Michezo

Kimwaga na Shaaban wanaendelea vizuri – Mwankemwa

Nyota wawili wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Joseph Kimwaga na Shaaban Idd, waliomajeruhi hali zao zinaendelea vyema kabisa baada ya kufanyiwa upasuaji mwezi uliopita.

Idd alifanyiwa upasuaji wa msuli uliochanika wa paja lake la mguu wa kulia pamoja na tatizo la henia huku Kimwaga naye akifanyiwa upasuaji wa goti la mguu wa kulia, wote wakipata matibabu hayo nchini Afrika Kusini.

Daktari Mkuu wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa, ameuambia mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa Kimwaga anatarajia kuanza mazoezi mepesi (Pysiotherapy) Oktoba 21 mwaka huu.

“Kimwaga atakwenda na mazoezi hayo madogo madogo na tunatarajia kwamba Kimwaga baada ya miezi miwili kupita ndipo ataruhusu kuanza kupiga mipira na vitu vingine vidogo vidogo na baada ya miezi mitatu ataweza kurudi tena uwanjani,” alisema.

Kuhusu maendeleo ya Idd, Daktari huyo bingwa wa tiba za michezo na za kawaida alisema kuwa Shaaban Idd, bado ataendelea kupatiwa matibabu nchini Afrika Kusini kwa muda wa mwezi na nusu kabla ya kurejea nchini baada ya kukaa huko kwa kipindi cha miezi miwili.

“Kwa sababu Shaaban hivi sasa atakuwa amekaa miezi miwili kule tunafanya taratibu aje kidogo nchini angalau siku 10 za kuweza kuiona familia yake kabla ya kurejea tena kwenye matibabu,” alisema.

Aidha, majeruhi wengine kipa Razak Abalora na kiungo Stephan Kingue, tayari wameanza mazoezi na wenzao jana Jumatatu jioni tayari kabisa kuanza maandalizi ya kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Mwadui utakaofanyika Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga Jumamosi hii Oktoba 14.

Abalora alipata mchubuko mkubwa kwenye paja lake kwenye mchezo uliopita wa Azam FC dhidi ya Singida United ulioisha kwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, naye Kingue alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya mgongo.

Kuelekea mchezo huo dhidi ya Mwadui, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam kikiwa na wachezaji wake wote kesho Jumanne alfajiri tayari kabisa kuifuata Mwadui mkoani Shinyanga.

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents