Michezo

Kilimanjaro Vs Zanzibar utakuwa mchezo mgumu – Ninje

Kocha Mkuu wa Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, Ammy Conrad Ninje amepanga leo siku ya Jumanne Desemba 5, 2017 kuanza kuyafanyia kazi mapungufu yote yaliyojitokeza kwenye mchezo wao dhidi ya Libya uliofanyika Jumapili Desemba 3, mwaka huu.

Akizungumzia mchezo unaofuata dhidi ya Zanzibar Heroes, Ninje amesema utakuwa mgumu kama ambavyo historia inaonesha wakati timu hizo mbili zinapokutana.

“Kuanzia mazoezi ya leo nitaiandaa timu kupata ushindi na nimepanga kwenda kuitazama Zanzibar itakapocheza mchezo wake dhidi ya Rwanda,” amesema.

Amesema ataiangalia Zanzibar Heroes kiufundi ili kubaini upungufu wao ili naye ajue namna atakavyoweza kutumia nafasi hizo kwenye mchezo unaofuata.

“Ni fahari kwa timu zetu hizi mbili kila mmoja kupambana kupata pointi bahati nzuri wao wanacheza kesho kwa hiyo mchezo wao nitautumia kutazama mapungufu (upungufu wao) yao yatakayoweza kutusaidia,’’ alisema Ninje.

Kilimanjaro Stars hii leo itaanza mazoezi rasmi kujiandaa na mchezo huo unaofuata.

Kilimanjaro Stars ipo kundi A pamoja na timu za Zanzibar, Libya, Rwanda na wenyeji Kenya.

Kenya wana pointi tatu baada ya kuifunga Rwanda mabao 2-0 wakati Kilimanjaro Stars na Libya wana pointi 1 kila mmoja baada ya kutoka sare ya bila kufungana kwenye mchezo wao wa kwanza wakati Zanzibar na Rwanda wenyewe hawana pointi huku Zanzibar ikiwa haijashuka dimbani katika kundi hilo.

Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Kenyatta ulioko Machakos nchini Kenya, Tanzania Bara ilipata sare katika safari ya kuwania Kombe la Cecafa dhidi ya Libya.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents