Siasa

Kikwete, Salma wamkuna mke wa Rais Bush

MKE wa Rais wa Marekani, Bibi Laura Bush amempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kuongoza kameni ya upimaji virusi vya UKIMWI kwa hiyari.

Na Mwandishi Wa Majira


MKE wa Rais wa Marekani, Bibi Laura Bush amempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kuongoza kameni ya upimaji virusi vya UKIMWI kwa hiyari.


Katika ujumbe aliomtumia Rais Kikwete mwishoni mwa wiki na kutolewa na Ikulu kwa vyombo vya habari jana, Bibi Laura, alisema, Tanzania imechukua hatua muhimu katika historia baada ya kuzindua Kampeni ya Kitaifa ya Kupima VVU Julai 14 mwaka huu.


Bi. Laura alisema, juhudi za Rais Jakaya Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete katika mapambano dhidi ya UKIMWI ni mfano wa kuigwa na viongozi wengine wa Afrika na dunia kwa ujumla.


Bibi Laura aliahidi kuwa,Serikali ya Marekani itatoa dola milioni 205 mwaka huu, kwa ajili ya kufadhili shughuli za upimaji VVU ili kusaidia kufanikisha kuwepo kwa “Tanzania bila UKIMWI.”


Alisema, Rais Kikwete na mke wake mama Salma, wamechukua hatua kubwa ya kupiga vita ugonjwa wa UKIMWI kwa kitendo chao cha kuongoza kampeni hiyo ya upimaji.


Aliwataka Watanzania kuheshimu ushauri uliotolewa na Rais Kikwete katika hotuba aliyoitoa, kwamba waache kunyanyapaa na kuwafedhehesha watu wanaoishi na VVU/ UKIMWI.


Bibi Laura alisema, “Serikali ya Marekani inajisikia fahari kuwa mshirika wa Tanzania katika kupiga vita VVU/UKIMWI pamoja na kutoa ushauri nasaha.”


Mwaka 2006, Serikali ya Marekani ilijitolea kusaidia shughuli ya upimaji na utoaji ushauri nasaha katika takribani vituo 200 vilivyowafikia takribani watu 400,000 nchini Tanzania.


“Mwaka huu, tunafanya kazi pamoja nawe katika kuongeza idadi ya wanaopima VVU ili ifikie watu takribani 700,000,” aliahidi Bibi Laura katika barua hiyo ya pongezi kwa Rais Kikwete.


“Tumeamua kufanya kazi pamoja na Serikali yako katika kuzuia maambukizi mapya ya VVU/UKIMWI na kuwapatia matibabu wanaoishi na ugonjwa huo nchini Tanzania.”


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents