Kifo cha Raisi wa Zambia Utata

Rais wa Zambia Mheshimiwa levy Mwanawasa ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, amedaiwa kufariki dunia jana asubuhi akiwa hospitalini jijini hapa

Mwanawasa_1.jpg

 

Rais wa Zambia Mheshimiwa levy Mwanawasa ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, amedaiwa kufariki dunia jana asubuhi akiwa hospitalini jijini hapa.

Mauti hayo inadaiwa yalimkuta Rais Mwanawasa baada ya kuugua kiharusi tangu mwanzoni mwa wiki hii, hasa baada ya kulalamikia maumivu makali kifuani.

Hayo yalielezwa jana na Msemaji wa Ubalozi wa Zambia nchini hapa, ingawa hakukuwa na tamko lolote kutoka kwa maofisa wa Zambia.

Aidha Rais Mwanawasa (59), alikimbizwa hospitalini Jumapili wiki iliyopita, alipokuwa mjini Sharm-el-Sheikh, Misri, baada ya kuugua kiharusi ghafla kabla ya kuhudhuria Mkutano wa Kawaida wa 11 wa Umoja wa Afrika (AU).

Ilielezwa kuwa alihamishiwa jijini hapa kwa matibabu zaidi na uchunguzi na baada ya hapo alifariki dunia. Rais Mwanawasa kabla ya kifo chake alikuwa ndiye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), ambayo imekuwa msuluhishi mkuu katika mgogoro wa kisiasa unaoikumba Zimbabwe.

Kiongozi huyo aliwahi kuugua kiharusi mwaka juzi, lakini kabla ya kuchaguliwa tena mwaka huo, alithibitisha kuwa afya yake ni salama na hana tatizo lolote.

Alitarajiwa kutoa msimamo wake mkali dhidi ya uchaguzi wa Zimbabwe katika mkutano wa AU, ambako alipangiwa kukaa jirani na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe, kwa mujibu wa alfabeti za majina.

Kiongozi huyo alisikitishwa na kitendo cha kiongozi wa upinzani nchini Zimbabwe, Bw. Morgan Tsvangirai, kulazimika kujiondoa katika kinyang’anyiro cha urais, kutokana na vitisho dhidi ya wafuasi wake.

Hata hivyo, habari kutoka Lusaka, Zambia, zilimkariri Makamu wa Rais akikanusha habari za kifo cha Rais Mwanawasa akisema bado anaendelea na matibabu hospitalini Paris.

"Rais jana alilala vizuri katika hospitali ya kijeshi ya Percy Ufaransa. Habari zilizotangazwa … si za kweli," alisema Makamu wa Rais, Bw. Rupiah Banda, katika taarifa yake.

Mapema jana, kituo cha redio cha Talk Radio 702 cha Afrika Kusini, kilitangaza kuwa Rais Mwanawasa amefariki dunia kikiukariri Ubalozi wa Zambia nchini humo.

Akiungwa mkono na Waziri wa Habari wa Zambia, Bw. Mike Mulongoti, Bw. Banda alisema Rais Mwanawasa alikuwa akitibiwa shinikizo la damu.

"Madaktari wanaomhudumia wameridhishwa na maendeleo yake na hali yake inaendelea vizuri. "Ameendelea kupata matibabu ya shinikizo la damu katika Chumba cha Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU) na hakuna mabadiliko yoyote," alisema Bw. Banda.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents