Siasa

Kikwete kuteta na Raila, Kibaki

RAIS Jakaya Kikwete, amesema anaguswa na mauaji yanayotokea Kenya na kwamba anaangalia uwezekano wa kufanya mazungumzo na wanasiasa, Mwai Kibaki, aliyetangazwa kuwa mshindi na Raila Odinga, aliyepinga matokeo.

RAIS Jakaya Kikwete, amesema anaguswa na mauaji yanayotokea Kenya na kwamba anaangalia uwezekano wa kufanya mazungumzo na wanasiasa, Mwai Kibaki, aliyetangazwa kuwa mshindi na Raila Odinga, aliyepinga matokeo.


Akizungumza katika mahojiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) juzi, Rais Kikwete, alisema kwa sasa yeye na viongozi wenzake wa Afrika Mashariki wanawasiliana kuona jinsi wanavyoweza kusaidia kuepuka madhara zaidi kwa wananchi.


Kikwete alisema pamoja na kuwa kuna Watanzania wengi wanaoioshi Kenya, anaguswa pia na vifo vya watu wengine ambao si Watanzania kwa kuwa wote ni binadamu.


Kikwete alisema hakuweza kwenda Kenya kushiriki katika kuapishwa kwa Kibaki kutokana na hali ilivyokuwa lakini alikiri kupokea mwaliko huo mapema zaidi.


Alisema walipata mwaliko kama ilivyo taratibu za nchi zote mwaliko ambao ulionyesha kwamba sherehe za kuapishwa zingeweza kuwa kati ya Desemba 29 na 30, 2007.


Rais Kikwete alisema ataendelea kuwasiliana na wanasiasa hao wa Kenya, kwa nia ya kuhakikisha kunakuwapo mazungumzo katika kumaliza mzozo ambao ukiachwa kama ulivyo unaweza kusababisha maafa makubwa zaidi kwa raia wasio na hatia.


Hivi sasa Kenya imeingia katika machafuko na tayari zaidi ya watu 100 wamekwishapoteza maisha katika machafuko yaliyotokea baada ya Tume ya Uchaguzi ya Kenya kumtangaza Kibaki wa chama cha PNU kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa kura milioni 4.5 dhidi ya zile za Raila milioni 4.3.


Muda mfupi baada ya Kibaki kutangazwa, aliapishwa harakaharaka katika Ikulu ya Nairobi katika sherehe ambazo hazikuhudhuriwa na mgeni yeyote zaidi ya watu walio karibu naye huku ulinzi mkali wa majeshi na polisi ukiimarishwa.


Baada ya taarifa za kuapishwa kwa Kibaki, Raila alitangaza kwamba tukio hilo ni sawa na mapinduzi ya kijeshi na kwamba hawezi kukubaliana na matokeo hayo kutokana na kudhihirika kuwapo kwa ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi.


Wafuasi wa Raila waliandaa mkutano juzi Jumatatu ambao walisema wangemuapisha “Rais wa watu” , lakini vurugu na mauaji yaliyoendelea kuamkia siku hiyo na kuendelea hadi asubuhi na hivyo kusababisha kuahirishwa kwa mkutano huo.


Mkutano huo uliopangwa kufanyika katika viwanja vya Uhuru Park, sasa umepangwa kufanyika kesho Alhamisi, lakini haijafahamika kama polisi wataruhusu tena kufanyika kwake.


Source: Raia Mwema

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents