Siasa

Kikwete sasa ‘awavaa’ rasmi Kibaki, Odinga

MWENYEKITI wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Kikwete, yuko Kenya kusaidia juhudi za kurejesha amani nchini humo.

Na Mwandishi Wa Majira

 

MWENYEKITI wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Jakaya Kikwete, yuko Kenya kusaidia juhudi za kurejesha amani nchini humo.

 

Rais Kikwete aliondoka nchini jana baada ya kuombwa na pande zinazohusika na mgogoro unaoitafuna Kenya, akiwamo mpatanishi mkuu, Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN), Bw. Kofi Annan.

 

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais na Habari, Bw. Salvator Rweyemamu, ilisema Rais Kikwete atakuwa Kenya kwa siku mbili.

 

Ilisema katika ziara hiyo ya kikazi, atakutana na kwa mazungumzo na Bw. Annan, Rais Mwai Kibaki wa Kenya na kiongozi wa chama kikuu cha upinzani cha Orange Democratic Movement (ODM), Bw. Raila Odinga.

 

Bw. Annan amekuwa kwa muda sasa akiongoza juhudi za upatanishi katika mgogoro huo ulioanza Desemba 30 mwaka jana, baada ya kutangazwa matokeo yaliyompa ushindi Rais Kibaki na kusababisha vurugu na mauaji ya watu zaidi ya 1,000.

 

Katibu Mkuu huyo mstaafu wa UN amekuwa akisaidiana na Rais mstaafu wa Tanzania, Bw. Benjamin Mkapa, na mke wa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Bw. Nelson Mandela, Bibi Graca Machel. Rais Kikwete anatarajiwa kurejea nchini leo.

 

Suala kubwa ambalo linasababisha mvutano katika mazungumzo hayo ni majukumu ya Waziri Mkuu ambaye pande mbili zimekubaliana cheo hicho kiwepo, huku upande wa upinzani ukitaka awe na nguvu za kusimamia Baraza la Mawaziri.

 

Wakati wapinzani wakitaka Katiba ibadilishwe ili kipengee cha majukuimu ya Waziri Mkuu kiingizwe, upande wa Serikali unashikilia Katiba ibaki vile vile kwa maana ya Rais kuwa na nguvu zaidi za kiutendaji kuliko Waziri Mkuu.

 

 

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents