECK na matokeo yaliyokusanywa kutoka katika vituo vya kupigia kura.


Tumwa alisema ECK lazima ibebe lawama kutokana na kilichotolea, ingawa haina uwezo wa kutengua matokeo iliyoyatangaza.


Wakati huo huo, mauaji yanayotokana na vurugu zilizoibuliwa na matokeo ya uchaguzi, yaliendelea na kulikuwa na ripoti kuwa watu 18 waliuawa huko Mombasa na Eldoret usiku wa kuamkia jana.


Hali imetulia katika Jiji la Nairobi lakini maduka mengi yalikuwa yamefungwa. Kulikuwa na upungufu wa mafuta hasa ya opetroli kutokana na kufungwa kwa vituo vingi au kuishiwa bidhaa hiyo.


Wakati huo huo, Marekani na nchi nyingine za Magharibi zimeelezea kutoridhishwa na matokeo ya uchaguzi huo na kuwataka wanasiasa nchini humo kufanya kila linalowezekana kukomesha vurugu.


Marekani, Uingereza na EU zilipongeza hatua za upigaji kura na kuwasifia Wakenya kwa kupiga kura kwa utulivu lakini sasa wanaelezea wasiwasi wao katika matokeo yaliyotangazwa, ambayo yamempa Rais Kibaki ushindi dhidi ya Odinga wa ODM na wagombea wa vyama vingine vinane.


Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, David Miliband, aliwataka viongozi wa Kenya kuchukua hatua zinazofaa kumaliza matatizo hayo.


“Huu ni muda muhimu sana kwa Kenya. Ni muhimu shughuli zote za uchaguzi ziwaridhishe watu wote wa Kenya,” alisema.


Wakati huo huo, Serikali ya Kenya imeunda kamati tatu kwa ajili ya kushughulikia matatizo yaliyojitokeza baada ya uchaguzi.


Pamoja na kuunda kamati hizo, tayari serikali imeanza kuwasiliana na ODM kuona jinsi matatizo hayo yanavuyoweza kumalizwa.


Lakini hilo linaonekana kuwa gumu kutokaan na sharti lililowekwa na Odinga kuwa hatokubali kukutana na Kibaki iwapo ataendelea kung’ang’ania wadhifa wa urais.


“Kukutana naye kama rais ni sawa na kukubali kuwa yeye ni mshindi, hilo haliwezekani, kwa sababu wote tunafahamu kuwa hajashinda kihalali,’ alisema.


Aidha, Odinga alisisitiza kufanyika kwa maandamano ya amani nchi nzima kesho, akisema kuwa anatarajia vyombo vya dola vitaheshimu hatua hiyo itakayochukuliwa na wananachi.


Alionya kuwa hatua hiyo ya kutumia nguvu ya umma haitakoma mpaka matatizo yote ya uchaguzi yatakapopatiwa ufumbuzi.


Wakati huo huo, vurugu ziliendela katika maeneo mbalimbali huku kukiwa na taarifa kuwa takriban watu 50 walifariki baada ya kanisa walimokimbilia kujihifadhi kuchomwa moto.


Kundi la watu walilivamia kanisa hilo katika mji wa Eldoret, ambalo lilikuwa limehifadhi mamia ya ‘wakimbizi’ hao, walisema polisi.


Watu wengine kadhaa waliungua vibaya na kukimbizwa hospitali. Inadaiwa kuwa waliouawa na watu wa kabila la Kikuyu ambao walivamiwa na Waluo.


Kwa mujibu wa taarifa zinazokusanywa, idadi ya vifo inaweza kuwa zaidi ya 250 hadi jana mchana.


Wakati huo huo, siku chache baada ya kuzuka kwa ghasia za kisiasa nchini Kenya, raia kadhaa wa nchi hiyo wameanza kuingia kisiwani Pemba wakikimbia ghasia hizo ambazo zimesababishwa na uchaguzi mkuu.


Wenyeji wa kisiwani Pemba walidai kuwa wamewaona wananchi mbali mbali, wengi wao wakiwa kina mama na watoto, wakishuka katika maboti na majahazi maalumu kutoka nchini Kenya. Walisema wameanza kuwapokea wakimbizi, hasa kutoka maeneo ya Mombasa.


Raia hao wa Kenya wanadaiwa kuingia kupitia pwani ya kaskazini ya Kisiwa cha Pemba katika vijiji vya Msuka na Micheweni, ambavyo vinakaribiana na Mombasa.


Wakimbizi hao wanadaiwa kutoka katika miji ya Mombasa, Lamu na Malindi.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Ali Omar, alisema kuwa hawana taarifa zozote hadi sasa za kuwepo wakimbizi kutoka Kenya katika mkoa wake, lakini aliahidi kufuatilia suala hilo kwa kina.


Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini Kabwe Zitto (Chadema), amejiunga katika juhudi za kusaka amani nchini Kenya kwa kumtaka Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Yoweri Museveni wa Uganda kuitisha mkutano wa dharura, ili kutafuta ufumbuzi wa ghasia nchini Kenya.


Zitto amelipitisha ombi lake hilo kwa Katibu wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC), Balozi Juma Mwapachu.


Katika barua hiyo, Zitto anawashauri viongozi wa jumuiya hiyo kuchukua hatua za haraka kutuliza ghasia na umwagikaji wa damu nchini Kenya.


Ilieleza kuwa si busara kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo kulifumbia macho tatizo la Kenya na kutaka wawakilishi wa vyama vya ODM na PNU waalikwe katika mkutano huo.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents